Misaada mingine inadhalilisha taifa


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 02 June 2009

Printer-friendly version

ZAMANI Tanzania iliweza kuwaambia Waingereza (waliotutawala) na Wamarekani, kwamba waende kuzimu wakipenda, kuliko Waafrika kuwekwa katika utwana.

Tulifanya hivyo kwa kujiamini, tena wakati Tanzania ikiwa katika mstari wa mbele katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, harakati ambazo ilijitolea kwa hali na mali. Watanzania walikufa Msumbiji na Zimbabwe.

Mimi sikumbuki iwapo Jakaya Kikwete, baada tu ya kuingia madarakani, aliwahi kutoa tamko bila kigugumizi, la kumshambulia George Bush kuhusu mauaji ya raia wasiokuwa na hatia huko Iraq na Afghanistan.

Lakini sababu ya hiyo ilikuja kujulikana miaka miwili baadaye, pale Bush alipoitembelea Tanzania katika ziara ambayo ilikuwa na kila aina ya kero, manyanyaso na udhalilishaji kwa wananchi kuliko manufaa.  

Ni ukweli usiopingika kwamba tangu tulipojipatia uhuru katika miaka ya 60, urafiki kati ya Tanzania na Marekani haukuwa mzuri, na hii ilitokana na msimamo wa nchi yetu kuhusu masuala ya ukombozi wa Bara la Afrika na kutetea wengine waliokuwa wanapigania haki zao.

Uswahiba kati ya Tanzania na Marekani umekuja siku za mwisho za Bush – wakati kura za maoni nchini humo kuhusu utendaji wake zikionyesha ulikuwa chini kuliko marais wote kwa miaka 50 iliyopita.

Kwa maneno mengine, wakati Wamarekani wenyewe walikuwa wanamdharau Bush kutokana na ubabe wake wa kivita, sisi ndio tukaanza kumuona ni mtu wa maana na hivyo kuwa swahiba mkubwa. Tulijali zaidi fedha kuliko utu.

Zamani tuliweza kuwaunga mkono watu wengine duniani, waliokandamizwa, kama vile Wapalestina, tena katika vikao vya Umoja wa Mataifa, ambako tulikuwa tunapinga maazimio ya Marekani na wenziwe wa nchi za Magharibi.

Leo hii hatuwezi kamwe kufanya hivyo. Lazima kwanza tuwasome sana akina Barrack Obama usoni ili wasije wakakasirika na kutunyima misaada ya kutuwezesha kupumua.

Kwa mfano, leo hii viongozi wetu hawawezi kukemea nchi za Magharibi; wanaogopa kukatiwa misaada inayotufanya tuishi, pamoja na kuwa na tani za dhahabu, kiasi kikubwa tukiwapa karibu na bure.

Tunaruhusu wizi huu ili tupewe msaada. Kwa mfano, kuna ahadi ya dola 700 milioni za msaada kutoka Marekani, fedha ambazo tunaambiwa nchi hiyo haijatoa kwa zaidi ya mwaka sasa.

Wakati tulipokuwa tunamnyooshea bakuli Bush aweke dola hizo, habari zilianza kuvuja kuwa mabilioni ya shilingi ya wananchi – tena zaidi ya hizo dola milioni 700, yalikuwa yameibwa na wajanja wachache, wakisaidiwa na wakubwa serikalini.

Mabilioni mengi yalipitia mikondo ya Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), makampuni ya Meremeta, Richmond, ujenzi wa minara pacha BoT, ununuzi wa rada, ndege ya Rais na mkataba usio halali na kampuni ya Alex Stewart na mingine mingi.

Lakini tunashuhudia Rais Jakaya Kikwete akienda Marekani mara kwa mara. Ziara yake ya hivi karibuni ilikuwa, pamoja na mambo mengine, kufuatilia ahadi za misaada alizotoa Bush.

Kufuatana na taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari vya Marekani, kuhusu mazungumzo ya Kikwete na Obama, ni kwamba Obama hakutoa ratiba kamili ya kutoa fedha hizo, bali alisisitiza kwamba michakato ya miradi itakayogharimiwa na msaada huo iharakishwe ili fedha zitolewe.  

Bush mwenyewe, wakati wa ziara yake nchini, alikaririwa akisema nchi yake haiwezi kutoa misaada kwa serikali ambazo zinalea ufisadi.

Hizo fedha za misaada hazitakabidhiwa Hazina ya Tanzania bali zitasimamiwa na Marekani yenyewe chini ya Shirika la Millennium Challenge Corporation (MCC).

Tukiacha zile taarifa za kawaida zilizokuwa zinatolewa na pande zote mbili, na ambazo zilikuwa zinasambazwa na vyombo vya habari vya serikali hapa nchini, masuala mengi mazito yalizuka katika mazungumzo ya Obama na Kikwete.

Hakujapatikana uthibitisho, lakini taarifa zinasema mazungumzo yao yaligusa hata suala la Mgogoro wa Zanzibar na vita dhidi ya ufisadi nchini.

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinaendelea kuwa tegemezi pamoja na kuwa na rasilimali kemkem. Harakati zinazoendelea hivi sasa, za wananchi kudai malipo halisi ya rasilimali zao, ni dalili inayoonyesha kwamba hali hii inatakiwa ikome, ingawa viongozi bado wameweka nta kwenye masikio.

Hivi sasa nchi yetu siyo tu inashindwa kabisa kusimamia kwa dhati kujenga uchumi wake, bali kwa kutegemea nchi za nje. Inashindwa hata kusimamia mustakabali wa maendeleo yake.

Kuomba kuna masharti yake. Mtu aombe ili kuziba pengo la muda na kuanzia hapo atafute jinsi ya kujitegemea.

Lakini Tanzania inaendelea kuomba na kudhalilishwa na misaada midogo kama ule wa dola 700 milioni; fedha ambazo zingepatikana kutoka makusanyo ya mwezi moja jijini Dar es Salaam.

0
No votes yet