Mivutano ya wanasiasa inaitafuna Mbarali


Innocent Ngoko's picture

Na Innocent Ngoko - Imechapwa 27 January 2010

Printer-friendly version

KWA muda mrefu Wilaya ya Mbarali imekuwa na matatizo yanayokwamisha kasi ya maendeleo yake. Siasa za makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizochipuka zamani na kudumu hadi sasa ni miongoni mwa matatizo hayo.

Wanasiasa wa ngazi mbalimbali wa CCM wamekuwa wakivutana na hivyo kusababisha jimbo kukosa viongozi mhimili wa kusaidia lipate maendeleo.

Taarifa zinasema vikumbo na mpasuko mpana uliopo kati ya Mbunge wa Mbarali, Esterina Kilasi na Baraza la Wazee wa CCM na wanachama wake ambao wanashutumiana kuhusiana na hali ya kisiasa ya jimboni na nje yake, vimekuwa vikidhoofisha mshikamano ambao ni nguzo kuu ya kupatikana maendeleo hayo.

Wengi wa viongozi wa CCM jimboni wanatumia muda mwingi kupambana badala ya kushikamana na kushughulikia maendeleo ya watu.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa hapa wanaona vikao vya mara kwa mara vya CCM vinavyojaribu kuzika tofauti za viongozi, havijasaidia kitu. Hata vile vilivyojenga makubaliano, yaliishia maneno matupu.

Sasa mgawanyiko unaozidi kuimarika, umesababisha baadhi ya watu kuendelea kuendekeza njaa kwani wamekuwa wakitumia vizuri mgawanyiko huo kujinufaisha. Muda mwingi utawakuta wanapanga namna ya kuchafuana.

Jimbo linalosifika kwa uzalishaji wa mpunga, linarudi nyuma. Viongozi hawashirikiani. Kila mmoja anaabudu kundi lake na wanasiasa wanaoyaongoza.

Shida za wananchi hazitafutiwi ufumbuzi. Wanajikuta wakiishia kushangilia tu vituko. Matokeo yake hawakupata mtetezi pale serikali ilipobinafsisha mashamba makubwa ya Kapunga na Mbarali na ilipoamuru na kutekeleza operesheni mbaya kuwahi kutokea hapa ya kuondoa wafugaji maeneo ya Bonde la Ihefu na wakazi wa kata za Msangaji.

Mamia ya mifugo walikufa na wengine kuibwa na viongozi waliosimamia operesheni hiyo ambao walitumia vibaya madaraka kunyonya wafugaji.

Tangu mashamba hayo yalipobinafsishwa na kupewa wawekezaji, hakuna lolote la maana lililofanyika hivyo kubaki hayazalishi chochote.

Wakazi wengi wa karibu na mashamba hayo wamelazimika kufuata matakwa ya wawekezaji hao ikiwemo masharti magumu ya kutopatiwa maji ya kutosha na kwa wakati.

Katika risala yake, Mkuu wa Mkoa, John Mwakipesile alimjulisha rais kwamba mmoja wa wawekezaji wa shamba la Kapunga ameamua kulima mibono shambani badala ya mpunga kama alivyoambiwa wa wakati wa ubinafsishaji.

Kauli hiyo ilimshangaza Rais Kikiwete na kulaumu viongozi kwa kushindwa kusimamia vema raslimali za taifa; na akahoji “Mwekezaji anapata wapi jeuri ya kulima mibono kinyume na makubaliano aliyofikia na serikali wakati wa kubinafsisha mashamba?”

Kazi ya kuhamisha wafugaji bonde la Ihefu na wakazi wa Kata ya Msangaji na vijiji vingine vya karibu nalo, ilitawaliwa na ubabe na ufisadi huku viongozi waliopewa dhamana kusimamia haki za raia wakiwemo Polisi, wakitumia dhamana hiyo kutajirika.

Wafugaji walipigwa viboko huku mifugo yao ikiporwa na kufilisiwa kwani wengi walishindwa kuikomboa.

Mamia ya wafugaji waliburuzwa mpaka kufika maeneo ya mikoa ya Lindi na Pwani ambako maisha yamekuwa magumu mno kwao.

Wakazi wa kata ya Msangaji na vijiji vingine vya wilaya ya Mbarali walioathirika na operesheni hiyo walipewa malipo kiduchu ili kwenda maeneo mapya waliyopangiwa likiwemo la Mlungu.

Operesheni iliyokusudiwa kunufaisha mazingira, ikawageukia wafugaji kuwa ndiyo njia ya kuwa mafukara milele.

Kauli ya Rais Kikwete kwamba operesheni hiyo imeleta tija kwa taifa, imechukuliwa kama msumari wa moto na wafugaji walioathirika nayo.

Hiyo ni kauli iliyozima hata matumaini yao ya kulipwa fidia kwa hasara waliyoingizwa na serikali kama ambavyo waliahidiwa.

Na kwa vile wafugaji hao hawana viongozi wawajibikaji ambao wangewasimamia hadi kupata haki zao kutokana mivutano ya kisiasa wanayoipalilia, inabaki kwamba yaliyopita si ndwele tugange yajayo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: