Mkapa aangukia Kikwete


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 21 April 2009

Printer-friendly version
Akutana na vigogo kuomba msaada
Tuhuma mpya zazidi kumuandama
RAIS mstaafu  Benjamin Mkapa

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa amelalamika kuwa anasakamwa na wanasiasa na anachafuliwa, MwanaHALISI limeambiwa.

Kwa miaka miwili mfululizo sasa, Mkapa amekuwa akitajwa na kuhusishwa na baadhi ya tuhuma za ufisadi na utovu wa “utawala bora” wakati wa kipindi chote cha utawala wake – 1995 hadi 2005.

Kufuatia malalamiko hayo, wachunguzi wa siasa za Tanzania wanasema inawezekana ukaidi wa Mkapa umeyeyuka na sasa yeye ameona kuwa “ni maji shingoni.”

Taarifa zinasema Mkapa alitoa malalamiko yake kwa mwanasiasa mmoja nchini (jina tunalo) nyumbani kwake, Sea View, Dar es Salaam hivi karibuni.

Alimkomalia mwanasiasa huyo kuwa na      yeye anashiriki kumchafua huku akionyesha kuwa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ya “kuwaacha viongozi wastaafu kupumzika” kuwa imeshindikana kutekelezwa.

Rais Kikwete aliwaambia waandishi wa habari mwaka 2007, alipoulizwa iwapo atachukua hatua dhidi ya Mkapa kufuatia tuhuma alizokuwa akibebeshwa, kuwa viongozi waliostaafu waachwe wapumzike.

Kilio cha Mkapa kimekuja kufuatia mlolongo wa tuhuma za kale na sasa kurudiwa mara kwa mara na kumnyima, yeye na familia yake, kuishi kwa raha hata katika jiji la Dar es Salaam ambako aliwahi kukutana na vijana mitaani wakiimba “Fisadi! Fisadi! Fisadi!”

Chanzo cha taarifa kinasema, hata hivyo, mwanasiasa huyo hakumsaidia Mkapa, kwani alikana kumkashifu na kusema angekuwa anataka kumkashifu, angefanya hivyo kwa vile alikuwa na ushahidi wa mambo yake mengi.

Huyo ni mwanasiasa wa pili katika kipindi cha miezi miwili kukutana na Mkapa. Mwingine ambaye ni waziri mwandamizi anadaiwa kumwambia Mkapa kuwa hakuna anayemwandama bali “mambo ni mazito.”

Taarifa zinasema waziri huyo alimweleza kuwa ahadi ya rais Kikwete ipo palepale lakini kwa hapo alipofika, ingekuwa vema naye (Mkapa) akajitahidi kujenga upya sura yake kwa “kurejesha baadhi ya mali unazodaiwa kumiliki kutoka serikalini.”

“Ni kweli nimekutana na Mkapa. Tumezungumza mengi. Nimemwambia tutakulinda, lakini na wewe jaribu kujisafisha kwa kurudisha mali serikalini, hasa ule mgodi wa Kiwira,” chanzo cha habari kimemnukuu waziri wa Kikwete akisema.

Mkapa anahusishwa na umiliki wa mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira mkoani Mbeya kupitia kampuni yake ya ANBEN anayomiliki na mkewe, Anna ikiwa miongoni mwa makampuni matano yaliyoingia ubia na kampuni ya TanPower Resources Company Limited.

Kupatikana kwa taarifa kuhusu waziri kubadilishana mawazo na Mkapa kunathibitisha kuwepo ufuatiliaji wa karibu wa Rais Kikwete kuhusu tuhuma zinazomkabili Mkapa.

Wakati Mkapa anatajwa kukutana na waziri na mwanasiasa machachari akitaka hatua zichukuliwe kumlinda, tuhuma mpya zimeibuka dhidi yake.

Mkapa, kupitia TanPower Resources Limited, anahusishwa na dhamana ya serikali ya kupata mkopo wa Sh. 17.7 bilioni kutoka CRDB Bank kwa ajili ya kuendeleza mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira.

Kwanza, inadaiwa kuwa Mkapa alimiliki kampuni akiwa bado rais (ANBEN 1998) wa nchi na hivyo atakuwa alitumia nafasi yake kujinufaisha binafsi na kampuni yake.

Pili, kwa kuwa alikuwa bado madarakani na kwa kuwa uamuzi wa kuuza Kiwira ulifanyika ndani ya Baraza la Mawaziri aliloliongoza, basi uamuzi huo ulikuwa wa upendeleo kwa kampuni yake.

Tatu, hata waziri aliyejenga hoja mbele ya baraza la mawaziri, Daniel Yona ametokea kuwa mshirika katika umilikaji wa mgodi huo, jambo ambalo haliendani na utawala bora.

Nne, mkataba wa kampuni ya Mkapa kuuza umeme kwa Tanesco ulifungwa Mkapa akiwa madarakani (Septemba 2005), jambo linaloonyesha upendeleo kwa kampuni yake na utovu wa utawala bora.

Kwa mujibu wa mkataba huo, kampuni ya Mkapa ingelipwa (dola 3.65 milioni – sawa na zaidi ya Sh. 4 bilioni kila mwezi.

Tano, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imegundua mwanzoni mwa mwaka huu, kuwa fedha za mkopo zilizodhaminiwa na serikali (Sh. 17.7 bilioni) hazikutumika kama ilivyokusudiwa.

Kutokana na kutotumia fedha palipohitajika, jenereta moja ya kuzalisha umeme imechakaa kiasi cha kutoweza kufanya kazi; na nyingine ina uwezo wa kuzalisha megawati moja tu ya umeme kutoka megawati sita wakati mgodi unabinafsishwa.

Nyaraka zinaonyesha kuwa TanPower Resources Limited kimkataba ilitakiwa kuzalisha megawati 200 za umeme kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza ni kuzalisha megawati 50 kufikia Julai 2007 na megawati 150 ifikapo Machi, mwaka huu. Yote hii sasa ni ndoto.

Uchakavu wa miundombinu umeathiri pia uzalishaji wa mkaa wa mawe na  mwekezaji “ameuza baadhi ya vifaa vya mitambo kama vyuma chakavu,” wameeleza wafanyakazi mgodini.

Sita, TanPower Resources Limited imeshindwa kulipa wafanyakazi wake 1,632 kwa karibu mwaka sasa licha ya kuonyesha kwenye mchanganuo wake kwamba ilitenga Sh. 3.0 bilioni kwa ajili hiyo.

Katika mazingira haya, serikali ambayo bado ina hisa katika mgodi huo (asilimia 15) italazimika kuwalipa wafanyakazi kwa mtindo wa Tanzania Railways Limited (TRL) ambako serikali imekuwa ikikingia kifua wawekezaji.

Mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira ulioanzishwa kwa msaada wa serikali ya China, Novemba 1988, ulitarajiwa  kuzalisha tani 150,000 za mkaa ghafi kwa mwaka na kwamba uzalishaji ungekua hadi kufikia tani milioni moja kwa mwaka.

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, tayari imependekeza mgodi wa Kiwira urejeshwe serikalini, jambo ambalo waziri aliyekutana na Mkapa anapendekeza.

Tathmini ya mgodi mwaka 1988 wakati ukibinafsishwa, na Mkapa akiwa madarakani, ilionyesha ulikuwa na thamani ya Sh. 4.2 bilioni. Lakini tathmini iliyofanywa na Taasisi ya Ardhi mwaka 1991 ilionyesha thamani ya Sh. 7 bilioni.

Kamati ya Bunge inasema imeshindwa kuelewa vigezo vilivyotumika kutupilia mbali tathmini iliyofanywa miaka mitano baadaye na serikali kuamua kuuza hisa zake kwenye mgodi huo kwa gharama ya Sh. 700 milioni tu.

Hata hivyo, kampuni ya Mkapa ililipa Sh. 70 milioni tu.

TanPower Resources Limited ina wanahisa watano – kila mmoja akiwa anamiliki hisa 200,000 ikiwamo ANBEM Limited inayomilikiwa na Mkapa na mkewe.

Makampuni mengine ni Devconsult International Limited ya S.L.P. 65440 Dar es Salaam inayomilikiwa na Daniel Yona na Dan Yona.

Mengine ni Universal Technologies Limited inayomilikiwa na Wilfred Malekia na Evans Mapundi; Choice Industries Limited inayomilikiwa na Joe Mbuna na Goodyear Francis; na Fosnik Enterprises Limited inayomilikiwa na Nick Mkapa, Foster Mkapa na B. Mahembe.

Makampuni matatu ya mwisho yanatumia anwani moja ya posta ambayo ni S.L.P 8764 Dar es Salaam.

Mkapa anakabiliwa pia na tuhuma za kuuza benki ya NBC kwa “bei poa,” na kupokea Sh. 500 milioni kutoka benki ya Afrika Kusini (ABSA) iliyonunua NBC ambazo hazikutolewa maelezo.

Vilevile Mkapa anatuhumiwa kuuza makampuni ya umma kwa kasi kana kwamba ameshikiwa bakora; kuuza nyumba za serikali kwa njia ya upendeleo na kwa bei ya bure na kuingilia zabuni ya Hotel 77 ya Arusha ambako serikali imelazimika kulipa fidia ya Sh. 3.3 bilioni na gharama nyingine.

Hivi karibuni, wakili wa mahakama kuu amekaririwa akidai kuwa Rostam Aziz, mbunge wa Igunga, alimwambia asaini hati za mikataba ya kampuni ya Kagoda Agriculture Limited ili wachote zaidi ya Sh. 40 bilioni kutoka Benki Kuu (BoT). 

Alisema, na bado haijakanushwa, kwamba aliyetoa amri ya kuchukua fedha hizo kutoka BoT, mbele ya Katibu wa CCM wakati huo Philip Mangula na marehemu Daudi Ballali, ni Benjamin Mkapa.

Asasi mbalimbali za kiraia na wananchi wa kawaida wamekuwa wakitaka serikali kumchukulia hatua Mkapa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: