'Mitume kumi na mbili' imevuna au imepoteza?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 24 February 2010

Printer-friendly version
Gumzo
SAKATA LA RICHMOND

HOJA za msingi hazijajadiliwa. Watuhumiwa wa ufisadi wameendelea kupeta. Vidonda vya migawanyiko vilivyokuwa vipate tiba, vimeshindikana kupona.

Kazi iliyopewa kamati ya rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi; ya kutafuta ukweli juu ya madai ya kuwapo mpasuko na hatua za kuchukua kukabiliana na migawanyiko, haikwenda kama ilivyotakiwa.

Badala yake, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyokutana kwa siku mbili mjini Dodoma wiki iliyopita, “iliweka wanachama wote wa CCM katika kapu moja la mafisadi.”

Ni baada ya kuipa kazi Kamati ya Mwinyi kupatanisha wanaoitwa “vigogo wa mpasuko bungeni,” Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Septemba mwaka jana, NEC iliipa Kamati ya Mwinyi kazi ya kutafuta chanzo cha mpasuko kati ya Bunge na serikali na kati ya serikali na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Ndani ya Baraza, Wawakilishi wa CCM wakiwamo mawaziri, walidaiwa kutoa matamshi yaliolenga kudhalilisha waziri mkuu, Mizengo Pinda na “kuhatarisha” Muungano.

Wiki mbili kabla ya mkutano wa Dodoma, wajumbe walewale waliotuhumiwa, “waliasi” serikali ya Muungano na chama chao. Waliungana na Chama cha Wananchi (CUF) kupitisha “Azimio la kuundwa kwa serikali shirikishi Zanzibar” ndani ya baraza.

Hata hivyo, NEC haikujadili suala la kudhalilisha waziri mkuu, wala madai ya kuhatarisha Muungano. Bali wajumbe walishusha tuhuma, shutuma na lawama zao kwa Rais Amani Abeid Karume kwa kusema kuwa ameruhusu “ndoa batili” kati ya CCM Zanzibar na CUF.

Walidai kwamba Rais Karume anataka kung’ang’ania madaraka na wengine wakafika mbali zaidi kwa kusema “Karume anataka kuikabidhi serikali kwa CUF.”

Nayo taarifa ya Kamati ya Mwinyi, imethibitishia NEC kwamba ndani ya Bunge kuna makundi mawili. Kundi la kwanza ni la watuhumiwa wa ufisadi ambalo linaongozwa na Rostam na jingine linalojiita la wapinga ufisadi, linaloongozwa na Spika Sitta.

Kamati imesema chanzo cha makundi hayo, ni mjadala wa mkataba wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya kitapeli ya Richmond Development Company (LLC).

Kule Kamati ya Mwinyi kuthibitisha kwamba kuna makundi mawili yanayonyukana bungeni, kumeumbua watetezi wakuu wa watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama hicho.

Si mara moja wala mbili, mbunge wa Ukonga, Makongoro Mahanga na wenzake wamekuwa wakikana kuwapo kwa makundi mawili bungeni.

Walisisitiza kuwa kuna kundi moja; linaongozwa na Spika Sitta. Likapachikwa hata jina “Mitume kumi na wawili.”

Hata hivyo, Kamati ya Mwinyi, ama kwa bahati mbaya, au kwa makusudi, imeruhusu umma kutilia shaka ripoti yake.

Mashaka hayo yanatokana na hatua ya Kamati kutaja Rostam na Sitta kuwa “vinara wa makundi” na kumtenga aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa.

Hakuwezi kuwa na mnyukano bungeni unaotokana na “sakata la Richmond,” kisha Lowassa akabaki nje. Labda kama Kamati ya Mwinyi ina ajenda ya siri ya kudhoofisha Lowassa kisiasa.

Kamati ya Mwinyi ingemtaja Rostam kama ni mfuasi wa Lowassa, labda ingeeleweka.

Vinginevyo, taarifa ya Kamati inataka kupendekeza kuwa “Richmond ni mali ya Rostam.” Kamati ingesema kwamba hatua ya Sitta na kundi lake kushupalia mkataba, kumesababisha Rostam kudhoofika kiuchumi.

Ameshindwa kulipa mishahara kwa wakati, wafanyakazi wa kampuni yake – New Habari (2006) Limited. Huko ndiko kulisababisha ajenge makundi ndani na nje ya bunge; ayafadhili na wakati mwingine ayaelekeze la kufanya.

Vinginevyo mpaka sasa Rostam hana alichopoteza. Bado ni mjumbe wa Kamati Kuu (CC), NEC na anaendelea kupeta bungeni.

Si mara moja wala mbili, Rostam amekana kuifahamu Richmond. Hata pale Bunge na vyombo vya habari vilipombana kufafanua uhusiano wa kampuni yake ya Caspian na Richmond, bado aliendelea kuapa kwa kusema, “Wallahi, Richmond si kampuni yangu.”

Hivyo basi, kama Kamati ya Mwinyi haijasema uhusiano wa Rostam na kampuni ya Richmond, haina haki ya kumhusisha na makundi hayo.

Kama Rostam si sehemu katika hili, katu hawezi kujenga makundi yanayoweza kuhatarisha uhai wa chama chake; kudhoofisha serikali na kukausha mkakati wa Rais Jakaya Kikwete wa kuendelea na urais kwa kipindi kingine.

Ni Lowassa ambaye amejeruhiwa na Richmond. Amepoteza wadhifa wake wa waziri mkuu, hadhi yake mbele ya jamii na kibaya zaidi, anatakiwa kufanya jitihada binafsi za kujisafisha kwa kuwa wenzake katika chama wamegoma kumsafisha.

Akishindwa kujisimamia na kujisafisha, atakuwa ametokomea kisiasa. Atakuwa amepoteza sifa ya kuwa kiongozi katika siku zijazo.

Kilichobaki mikononi mwake, ni marupurupu ya uwaziri mkuu. Basi. Hata haya, wapinzani wake wanasema anayapata kwa hisani ya watawala, si kwamba anastahili.

Kiini cha Lowassa kufikishwa hapa si kingine, bali ni kile wapambe wake wanachodai “njama za Sitta na kundi lake kummaliza kisiasa.”

Mbali na hilo, kuna jingine kubwa zaidi ambalo Kamati imepewa jukumu la kulifanya. Kupatanisha Sitta na Rostam ili kumaliza mpasuko.

Hata hivyo, Kamati na NEC havijasema kwamba baada ya kupatanisha Sitta na Rostam, itapatanisha wananchi wa Simanjiro, mkoani Arusha, waliokesha wakitetea mbunge wao, Christopher ole Sendeka, waliyedai kubambikiwa kesi na mfuasi wa Lowassa, ili kumdhalilisha kisiasa.

Kamati haijaeleza wananchi hawa waliotembea kwa miguu kutoka Simanjiro hadi Arusha mjini, kuunga mkono mbunge wao na kushuhudia Sendeka alivyodhalilishwa na kunyanyaswa.

Si hivyo tu, NEC haijaeleza iwapo Sendeka atakuwa amemalizana na Lowassa kwa Sitta na Rostam kusema “yamekwisha.”

Ni Sendeka ambaye taarifa zinasema alikuwa wilayani Kiteto katika kampeni za CCM aliyeombwa na katibu mkuu wa chama hicho, Yusuph Makamba kuongozana naye kurejea Dodoma kumuokoa Lowassa kwa kile Makamba alichoita, “Sitta anataka kumfukuza ndugu” yake.

Lakini mara baada ya kufika Dodoma, Sendeka alinukuliwa akimwambia Makamba, “Nakushukuru kwa kunifikisha Dodoma, lakini hapa Lowassa hawezi kutoka.”

Haya yalitokea siku mbili kabla Kamati Teule ya Bunge kuwasilisha ripoti yake bungeni.

Kingine ambacho NEC, kama Kamati ya Mwinyi havijasema, ni wananchi wa Tabora wanaokwaruzana kutokana na makundi ya Sitta na Profesa Juma Kapuya. Sitta na Kapuya wamejenga makundi yaliyobeba hata ambao hawakuwamo.

Ismail Aden Rage ambaye tayari ameungana na Sitta kupambana na Kapuya, NEC haijasema kama aweza kusamehe kwa hatua ya kuwapatanisha Sitta na Rostam.

Hali ni viyohiyo kwa wananchi wa Kyela, waliopigwa virungu na mabomu ya machozi na polisi kwa kutetea mbunge wao, Harrison Mwakyembe.

Ni baada ya Mwakyembe aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati Teule iliyochunguza Richmond, alipowasili jimboni mwake.

Hata mvutano kati ya Mwakyembe na mkuu wa mkoa wa Mbeya, John Mwakipisile, NEC haijasema kama utakwisha kwa kupatanisha Sitta na Rostam.

Haifahamiki pia iwapo “ndoa ya Sitta na Rostam” inaweza kumaliza mvutano kati ya mbunge wa Nzega Lucas Selelii na mwanasiasa kijana, Hussen Bashe anayetajwa kuwa kutoka kundi la Rostam Aziz.

Wala hakuna uhakika kama Nape Nnauye aliyesafiri hadi Nzega akiwa na kundi la “wapambanaji wa ufisadi,” kumtuhumu Bashe kuwa ana uraia wa karatasi, kama wanaweza kusameheana.

Hata kama Nape siye aliyehubiri kuwa Bashe ni Msomali, lakini kule kuwa kwake katika kundi lililomdhalilisha tayari kumejenga ufa miongoni mwao ambao hauwezi kuzimwa kwa Sitta na Rostam kushikana mikono.

Hata Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Salum Londa, hawezi kumsamehe mbunge wa Same Mashairiki, Anne Kilango Malecela kwa hatua yake ya kukubaliana na mbunge wa CHADEMA, Halima Mdee.

Londa aliwasilisha kesi bungeni akituhumu Mdee kumkashifu na kumdhalilisha. Lakini apoona mambo yanakwenda kombo, aliamua kuondoa kesi yake.

Hata hivyo, Sitta ambaye alikuwa na uwezo wa kuamuru Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, inayoongozwa na Kilango, kusitisha usikilizaji wa shauri hilo, aliruhusu kazi hiyo kuendelea pamoja na kwamba walalamikaji wote wawili – Londa na Makamba – walikuwa wameondoa malalamiko yao.

Kilango na Sitta walinukuliwa wakisema, “kesi ya Makamba na Londa lazima ihitimishwe;” uhitimishaji ulioishia kumpa ushindi Mdee.

Kamati ya Mwinyi haijasema kama mkutano wa Sitta na Rostam utawahusisha pia mbunge wa Kishapu (CCM), Fred Mpendazoe na mwenzake wa Vunjo Aloyce Kimaro.

Kwa zaidi ya miaka minne sasa, Kimaro na Mpendazoe, wamekuwa wakitaka rais mstaafu Benjamin Mkapa achukuliwe hatua za kisheria kwa kuhujumu taifa.

Mkapa anatuhumiwa kujimilikisha mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya kinyume cha taratibu.

Kama yote haya yawezekana, je, nani anapatanisha Sitta na Nazir Karamagi, mbunge wa Bukoba Vijijini aliyetuhumiwa bungeni kwa ufisadi kupitia mkataba wa kampuni ya TICTS na mgodi wa madini wa Buzwagi? Bila shaka hakuna.

Kinachotakiwa si kutafuta “utakaso” bali kurejesha upya mjadala wa Richmond bungeni. Kwa kufanya hivyo, ndipo mzizi wa fitina utakapomalizika.

Na kwa kuwa Spika Sitta amefunga mjadala, basi suala hilo litarudi bungeni katika Bunge la 11 katika mkutano wake wa tatu, Aprili mwaka 2011.

Kanuni ya Bunge inaruhusu mjadala kurejeshwa bungeni baada ya miezi 12. Hivyo, ni lazima Richmond itarejea, ama kupitia wabunge wa vyama vya mageuzi, ambao hawakuridhishwa na namna Sitta avyofunga mjadala, au kutoka katika kundi la wafuasi wa Lowassa.

Wakati huo, Sitta hatakuwa tena Spika wa Bunge la Jamhuri. Kwa jinsi CCM ilivyoamua kukumbatia watuhumiwa wa ufisadi, Spika atakuwa Lowassa au Andrew Chenge.

Na kwa kuwa NEC imekataa kumsafisha Lowassa, huo ndiyo utakuwa mpenyo pekee kwa Lowassa kujisafisha na hatimaye kujipanga kwa urais wa mwaka 2015.

Kwanza, Spika mpya ataunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kama Kamati ya Mwakyembe iliyotumia zaidi ya Sh. 450 milioni ilitenda kazi kwa maslahi ya taifa au ilikuwa na ajenda binafsi na Lowassa.

Pili, Kamati Teule itachunguza ushupavu wa Lowassa wa kuipa kazi Richmond ulitoka wapi? Alikuwa peke yake au kulikuwa na baraka za rais Kikwete? Na kama Kikwete alishiriki, kwa nini alikubali kumtosa?

Tatu, ni kweli kwamba anayedaiwa kuwa mmiliki wa Richmond/Dowans, Brigedia Jenerali Alwi wa Faalme za Kiarabu, ni swahiba mkuu wa Rais Kikwete na Rostam?

Kupatikana kwa majibu ya maswali haya, ndiko “kutasafisha” Lowassa na hapo, itakuwa muda mwafaka kufunga mjadala na mwisho wa mnyukano bungeni na ndani ya cha hicho.

Ni utata mtupu. Ni mazonge. Tunasubiri kuona mengi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: