Mkakati wasukwa kumwangusha Spika Sitta


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 28 October 2009

Printer-friendly version
Spika wa Bunge, Samwel Sitta

BAADA ya kukwama kwa jaribio la kwanza la kumng'oa Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta mjini Dodoma kupitia chama chake, sasa la pili linadaiwa kuandaliwa kwa ustadi.

Ni piga nikupige kati ya kambi mbili za Chama Cha Mapinduzi (CCM). Upande mmoja unasimama na spika wakati mwingine unadaiwa kusimama na aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa.

Mkakati wa kumg’oa Sitta ambao nusura utekelezwe kwa mafanikio makubwa kule Dodoma katika vikao vya CCM vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), unahusishwa na kambi ya wanaomshabikia Lowassa.

Ni Dodoma ambapo ulisikika wito wa kumvua uanachama Sitta. Ulitolewa na baadhi ya wajumbe kitu ambacho kingemvua ubunge wake na kumtoa kwenye kiti cha spika.

Jaribio lile lilikuwa ni onyo na tahadhari kwa kile ambacho kinatarajiwa kutokea tena katika mojawapo ya vikao vya Bunge – hasa hiki kilichoanza jana.

Baada ya kushindwa kumng’oa Sitta kwa kutumia taratibu za chama, ambazo hata Pius Msekwa, aliyekuwa spika kabla ya Sitta amekiri hazikufuatwa sawasawa, sasa kuna mkakati wa kutumia kanuni za bunge kumng’oa Sitta.

Mkakati huo unalenga kutumia kanuni za bunge kuweza kumuondoa Sitta katika nafasi yake. Taratibu hizo zikifuatwa, Sitta anaweza kupoteza nafasi yake ya spika pasipo kupoteza ubunge wake.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania (ibara ya 84 na 85) Bunge laweza kumuondoa spika katika kiti chake na Kanuni za Utendaji za Bunge zimeweka utaratibu wa kufuata katika kufanya hivyo na ni utaratibu ambao kimsingi siyo mgumu sana.

Ili kumwondoa spika hoja inaweza kuletwa na mbunge yoyote ikiwa na tuhuma mahsusi, maelezo kamili, sahihi yenye kueleweka na isiyokuwa na visingizio, kebehi au matusi au lengo la kumchafulia mtu jina.

Hoja hiyo ikiungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge, basi spika aweza kuondolewa madarakani ingawa anaweza yeye mwenyewe kuamua kujiuzulu.

Mkakati huu ambao unadaiwa kusukwa “vizuri,” unategemea kuona jinsi gani Sitta ataendesha vikao vya mkutano huu wa bunge; kama bado anawapendelea watu fulani au kuonekana kuendeleza “vita vyake vya ufisadi.”

Taarifa zinasema kuna mbunge ambaye ameandaliwa kutoa hoja ya kutokuwa na imani na spika na kutaka Bunge limjadili na hatimaye kupiga kura.

Watoa habari wanaeleza kuwa tayari zipo kura za “kutosha tu” kumuondoa spika madarakani, ingawa mmoja wa watetezi wa Sitta amenukuliwa akisema, “Hao wanaweweseka tu. Wanamtisha nani?”

Rais Kikwete alipozungumza mara ya mwisho na waandishi wa habari kwa kirefu hasa kuhusu yale yaliyotokea Dodoma, aliashiria kwa umma kuwa hali ndani ya chama chake si shwari.

CCM imeghubikwa na kashfa za kifisadi na hali ya serikali yake ambayo baadhi ya watu wanaamini inafuata nyayo zilezile za mtangulizi wake, Benjamin Mkapa siyo nzuri sana; na kwamba kuna mpasuko ambapo hata baadhi ya watu wanaogopana kiasi cha kuweza kulishana sumu.

Alipoulizwa kuhusu suala la Richmond na hasa Lowassa ambaye ni rafiki yake wa siku nyingi, Kikwete alituma ujumbe mfupi ambao ndio ulimfanya Lowassa siku chini ya saba baadaye, kumjibu Kikwete katika mtindo ambao umeonekana ni wa “kumbipu ” rais.

Alipokuwa akijibu swali la Bw. Joseph Machumu, Rais Kikwete alieleza kuwa “katika mapambano ya rushwa hakuna udugu wala urafiki, na suala la kuamua nani ashitakiwe au nani asishitakiwe halipo katika mamlaka yangu, hilo ni la Mkurugenzi wa Mashataka wa Serikali (DPP.)”

Alisema  kuwa endapo DPP akiridhika kwamba, mtu fulani ana shitaka la kujibu mahakamani, wanastahili kumfikisha mahakamani bila ya ushauri kutoka kwangu “kwa sababu katika vita hii hakuna rafiki wala ndugu.”

Kauli hiyo ya Kikwete ilichukuliwa na kambi ya Lowassa kuwa ni kujaribu kujitenga nao na walihitaji kumjibu Kikwete kiaina na kumtumia ujumbe wa wazi kuwa mabaya yote ambayo wao wanahusishwa nayo, yeye naye yumo.

Hilo ndilo wafuasi wa Lowassa wanajaribu kuonyesha hata sasa. Wanataka Kikwete aone na ajisikie kuwa hawezi kuwanyoshea wao kidole bila na yeye mwenyewe kujinyoshea.

Akizunguzumza na gazeti moja la kila siku nchini hivi karibuni, Lowassa alionekana kujibu hoja ya “urafiki” na Kikwete. Alisema kwamba urafiki kati yao umetoka mbali.

“Hatukukutana barabarani. Bali urafiki wetu ni wa tangu chuo kikuu. Hivyo hatuwezi kutenganishwa na kikundi cha watu wachache,” Lowassa alisisitiza.

Aidha, Lowassa alikumbushia pia staili yake kuwa Kikwete hakufika hapo alipofika kivyakevyake, bali “mwaka 1995 tulikubaliana tukaenda Dodoma kuchukua fomu za urais tukiwa pamoja, kwamba akipata mmoja ni sawa tu na amepata mwingine.” 

Kauli hizo mbili zilikuwa zina lengo la kumkumbusha Kikwete kuwa hawezi leo hii kuwageuka marafiki zake hao wa zamani kwa kisingizio cha kuongoza vita dhidi ya ufisadi.

Hakuishia hapo. Alisema, “Mwaka 2005 nikaamua kumpisha mwenzangu kwani namwamini ana uwezo, nami nikamuunga mkono na kuendesha hata vikao vyake vya kampeni.”

Ni wazi kwamba kauli hiyo ilikuwa inamuweka Kikwete kwenye kona ya ulingo wa kisiasa ambapo marafiki zake wanamkumbusha kuwa hata urais alionao sasa ni kwa sababu Lowassa alikubali “kumpisha.”

Wachambuzi wa kisiasa nchini wanasema kauli hizo za Lowassa zimechukuliwa kuwa ni ujumbe kwa Kikwete kuwa asithubutu kuwakana sasa kwani wanayajua mambo yake na wanajua jinsi gani yeye mwenyewe ni sehemu ya baadhi ya mambo ambayo wao wanatuhumiwa.

Rais Kikwete kabla ya kuwa rais amewahi kushika wizara mbalimbali ambazo leo nazo zinaguswa na tuhuma za ufisadi. Miongoni mwa wizara alizowahi kuziongoza ni ile ya Nishati na Madini, Fedha na Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa.

Suala jingine ambalo linatarajiwa katika mkutano huu wa bunge, hasa litakapoletwa tena suala la Richmond, ni utetezi wa nguvu wa Lowassa ambao unaweza kutangulia mchakato wa kumjadili spika. 

Utetezi huu ambao utakuwa ni wa kwanza kwa Lowassa bungeni unatarajiwa kusababisha kundi la kina Mwakyembe kujikuta wakikejeliwa na nguvu zao kukatwa makali, taarifa zimeeleza.

Mwelekeo wa utetezi huu umeanza wiki chache zilizopita ambapo baadhi ya wabunge ambao walionekana huko nyuma kuwapinga kina Mwakyembe na wale wajiitao wapambanaji, walipoanza na wao kujitokeza na kuunga mkono “vita vya ufisadi.”

Baadhi ya wabunge hao ni pamoja na Sofia Simba, John Chiligati na mbunge wa kuteuliwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba.

Mtoa taarifa anasema Lowassa akisimama kutoa utetezi wake, bunge litalipuka kwa shangwe na wabunge wengi wataonekana kumuunga mkono na kusababisha kambi ya kina Mwakyembe “kuubuka.”

Lakini jambo moja la wazi ni kwamba kambi hizi mbili kwa jinsi zilivyogawanyika sasa, haziwezi kamwe kukaa pamoja katika chama kimoja.

Kambi hizi mbili hazina budi kugawanyika kwani haziwezi kupatana na hilo linatokana na udhaifu mkubwa wa kiuongozi ndani ya chama unaoonyeshwa na mwenyekiti wake Rais Kikwete. Bali hakuna kambi inayotaka kuhama CCM

Mmoja wa watetezi wa Lowassa anasema kwa mijadala itakayovurumishwa Dodoma, hata uchaguzi mkuu wa urais na wabunge unaweza kuitishwa mapema zaidi mwakani kuliko inavyotarajiwa.

“Hili halijawahi kutokea na halikutarajiwa, lakini linawezekana,” ameeleza mbunge wa CCM kanda ya kati.

Iwapo yote haya yatatendeka, wananchi  wanaofikiri kuwa walikuwa wameona mwisho wa kisiasa wa aliyekuwa waziri mkuu kutokana na kashfa ya mkataba tata wa Richmond, watajilaumu kuwa walishindwa kusoma alama za nyakati, ameeleza mtoa habari 

Kwani kujiuzulu kwa Lowassa hakujamfutia mashabiki, wapenzi na watu walioamini katika uongozi wake na ambao wako tayari kufanya lolote kuona anarejea kileleni.

Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe ndiyo ilionyesha kuwa kampuni ya Richmond isingeweza kupata tenda ya kuleta majenereta ya kufua umeme pasipo shinikizo na msukumo toka ofisi ya waziri mkuu.

Tangu ajiuzulu, miaka miwili iliyopita, kundi linalomtetea Lowassa ndani na nje ya bunge limekuwa likiamini kuwa Lowassa hakupewa nafasi ya kuelezea upande wake na kujitetea ipasavyo na kwamba ripoti ya Kamati Teule ililetwa bungeni kwa shabaha ya kumtega.

Kundi hili ambalo linamlaumu pia hata Rais Kikwete, likidai kuwa ndiye mtu pekee na mwenye uwezo ambaye angezuia Lowassa kujiuzulu; ndilo linadaiwa kuandaa matukio makuu bungeni katika mkutano ulioanza jana.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: