Mkapa akengeuka tuhuma zake


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 27 May 2008

Printer-friendly version
Atuhumu kutungiwa uongo na wenye chuki
Ashindwa kugusia tuhuma mahsusi
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa amekengeuka tuhuma zake na kujikita katika mayowe na shutuma akisema kuwa wanaomtuhumu kwa ufisadi wanamuonea bure maana yeye si tajiri.

Mkapa, mwanasiasa aliyepigiwa debe na Mwalimu Julius Nyerere kama "mtu safi" wa kushika madaraka ya kuongoza Tanzania mwaka 1995, aliwaambia wananchi wa kijijini kwake Lupaso, Masasi, mkoani Mtwara juzi kwamba wanaomtuhumu kuibia nchi wana chuki naye kwa kuwa aliwanyima vyeo alipokuwa rais.

Mkapa alitoa maelezo hayo wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya tiba kwa kituo cha afya kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki kijijini Lupaso. Hakusema wapi amepata vifaa hivyo wala thamani yake.

"Mimi si tajiri, nimeomba msaada nimepewa? nimejinyima na mke wangu ndio tukaweza kusafirisha vifaa hivi kutoka Canada hadi Dar es Salaam. Kutoka hapo hadi hapa (kijijini) vimesafirishwa na Serikali" sikuwa na uwezo wa kununua vifaa kama hivi. Nitapata wapi fedha za kuvinunua,? alisema.

Mkapa hakutaja tuhuma mahsusi anazozikana bali alitoa maelezo ya jumlajumla ya kusema hakufanya kosa lolote alipokuwa Ikulu kutoka Novemba 1995 hadi Desemba 2005.

Hiyo ni mara ya pili kujitokeza hadharani kijijini kwake kujibu tuhuma dhidi yake, wakati amekuwa mgumu wa kukutana na waandishi wa habari anapokuwa jijini Dar es Salaam au katika miji mingine kama mjini Dodoma kunakofanyika vikao vya Bunge na vikao vya juu vya chama chake, CCM, yeye akiwa mmoja wa wajumbe wa vikao hivyo.

Kwa muda mrefu sasa, kumekuwa kukitolewa tuhuma kwenye vyombo vya habari nchini kumhusu yeye zikiwemo za kukiuka maadili ya uongozi alipokuwa madarakani kwa kujifanya mjasiriamali na kuanzisha kampuni ya kibiashara na kununua mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya uliokuwa chini ya shirika la umma.

Imeelezwa kwamba Mkapa alinunua mgodi huo chini ya kampuni ya Tan Power Resources Limited na kutajwa kama mwenye hisa mmoja wapo, pamoja na mtoto wake, Nicholas, mkewe, Anna, na aliyekuwa waziri wa fedha na baadaye nishati na madini, Daniel Yona.

Kutokana na mgodi huyo, taarifa zimesema kwamba amekuwa akinufaika kwa kulipwa Sh. 140 milioni kwa siku kutoka Shirika la Umeme nchini (TANESCO) linalonunua umeme unaozalishwa na mgodi huo.

Mkapa pia anatuhumiwa kuwa alielekeza kuchotwa kwa fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu 2005 kupitia makampuni mbalimbali yakiwemo hewa ambayo yamethibitishwa kuwa yalighushi nyaraka za kuhalilisha kuwa wanaidai serikali.

Makampuni kadhaa yalianzishwa na kuchotewa zaidi ya Sh. 133 bilioni zilizokuwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu. Ufisadi huo ni moja ya kashfa nzito zinazoikabili serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Kwa sasa, Timu ya Rais inayoundwa na taasisi tatu chini ya uongozi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, inaendelea kufuatilia ugunduzi wa maodita wa Ernst&Young waliokagua akaunti hiyo na kubaini upotevu wa kiasi hicho cha fedha katika mwaka wa fedha wa 2005/06 pekee.

Kashfa hiyo imesababisha Rais Kikwete kumfukuza kazi 8 Januari, mwaka huu, aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Dk. Daud Ballali ambaye aliajiriwa kwa mkataba mwaka 1997 chini ya utawala wa Mkapa.

Dk. Ballali, mara baada ya ugunduzi huo kubainika na maodita hao kukabidhi ripoti yao serikalini, aliripotiwa kuwa amekwenda Marekani kwa matibabu ambayo hayakuwahi kuelezwa hasa ya ugonjwa gani hadi alipotangazwa kuwa amefariki nchini humo katikati ya mwezi huu.

Mwezi uliopita, serikali, kupitia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ilisema bungeni, kwamba itachunguza tuhuma dhidi ya Mkapa na kuchukuwa hatua zifaazo; kama ni mahakamani kwa kumshitaki iwapo itabainika alifanya kosa la jinai au la ukiukaji maadili ya uongozi.

Mpaka aliingia madarakani kwa makeke akianza kutangaza mali zake kama mfano wa uadilifu aliojionyesha, lakini alipoondoka Ikulu, hakutangaza tena ametoka akimiliki mali gani zaidi ya zile za awali; gari bovu, nyumba ya kawaida na shamba.

Awamu ya tatu ya uongozi wa Tanzania iliyoongozwa naye, inatajwa kama awamu iliyosababisha matatizo makubwa ya kiuchumi nchini hasa katika eneo la kufisidi raslimali za taifa kama vile migodi ya madini mbalimbali na mikataba inayoifanya serikali kulipa mabilioni ya shilingi kwa huduma duni.

Raslimali nyingi zilikwenda mikononi mwa wageni kwa mwamvuli wa sera ya ubinfasishaji, huku serikali yake ikishindwa kusema fedha zilizopatikana kutokana na ubinafsishaji ziko wapi.

Kutokana mwenendo wa mambo ulivyokuwa alipokuwa madarakani, anaonekana kama mstaafu mwenye miliki kubwa ya mali kiasi cha kuitwa bilionea.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: