Mjadala wa Richmond bado haujafungwa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 17 February 2010

Printer-friendly version

MJADALA juu ya mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura kati ya serikali na kampuni ya kitapeli ya Richmond Development Company (LLC), ungali mbichi.

Pamoja na Bunge kutangaza kufungwa kwa mjadala mwishoni mwa mkutano wa 18 uliomalizika wiki iliyopita, kila mwenye nia njema kwa taifa hili anajua kuwa utata ungalipo na mjadala unaendelea.

Mjadala ungali hai kwa kuwa mambo ya msingi katika sakata hili hayajapatiwa ufumbuzi. Kuukatisha ni sawa na kusaliti wananchi na taifa kwa jumla.

Jumatano iliyopita, Spika wa Bunge, Samwel Sitta alitangaza bungeni “kufungwa kwa mjadala wa Richmond,” kwa kile kilichoitwa, “Kuachia mamlaka ya juu ya nchi kuchukua hatua.”

Alisema Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeridhishwa na utekelezaji wa serikali kwa yale maazimio 23 ya Bunge kuhusu Richmond.

Bunge lilisema badala ya kubaki kama maazimio yake, taarifa za utekelezaji ambazo zitafanywa na serikali, sasa zitapelekwa kwenye kamati husika za kisekta.

Mwaka 2006, serikali, kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO), iliingia mkataba wa kufua umeme wa dharura na Richmond ambayo tayari ilithibitika kuwa ni kampuni hewa.

Kugundulika kwa kashfa hiyo ya kutoa zabuni kwa kampuni isiyo na uwezo kifedha, kiufundi na hata kimaadili ndiko kulisababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa na waliokuwa mawaziri wa nishati na madini, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.

Katika hali hii, Spika Sitta na wenzake hawawezi kufunga mjadala huu bila ya kwanza kujibu hoja 19 za msingi kwa nini mjadala usifungwe.

Kwanza, yako wapi mamilioni ya shilingi ya wananchi ambayo bunge limekuwa likisema zimelipwa kwa kampuni feki kama sehemu ya malipo ya “Capacity Charge” na gharama nyingine?

Katika mkataba huo kati ya serikali na Richmond, serikali ilikubali kuilipa kampuni hiyo Sh. 152 milioni kwa siku hata kama haikutumia umeme kutoka kwake.

Si mara moja wala mbili, wajumbe wa Kamati Teule ya Bunge waliochunguza mkataba huo, akiwamo mwenyekiti wake, Dk. Harrison Mwakyembe wamenukuliwa wakisema pamoja na kwamba kampuni hiyo ilishindwa kutekeleza mkataba wake na TANESCO, lakini serikali ililipa Richmond mamilioni ya shilingi.

Pili, mjadala hauwezi kufungwa kama mmiliki halisi wa kampuni iliyotia doa serikali hajajulikana; na nakala halisi ya mkataba haijatoka hadharani.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya serikali, Dk. Msabaha ndiye alikuwa na nakala halisi ya awali kabisa, yenye majina ya wakurugenzi wa kampuni hiyo feki; nakala ambayo hata Kamati ya Bunge iliyochunguza kashfa hiyo haikuiona.

Mjadala hauwezi kufungwa kama uhusiano wa kampuni ya Richmond na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, haujawekwa wazi.

Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, Rostam amekuwa akikana umiliki wa Richmond, pamoja na kutajwa mbele ya Kamati Teule ya Bunge na mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu.

Ni Rostam aliyeruhusu Richmond kutumia sanduku la barua, barua pepe na wafanyakazi wa kampuni yake iitwayo Caspian yenye makazi yake Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam.

Tatu, mjadala hauwezi kufungwa wakati haijajulikana watendaji wa serikali na wanasiasa wote waliohusishwa na Richmond walilipwa nini na kiasi gani hadi kukubali kuvunja taratibu na sheria za nchi kwa kuipa kampuni feki kazi ya maana?

Wenye nia njema wanauliza na wataendelea kuuliza je, watumishi walilishwa nini hadi kukubali kutenda kazi kwa maagizo ya wamiliki wa Richmond badala ya serikali iliyowaajiri.

Nne, mjadala hauwezi kufungwa wakati hata Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), haijamtaja mhusika mkuu wa chama hicho anayedaiwa kuwa alikuwa kiungo cha Richmond.

Tano, mjadala hauwezi kufungwa wakati kila mmoja anajua kuwa Dk. Msabaha alidaiwa kujiapiza kwa kusema, “…sitakubali kutolewa kafara, lazima nife na mtu.” Bado Dk. Msabaha yuko bungeni na hajamtaja mtu aliyetaka kufa naye.

Sita, mjadala hauwezi kufungwa hivihivi tu wakati Lowassa hakuwa mmoja wa watu waliokuwa wametajwa na Kamati Teule, hakushauriwa kujiuzulu, lakini ilikuja kudhihirika kuwa alikuwa ameshiriki kushinikiza kampuni ya Richmond ipewe kazi ya kufua umeme wa dharura.

Saba, mjadala haujafungwa bila ya kwanza kumpa nafasi Dk. Msabaha kuwataja hata wale ambao hawakutajwa na Kamati ya Bunge – ambao walikuwa wazito zaidi, na ambao Lowassa alikuwa akiwalinda wasiguswe.

Madai kuwa Lowassa aliamua kujiuzulu ili kumfunga mdomo Dk. Msabaha asitaje hao waliokuwa wakilindwa, hayajawekwa wazi na hayajathibitishwa.

Nane, mjadala hauwezi kufungwa bila kujua kama ni kweli Rais Jakaya Kikwete alijua “kila kitu” kuhusu mradi huo na kwamba alipoona mambo yamekuwa magumu zaidi alimshauri Lowassa afanye uamuzi ambao usingefumua makubwa zaidi, hata kama ungemgharimu nafasi yake ya waziri mkuu?

Katika kikao chake Butiama, mkoani Mara, Kamati ya Usalama na Maadili iliitaarifu Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) juu ya mchakato uliokuwa umechukuliwa kuwalinda vigogo na kwamba katika orodha ya waliopaswa kujiuzulu, Lowassa hakuwamo.

Kamati ilisisitiza kuwa Lowassa alishinikiza wahusika katika wizara ya nishati na madini, wakati huo chini ya Dk. Msabaha, kuikubali Richmond kwa sababu ya maslahi ya waliokuwamo.

Tisa, mjadala hauwezi kufungwa bila ukweli kujulikana kuwa Dk. Msabaha alijua fika namna mkataba wa awali wa Richmond ulivyoandaliwa, na majina yaliyokuwamo katika orodha ya wamiliki wa iliyoitwa kampuni ya Richmond.

Kumi, mjadala hauwezi kufungwa kama nakala halisi ya mkataba haijatoka hadharani.

Kumi na moja, mjadala hauwezi kufungwa bila ya kwanza kupatiwa majibu ya kina kuhusu malalamiko ya Lowassa kwamba alisakamwa kwa hoja dhaifu na visasi vya uwaziri mkuu.

Kufunga mjadala huu bila ya kujulikana ukweli ni kuthibitisha kuwa wote waliohusika walikuwa na nia mbaya na Lowassa.

Kumi na mbili, huwezi kufunga mjadala wakati watendaji serikalini wamekiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA) ya mwaka 2004 tena kwa makusudi kwa lengo la kubeba Richmond.

Kumi na tatu, mjadala huu hauwezi kufungwa kwa utashi wa kikundi kidogo cha watu walioweka mbele maslahi yao binafsi au yale ya vyama vyao.

Kumi na nne, mjadala hautafungwa hadi baada ya umma kuridhika kwamba “serikali imetekeleza wajibu wake katika kuadabisha wote waliohusika kwenye mkataba huu.”

Kumi na tano, mjadala hautaisha hadi wananchi waridhike kwamba Lowassa alijiuzulu ili kuepusha mawaziri kuanza kutajana.

Ingefikia hatua hiyo, Dk. Msabaha anadaiwa alikuwa tayari kuweka hadharani majina ya wakurugenzi halisi wa Richmond, akiwamo “mtoto mmoja wa kigogo mzito” serikalini.

Si kigogo wala mtoto wa kigogo anayejulikana kwa wananchi. Wanasubiri Dk. Msabaha amtaje au mtu mwingine ataje ndipo mjadala utamkwe umefungwa.

Kumi na sita, mjadala hauwezi kufungwa wakati mpaka sasa haijafahamika kinagaubaga, nini hasa ilikuwa dhamira halisi ya Rais Kikwete hadi kukubali Lowassa kujiuzulu.

Hili ni muhimu kujulikana hasa kwa kuwa ni Kikwete aliyemlinda, hadi mwisho, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hoseah na maofisa wengine wa taasisi hiyo waliotuhumiwa kuandaa taarifa isiyo sahihi juu ya Richmond.

Kumi na saba, mjadala wa Richmond hauwezi kufungwa kwa sababu Bunge, katika hatua ya mwisho, limejikunja katika shuka la aibu, kushindwa kutaja mkosaji na hatua zilizochukuliwa.

Kwa mfano, taarifa ya Kamati iliyosomwa bungeni na mwenyekiti wake, William Shelukindo (Bumbuli – CCM), ilisema, Azimio Na. 9 lililokuwa linataka Hoseah aondoke, halikujadiliwa kwa sababu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU huteuliwa na Rais na pia TAKUKURU inachunguza wabunge.

Sasa swali la kujiuliza: Nini kilianza kati ya bunge kutaka Hoseah aondolewe na hatua yake ya kuchunguza wabunge? Jibu ni kwamba lilianza azimio la bunge.

Je, sasa hoja kwamba wabunge wanachunguzwa na Hoseah ilitoka wapi? TAKUKURU si Hoseah, ni taasisi.

Serikali inaweza kumuondoa Hoseah na bado kazi ya kuchunguza wabunge ikaendelea. Ni kama vile mahakamani, kutuhumu hakimu au jaji, hakufanyi kesi kutosikilizwa au kusitishwa kwa utekelezaji wa hukumu.

Kama bunge lilijua kwamba Hoseah anateuliwa na rais kwa nini liliagiza aondolewe katika nafasi yake? Lilikuwa linamuagiza nani?

Lakini kuna jingine kubwa zaidi. Kama bunge liliweza kuchagiza serikali hadi Lowassa akajiuzulu, limeshindwaje kwa Hoseah?

Kumi na nane, bunge haliwezi kufunga mjadala wa Richmond maana ajenda ya Richmond haikuwa ya bunge. Ilikuwa ni ajenda ya wananchi kupitia vyombo vya habari na wabunge wa vyama vya mageuzi.

Kimsingi Sitta na wenzake wameegemea utetezi dhaifu na Sitta ameshindwa kusimamia kauli yake mwenyewe kwamba atakuwa “Spika wa kasi na viwango.”

Sasa Sitta na wenzake, hasa wale walioitwa “Wapiga vita ufisadi,” wanageuziwa kibao kuwa walijipachika katika hoja hii kwa lengo la kujitafutia umaarufu wa kisiasa. Mtu wa kuwatetea sharti awe na hoja kubwa zaidi.

Kumi na tisa, serikali imewafikisha Gray Mgonja na Basil Mramba mahakamani kwa tuhuma za kutumia madaraka vibaya. Je, kama hili limewezekana, serikali hiyohiyo imeshindwaje kufikisha mahakamani waliotia hasara kupitia Richmond?

Ni muhimu Sitta na wenzake wakaelewa kwamba kufunga mjadala, ni kukubali “kufunga ndoa na mafisadi.”

Wananchi wanaona yote haya. Wananchi wataendelea kujadili. Wananchi wataamua.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: