Misingi ya kutaifisha Dowans hii


Tundu Lissu's picture

Na Tundu Lissu - Imechapwa 02 March 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

KUNA hoja mbili kuu za kisheria zinazoweza kutumika kutaifisha mitambo ya kampuni ya kufua umeme ya Dowans. Kwanza, kutaifisha kwa kulipa fidia. Pili, kutaifisha bila kulipa chochote.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imeweka “Malengo muhimu na misingi ya mwelekeo wa shughuli za serikali kuwa ni pamoja na ustawi wa wananchi.”

Katiba pia imewapa wananchi haki mbalimbali na wajibu. Kwa mfano, ibara ya 24(1) ya katiba inatoa haki ya kumiliki mali na hifadhi ya mali hiyo na “... ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang’anywa mali yake kwa madhumuni ya kuitaifisha au madhumuni mengineyo bila idhini ya sheria ambayo inaweka masharti ya kutoa fidia inayostahili.”

Kifungu hiki cha katiba hakikatazi utaifishaji, bali kinakataza utaifishaji usiokuwa na idhini ya sheria inayoweka masharti ya malipo ya fidia stahili.

Aidha, haki ya kumiliki mali, kama zilivyo haki nyingine zilizowekwa na katiba, zimewekewa mipaka na ibara ya 30 ya katiba hiyo. Hivyo basi, kwa mujibu wa ibara ya 30(2)(a), utaifishaji wa mitambo ya Dowans hautakuwa haramu iwapo utafanywa kwa ajili ya kuhakikisha maslahi ya umma hayaathiriwi na matumizi mabaya ya uhuru na haki ya kumiliki mali ya wamiliki wa Dowans.

Vilevile, halitakuwa kosa kutaifisha mitambo ya Dowans kwa ajili ya kuhakikisha ulinzi, usalama wa jamii, afya ya jamii, mipango ya maendeleo ya miji na vijiji, ukuzaji na uendelezaji wa mali au maslahi mengineyo yoyote kwa nia ya kukuza manufaa ya umma; au kuwezesha jambo jingine lolote kufanyika ambalo linastawisha au kuhifadhi maslahi ya taifa kwa ujumla.

Hii ni kwa mujibu wa ibara ya 30(2)(b) na (f) ya katiba.

Sio tu kwamba katiba inaruhusu utaifishaji wa mitambo ya Dowans, zipo pia sheria zinazoweka utaratibu wa malipo ya fidia kama inavyotakiwa na katiba.

Kwa vile Dowans ni kampuni ya nje, kwa maana ya kusajiliwa Costa Rica na kwa maana ya sehemu kubwa ya hisa zake kumilikiwa na Brigadia Suleiman Al Adawi ambaye siyo raia wa Tanzania, basi sheria inayoweka masharti ya ulipaji fidia kwa utaifishaji wa mali kama mitambo ya Dowans, ni Sheria ya Vitega Uchumi ya Tanzania ya mwaka 1997. Kwa kiasi kikubwa sheria hii, inawahusu wawekezaji wa kigeni.

Hata hivyo kuna shaka kubwa kama Dowans inaweza kunufaika na ulinzi wa sheria hiyo kwa vile iliingia nchini na imekuwa ikifanya biashara zake bila kufuata utaratibu uliowekwa na sheria hiyo, ikiwamo kusajiliwa kama mwekezaji katika kituo cha uwekezaji cha taifa (TIC).

Kwa maana hiyo, endapo mitambo ya Dowans itataifishwa itapaswa kulipiwa fidia kwa mujibu wa sheria ya vitega uchumi iwapo tu itakuwa iliingia nchini na; au inafanya biashara, kwa mujibu wa sheria hiyo.

Kuhusu hoja ya pili ya kutaifisha bila kulipa fidia, hii inaegemea katika maswali yafuatayo: Kwanza, Dowans iliingiaje nchini kwa njia halali? Pili, Richmond iliyokuwa mmiliki wa kwanza wa mkataba wa kufua umeme nayo iliingia nchini na kuendesha shughuli zake kihalali?

Swali la pili lilishajibiwa na Kamati Teule ya Bunge, kwamba Richmond iliingia nchini na kupata mkataba wa kufua umeme kwa njia za rushwa na hivyo kwa vyovyote vile, wamekiuka sheria za nchi hasa sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA) ya mwaka 2004.

Zaidi ya hayo, ushahidi uliotolewa mahakamani umethibitisha uharamia mwingine wakati wa kuingia mkataba. Kwamba aliyekuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa TANESCO, Johannes Lottering alitishwa na mkurugenzi wa nishati katika wizara ya nishati na madini, Bashir Mrindoko ili aridhie mkataba na Richmond.

Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) inasema katika hukumu yake, “…Ijumaa ya 23 Juni 2006, Bw. Lottering alipokea simu kutoka kwa kamishna wa nishati na masuala ya mafuta katika wizara ya nishati na madini ikimtaka aende kwenye ofisi za wizara hiyo mara moja.

“Lottering hakuwa ameelezwa mapema kuwa angehitajika wizarani na kamishna wa nishati hakumpa sababu yoyote ya kumhitaji. Bw. Lottering aliitikia wito huo kama alivyoagizwa na alipofika alimkuta mwakilishi wa Richmond.” Hapo ndipo mkataba uliposainiwa.

Jibu la swali la pili nalo ni hasi. Dowans hawakuingia nchini na kuendesha shughuli zao kihalali. Kuna ushahidi wa kutosha unaothibitisha kwamba kama ilivyokuwa kwa Richmond, Dowans nayo ilitegemea kubebwa na viongozi wakuu kabisa serikalini ili kuweza kurithi mkataba haramu wa Richmond.

Bila shinikizo na; au vitisho vya waziri Ibrahim Msabaha, waziri mkuu wakati huo Edward Lowassa na kamishna wa nishati Mrindoko, ni wazi Dowans isingeruhusiwa kurithi mkataba feki wa Richmond. Kubebwa huko kwa Dowans kulikuwa ni kinyume na sheria za nchi.

Hata hivyo, kuna ushahidi wa kutosha unaoonyesha kuwa Rostam Aziz, mbunge wa Igunga, kwa kusaidiana na Edward Lowassa na waziri wa nishati na madini wa wakati huo, Dk. Ibrahim Msabaha, walishinikiza shirika la umeme la taifa (TANESCO) kuipa kazi ya kufua umeme wa dharula kampuni feki ya Richmond.

Pamoja na Rostam Aziz na washirika wake kufahamu Richmond haikuwa na uwezo wa kufanya kazi iliyoomba; na wataalam wa TANESCO walikuwa tayari wameinyima kazi kwa sababu ya kutokuwa na sifa, bado viongozi hao walishinikiza TANESCO kuingia mkataba na kampuni hiyo.

Hata kama Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba wa Richmond haikumtaja kwa jina Rostam Aziz, bado kitendo chake cha kushinikiza mkataba kwa kampuni iliyokataliwa kwa sababu za kitaalam “kilikuwa ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na matumizi mabaya ya madaraka.”

Haya yamejidhihirisha katika ushahidi uliotolewa ICC unaomhusisha Rostam na  Dowans kwa upande mmoja na TANESCO na Richmond kwa upande mwingine.

Aliyekuwa ofisa mtendaji mkuu wa wa TANESCO, kati ya mwaka 2006 na 2007, Andrew Tice aliiambia ICC kuwa “katika kipindi cha Oktoba, Novemba na Desemba 2006, Henry Surtees – mfanyakazi wa Rostam Aziz katika kampuni yake ya Caspian – alifanya kazi kubwa ya kuhakikisha Dowans inachukua mkataba wa Richmond na inanunua mitambo yote muhimu kwa ajili ya mradi huo.”

Henry Surtees ndiye ICC iliyesema alitumwa nchini Marekani, 7 Oktoba 2006 na Rostam kusaini mkataba kati ya Richmond na Dowans, huku TANESCO wakiwa hawana lolote wanalolijua.

Waliokuwa wanalifahamu hilo ni kinara mkuu wa “dili” hiyo, waziri wa nishati na madini, Nazir Karamagi na Lowassa.

Hivyo kusema Rostam Aziz, Karamagi na Lowassa walikuwa wamekula njama za pamoja za kuhamisha mkataba wa Richmond kwenda Dowans, hakuwezi kuwa ni kusema uongo. Vivyo hivyo ikisemwa kuwa  wanahusika pia walishiriki katika njama za kuificha taarifa TANESCO juu ya uhamishaji wa mkataba wake.

Hii ni kwa sababu, ushahidi uliotolewa ICC unaonyesha TANESCO ilijulishwa uhamishaji wa mkataba 4 Desemba 2006 – karibu miezi miwili baada ya Mohammed Gire wa Richmond na Henry Surtees wa Caspian Ltd./Dowans kusaini uhamisho wa mkataba.

Mwandishi wa makala hii ni wakili wa mahakama kuu na mbunge wa Sigida Mashariki (CHADEMA). Anapatikana kwa simu: 0786 572571
0
Your rating: None Average: 4 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: