Mjadala wa Katiba kama usanii


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 13 April 2011

Printer-friendly version
Vijana waliofurika ukumbi wa Karimjee kujadili Katiba

ENEO la Karimjee, ukumbi maarufu jijini Dar es Salaam. Nakuta mjadala wa muswada wa sheria ya marejeo/mapitio ya Katiba wa 2011 ndio kwanza umeanza.

Sikupata kuingia ukumbini.Hakuna nafasi ya kuingia sembuse ya kukaa. Si ukumbi mkuu wa chini, wala ukumbia mdogo wa juu. Kote kumejaa wananchi.

Ofisa wa Polisi ananiuliza ninatoka taasisi gani. Nilipomtajia, akabadilika sura. Akawa mchangamfu. Akasema, “Tena wewe ingefaa hasa uwemo ndani. Lakini angalia mwenyewe, unaweza kupita?”

Ukweli hapakuwa na njia maana mlango umefungwa na mbele yake kwa ndani, wamesimama wananchi. wameuzuia hapapitiki.

Nikamuuliza juu vipi? Akanionesha tangazo lililosomeka, “Ukumbi wa juu umejaa.” Pembeni yake, kuna tangazo lililotoa taarifa ya kujaa ukumbi mkuu.

Akanisihi nibaki nje ambako kulifungwa spika kwa ajili ya wananchi kusikiliza mjadala unaoendelea ndani. Nikaridhia, sikuwa na njia.

Ghafla nikabaini jambo.Ndani mjadala unaendelea. Kumbe na nje kulikuwa na mjadala. Mijadala miwili. Bali ni mijadala tofauti. Wa ndani unaongozwa na Pindi Chana, mbunge wa Viti Maalum na mjumbe wa Kamati ya Sheria na Katiba ya Bunge.

Mjadala wa nje hauna mwenyewe. Kila anayemudu kusema, anasema. Anasema atakalo. Na huu wa nje, ulikuwa na usanii wake kama ulivyokuwa ule wa ndani.

Mjadala ndani ulikuwa unavunjikavunjika.Nikachungulia ndani kupitia madirishani baada ya kusikia zogo jingi kutokea ukumbini.

Kulikuwa na vijana, wasichana na wavulana, baadhi yao wakiwa wamevalia nguo zilizojenga taswira fulani ya kisiasa. Hawa walikuwa wakizomea kila mtu aliyepewa kipaza sauti na kujadili muswada.

Lakini alipopewa kipaza sauti mtu waliyeamini kuwa ni “mtu wao,” walimshangilia kwa nguvu kubwa huku wakipigapiga viti. Hawakujali alichokisema. Ni kushangilia tu.

Nikajisogeza mlango mkuu wa kuingilia ukumbini. Saa tano sasa ulishakuwepo mwanya kwa mtu kupita na kujichomeka ndani. Nikapita. Niliketi na kuanza kujionea nilichoanza kukisikia nilipokuwa nje.

Kulia tu ukishaingia ukumbi mkuu, niliona watu wa kawaida walioonesha kama wamefika kwa mkumbo. Hili nilishalithibitisha nilipokuwa nje kwa kuuliza baadhi ya vijana wenzao waliosema walichoka kukaa ndani na kuamua kutoka.

Baadhi yao walikuwa wameshika karatasi. Nikabaini ilikuwa ni muswada unaojadiliwa ambao umeandikwa kwa Kiingereza. Kassim Bakari, John Tupa na Mwanaidi Shabani walinithibitishia hawafahamu lugha hii.

“Ukweli kaka yangu, hapa sipati picha. Nadhani nimekubali upuuzi.Haya si mambo yetu sisi tuliokosa elimu ya sekondari. Natafuta njia nirudi nyumbani,” alisema Mwanaidi, mkazi wa Buguruni.

Mwanaidi alifika Karimjee kwa gari maalum na wenzake asiowajua idadi na kwamba waliletwa na aliyemtaja ni kiongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Buguruni.

Nilipokuwa nje, Shabani Kabwe, mhitimu wa darasa la saba mwaka 2010, aliniambia kwamba alikuja Karimjee bila ya kufahamu alichokuja kukifanya. Alisema amekuja na wenzake kuitikia wito wa Meja, aliyedai ni kiongozi wa CCM Buguruni.

“Tena tunamsubiri hapa hatumuoni. Sisi tumechoka kukaa maana humo ndani hakuna tunachokifanya na tumeanza kusikia njaa. Unajua hatuna hata nauli ya kurudi nyumbani kwani yeye ndiye ametuahidi kutupa Sh. 2,000 tukimaliza kazi,” alisema.

Kijana aliyevaa vizuri na kufunga tai, Peter Chana, aliniambia amefika ili kujadili muswada wa katiba, ingawa alikuwa hajapata nafasi ya kuzungumza ukumbini.

“Mimi nimekuja kutoa maoni yangu. Nimekaa na vijana wenzangu kijiweni na kukubaliana niwasilishe maoni yetu. Nafasi haipatikani lakini sijavunjika moyo,” alisema huku akishutumu utaratibu mbaya uliowekwa wa mjadala na udhaifu wa kamati ya bunge kuvumilia “wahuni” wazomee wanaojadili.

Kamati ilielekeza watakaopata nafasi ya kujadili, waende moja kwa moja kwenye kifungu kilichokuwa kinajadiliwa. Hiyo ilikuwa ni tofauti na mjadala ulivyoendeshwa siku iliyotangulia, Alhamisi.

Siku hiyo ya kwanza ya mjadala, walialikwa viongozi wa vyama vya siasa. Hoja nyingi zikawa za wanasiasa katika mtizamo wa kisiasa. Wachache, hasa wa upinzani, walieleza mantiki ya muswada na vile ulivyoshindwa kukidhi matarajio ya wananchi walio wengi.

Kutofautiana kwa maoni yao, ndiko kulichangia mjadala kuvunjika. Vyama vililaumiana kuamsha hisia kali. CCM ililaumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na chenyewe kikalaumu makada wa CCM waliokusudia kusifia kila kitu katika muswada.

Mtafaruku uliotokea ukumbini, ulimkimbiza Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki kupitia CHADEMA. Akiwa naye ni mjumbe wa Kamati ya Bunge inayoendesha mjadala wa muswada huo, aliitisha waandishi wa habari na kusema, “Mjadala wa leo hauna maana yoyote.”

Lissu ambaye ni mwanasheria, alisema utaratibu ulikuwa mbaya na meza kuu imeshindwa kudhibiti makundi ya vijana wa CCM waliopelekwa kuzomea wananchi waliokwenda kutoa maoni yao kuhusu muswada.

Alisema, “Kinachoendelea humo ndani ni kupoteza muda. Makundi ya vijana wasio na kazi wameletwa na CCM kuja kuzomea watoa maoni wema. Na kwa sababu muswada wenyewe umeandaliwa kivodafasta, hata mjadala wake unapelekwa kivodafasta.

“Mwenendo huu hautatufikisha Watanzania katika kupata katiba tunayoitaka. Tutakuwa tunaendeleza mambo ya watawala. Sasa mimi kama Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, nasema chama chetu hakikubali muswada huu, na tutakwenda mitaani kuwaambia hivyo wananchi ili nao waukatae maana hauna maslahi nao.”

Lissu alipomaliza maelezo yake nje ya ukumbi wa Karimjee, alipanda gari na kuondoka huku akisema, “Siwezi kubaki hapa na kusikiliza mambo ya ovyo.”

Wakati anaendelea kuzungumza na waandishi wa habari, vijana waliojitambulisha kama “vijana wa taifa,” walikuwa wakizungumza kwa sauti kama vile wakikusudia kumvuruga Lissu.

Nilijaribu kuwasihi wakae kando ya mkutano wa Lissu. Ndipo walipojibu kwa hasira, “Yeye ni mwananchi na sisi ni wananchi vilevile tuna haki ya kusema.” Hata niliposisitiza kuwa watasikilizwa baada ya Lissu, walimaka, “Acha aongee hapo na sisi tunaongea hapa. Hakuna tatizo kila mtu ana haki.”

Maelezo hayo yalionyesha kutopendezwa na msimamo wa Lissu. Kuthibitisha, kijana mmoja aliporudi ukumbini, na kupata nafasi tena kujadili muswada, alitaka kamati imdhibiti Lissu kwa kile alichoita, “amesaliti kamati” kwa kutoa msimamo nje ya ukumbi kupitia vyombo vya habari.

Watu kadhaa kutoka hapo walionekana wakitoka nje ya ukumbi.Wachache wakawa wanarandaranda huku wengi wakiamua kukaa kwenye kivuli cha miti ya bustani kupumzika.

Alikuwepo Marry Francis. “Mimi kaka yangu nilikuja hapa kusikiliza tu mjadala wa katiba. Nimekuja na wenzangu wao bado wapo kule ndani, isipokuwa mimi naona nimechoka na ni kama vile nimekuja kupoteza muda. Sielewi.”

Mara aliwasili Tambwe Hiza, naibu mkuu wa propaganda wa CCM. Haraka akasifia utaratibu uliopo. Nilishangaa kwa sababu alikuwa ndio anaingia kwa gari.

Nilipomuuliza inakuaje anasifia hali wakati ndio anawasili Karimjee, alisema, “Mimi najua. Na nimekuja na maoni yangu baada ya kupitia vifungu mbalimbali vya muswada. Unajua CHADEMA jana (Alhamisi) walikuja na vijana wao ili kutuvuruga. Leo tumewahi sijui wanalalamika nini.”

Muda mfupi baadaye, aliwasili kada wa CCM na Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Nape Nnauye. Alikwenda moja kwa moja ukumbini ambako haikuchukua hata dakika tano, alisikika akitoa maoni.

“Ndugu wananchi wenzangu hii si katiba ya chama fulani. Na hivi vyama vingine vimekuja mwaka 1992. Tukiruhusu siasa za vyama kuingia katika jambo haili muhimu la kitaifa, kwamba tukiingiza ushabiki wa vyama, tutaipeleka kubaya nchi yetu.

“Halafu mimi naona jambo lolote lazima tupate mahala pa kuanzia. Huu muswada ni hatua muhimu ya kwanza. Sasa kinachotakiwa tutoe maoni yetu kwa hatua inayofuata,” alisema.

Wengi wa waliopata kujadili, walisema muswada una upungufu katika vifungu mbalimbali. Maeneo yanayomtaja rais na mamlaka aliyonayo, kuzuia kujadili masuala ya muungano na mengineyo, kuipa jukumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia kura ya maoni na kuzuia wanasiasa kushiriki kampeni ya kuhamasisha wananchi kuhusu suala la katiba.

0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: