Mjadala wa Richmond urejeshwe tena bungeni


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 30 November 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

RIPOTI ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba tata kati ya serikali na kampuni ya kufua umeme wa dharula ya Richmond Development Company (RDC), hatimaye “imekamilika.”

Kukamilika kwa ripoti hiyo kumefuatia hatua ya Edward Lowassa – mmoja wa watuhumiwa wakuu wa ufisadi kwenye kashfa hiyo, kutaja watuhumiwa wengine wawili muhimu, Rais Jakaya Kikwete na Rostam Aziz.

Akihutubia mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama chake, Alhamisi iliyopita, mjini Dodoma, Lowassa alinukuliwa akisema, “Nisihukumiwe peke yangu.”

Alisema, “Hakuna jambo nililolifanya ambalo Rais Kikwete hukulifahamu au hukunituma.”

Alikuwa akichangia ajenda ya “kujivua gamba” iliyosomwa katika kikao hicho na Pius Msekwa, makamu mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara.

Lowassa alijiuzulu uwaziri mkuu Februari 2008 baada ya Bunge kumtuhumu kufanya upendeleo wa kuipa kazi ya kuzalisha megawati 100 za umeme wa dharura, kampuni “kutoka Marekani” ambayo ilikuja kuthibitika kuwa haikuwa na sifa wala uwezo wa kifedha na kitaaluma.

Katika kikao hicho, Lowassa alieleza hatua kwa hatua ushiriki wa Kikwete katika mkataba huo wa kinyonyaji na usiokuwa na maslahi kwa taifa.

Alisema, “Kila hatua niliyofanya nilikujulisha. Kila jambo nililolifanya nilikueleza. Kuna wakati nilitaka kuvunja mkataba huu, lakini ulinizuia na kunielekeza nilipeleke suala hilo kwa kamati ya makatibu wakuu ili kupata ushauri.”

Akiongea kwa njia ya kumsuta Kikwete, Lowassa alisema, “Hata pale uliponiomba nitafute mtu wa kutusaidia, nilipotaja jina la Rostam (Rostam Aziz), haraka ulisema ni sawa.”

Je, hatua ya Lowassa kumtaja mshirika wake huyo katika jambo hili ina maana gani? Je, imemsaidia kujikwamua kutoka katika kitanzi cha kufukuzwa ndani ya chama na kuitwa fisadi anayekichafua chama mbele ya umma? Majibu ni mengi.

Kwa yale ambayo Lowassa amesema na kunukuliwa na hajayakana, basi ameshiriki kukamilisha ripoti ya Kamati Teule iliyochunguza Richmond.

Tangu awali mwanasiasa huyo amekuwa akiilalamikia ripoti hiyo, akisema haikuwa kamili kwa vile hakuhojiwa wakati yeye alikuwa mlango wa pili tu, kutoka ikulu ya Rais Kikwete na pia hakuwa mbali na mahali ambapo kamati teule ilikuwa inakutana.

Hakuna ajuaye vema, isipokuwa Lowassa, kwamba kama angehojiwa na kamati angeyasema haya – katika joto la wakati huo, au angeghubikwa na usiri wa miaka yote kwa mtu aliyemwita rafiki ambaye “hawakukutana barabarani.”

Miezi kadhaa baada ya ripoti ya kamati teule ya bunge kutolewa hadharani na Lowassa kujiuzulu; aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe alinukuliwa akiwajibu baadhi ya watuhumiwa kuwa, “Kuna mambo mengi ambayo kamati iliyaona, lakini ilishindwa kuyatoa hadharani ili kulinda nchi isitikisike.”

Dk. Mwakyembe alifika mbali zaidi kwa kusema, “Kama Lowassa hajaridhika na kilichotendeka, ni vema akarejesha mjadala huo bungeni.” Alisema yuko tayari kueleza kile ambacho alikiita “makubwa zaidi.”

Je, yawezekana hicho ambacho Dk. Mwakyembe na kamati yake walisita au walikiogopa, ndicho ambacho Lowassa amekieleza kwa wajumbe wa NEC, tena wakiwa mbele ya Kikwete mwenyewe?

Kwa maelezo haya ya Lowassa, sasa ni wazi kuwa Dk. Mwakyembe na kamati yake, wangeeleza kila walichokiona kwenye uchunguzi wa Richmond, Lowassa asingepata nafasi ya kumuumbua Kikwete kama alivyoanza kufanya.

Aidha, labda Lowassa asingeweza kujiuzulu wadhifa wake; asingeondoka peke yake ndani ya serikali na labda ikulu ingetekeleza kwa ufasaha maazimio yote 23 ya Bunge kuhusu suala hilo.

Lakini hatua ya Mwakyembe na wenzake kunyamazia baadhi ya taarifa hizo, ndiko kulikosababisha Richmond/Dowans kwenda mahakamani; Lowassa kuibukia NEC kumuumbua Kikwete; serikali kushindwa kutekeleza maazimio ya Bunge; na Rostam kuendelea kukana kuhusika na makampuni hayo, wakati nyaraka kadhaa, pamoja na taarifa nyingine za siri zinaonyesha yeye ndiye “mmiliki halisi” wa Dowans.

Hata hivyo, matamshi ya Lowassa ndani ya NEC hayajaweza kumuondoa katika tuhuma za kushiriki katika kuingiza nchi kwenye mkataba huu wa kinyonyaji. Kilichosaidia kwenye kauli yake, ni kujulikana kwa watuhumiwa wengine muhimu ambao hapo awali walikuwa wanahisiwa tu bila kufahamika wazi.

Jambo jingine muhimu katika utetezi wa Lowassa ni ukweli kuwa hakusema kuwa hahusiki kuiingiza nchi kwenye utapeli wa Richmond. Bado kwa kauli yake anakiri kuwa aliwajibika kwa yaliyotendeka, aliyosimamia kutendwa na yale aliyoagiza kutekelezwa.

“Hakuna nilichokitenda ambacho hakikufahamika kwa Kikwete,” huo ndio msingi wa kauli yake.

Matamshi haya ya Lowassa yanakuja baada ya mvutano wa muda mrefu uliotokana na hatua ya Rais Kikwete, akiwa Mwenyekiti wa CCM kuasisi dhana ya kujivua gamba ndani ya chama hicho.

Vikao vya chama hicho vilibariki “shingo upande,” utekelezaji wa dhana hiyo, lakini baadhi ya watendaji wapya wa chama hicho wakaishupalia kwa kuwalenga watuhumiwa wa ufisadi akiwamo Lowassa.

Dhana ya kujivua gamba ilizua mjadala mkali ndani ya chama huku kila kukicha wananchi wakikosa majibu kutoka kwa muasisi wa dhana hiyo. Matokeo ya kukosa majibu ni kila mtu kujaribu kueleza maana ya gamba kadri alivyoelewa.

Kuibuka kwa Lowassa katika hatua hii ya “gamba,” kumebadilisha upepo ndani ya chama hicho na sasa inaoenakana dhana hiyo haitekelezeki kirahisi kama ilivyofikiriwa.

Gamba lililoanza likidhaniwa ni la nyoka, sasa limegeuka kuwa gamba la kitunguu ambalo kila unapotoa moja, hujikuta unalazimika kuondoa linalofuata na hatimaye kumaliza kitunguu kizima.

Wachunguzi wa mambo ya siasa wanasema Rais Kikwete aliingia Dodoma kuongoza vikao vya chama akiwa jasiri na mwenye kujiamini, lakini aliishia kufunga vikao hivyo akiwa majeruhi wa tuhuma za Lowassa.

Habari zilizovuja mapema kabla Lowassa kuzungumza zilisema, Kikwete alikuwa anasitasita kuruhusu mjadala wa gamba kwa hofu kwamba “Lowassa amejiandaa kumhusisha na Richmond yake.”

Hilo pia lilidhihirishwa na matamshi ya Kikwete wakati wa ufunguzi wa kikao cha NEC aliposema kwa mafumbo, “Msiwe na wasiwasi, halitaharibika neno lolote hapa.”

Kukwama kwa mkakati wa kujivua gamba ulioongozwa na Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye kunatokana na kauli ya Lowassa, kwamba “msinihukumu peke yangu.” Sasa kama Kikwete naye ni mtuhumiwa, nani anaweza kumuondoa mwenzake?

Mara baada ya kukabidhiwa wadhifa wa ukatibu mwenezi wa CCM, Nape amekuwa akisisitiza, “…Kilichokuwa kinasubiriwa ni suala la utekelezaji tu; NEC imetoa siku 90 kwa mafisadi kuondoka, vinginevyo tutawafukuza.”

Hatua ya Kikwete kunyamaza wakati Lowassa anamtuhumu kuwa mshiriki wa Richmond, imethibitisha madai ya muda mrefu yaliyokuwa yakiporomoshwa na viongozi wa upinzani, hususan CHADEMA, kwamba kiongozi huyo wa nchi ana mkono wake katika suala hilo.

Lakini kuna jingine. Hadi Bunge linamlazimisha Lowassa kujiuzulu, Rais Kikwete hakusikika kukaripia Lowassa, wala katibu mkuu wa nishati na madini, Arthur Mwakapugi kwa hatua yao ya kuficha ukweli na kupindisha maamuzi ya serikali.

Kikao cha baraza la mawaziri cha 10 Februari 2006, kinasisitiza hilo pia. Mkutano kati ya aliyekuwa waziri wa nishati na madini, Dk. Msabaha na watendaji wa wizara yake, 21 Februari 2006 unaeleza bayana “mpango wa serikali, si kukodisha mitambo, ni kuinunua.”

Kama Rais Kikwete angefanyia kazi taarifa kuwa kampuni ambayo Lowassa alikuwa anahaha kutaka kuipa kazi imeshindwa hata kupeleka wataalamu wake nje ya nchi kuangalia mashine za umeme, angeweza kuzuia mkataba huu kufungwa.

Wala Rais Kikwete hawezi kusema kuwa serikali yake haikuwa inafahamu juu ya jambo hili; bali kwa kuwa  aliruhusu marafiki zake – Lowassa na Rostam – alishindwa kuzuia Richmond kupewa kazi.

Kikwete alifahamu kuwa Richmond ilikuwa na mapungufu 13  ikilinganishwa na wazabuni wengine, lakini wateule wake waliingiza serikali katika mkataba tata na kampuni isiyo na sifa.

Lowassa hasafishiki kwa kauli zake. Ni yeye aliyeagiza TANESCO kutangaza upya zabuni ya kutafuta kampuni ya kuzalisha umeme wa dharula.

Alitenda yote haya bila kufuata sheria za manunuzi ya umma na ndiyo chanzo cha serikali kushindwa katika shauri lake na makampuni ya Dowans Tanzania Ltd., Dowans Holding SA na Richmond Company Ltd.

Lakini ndani ya NEC, Kikwete hakutoa kauli ya kumjibu Lowassa. Hakusema mathalani, “sihusiki na hili unalolieleza hapa.” Hatua yake ya kukaa kimya, yaweza kuwa inathibitisha kilichosemwa na Lowassa.

Wala hatujasikia wasaidizi wa rais – idara ya mahusiano ya ikulu au idara ya habari maelezo – ambao wamekuwa mstari wa mbele kutetea rais, wakiinua sauti kuhusiana na madai dhidi ya rais.

Katika mazingira haya, wananchi wanasubiri kauli ya rais. Wanasubiri pia kauli ya bunge – iwapo kuna yeyote atakayepeleka suala hilo bungeni.

Kwani katika hali ya sasa – ya ukimya wa kishindo ndani ya ikulu – ya Lowassa ni yaleyale ya Kikwete. Na huenda ni magumu zaidi ya yaliyofichuka, kwani Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi hawajasema wajuacho.

Mawaziri hao wawili wa zamani wa wizara ya nishati, walitumika kutoa kauli zilizofanana na zile za maofisa uhusiano wa Richmond na Dowans – utetezi. Bila shaka wana lao la kupasua.

Bali swali hapa ni “nani atamfunga paka kengele.” Je, bunge lina ujasiri wa kurejea suala la Richmond na hata kumhoji rais juu ya tuhuma ambazo hajajibu – kwa kukubali au kukataa? Je, huu waweza kuwa mwanzo wa fikra za kutokuwa na imani na rais ndani ya bunge?

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: