Mkapa akianza, serikali ikimbie


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 29 September 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

MATUKIO mawili yanatarajiwa kubadilisha mwelekeo wa kiuchumi wa eneo la mashariki mwa Bara la Afrika katika siku za usoni.

Kwanza, kugundulika kwa mafuta nchini Uganda na pili kujitenga kwa Sudan Kusini kutoka Jamhuri ya Sudan.

Ugunduzi wa mafuta nchini Uganda unamaanisha kwamba katika kipindi cha miaka kumi ijayo, pato la taifa la nchi hiyo litakua zaidi ya mara 20 kutoka ilivyo sasa.

Vilevile, iwapo Sudan Kusini itafanikiwa kujitenga kutoka Jamhuri ya Sudan katika kura ya maoni itakayopigwa Januari mwakani, nchi mpya ya 54 itazaliwa katika Bara la Afrika. Hilo likitokea, kutakuja na changamoto mpya za kiuchumi.

Taifa la Sudan lina utajiri mkubwa wa mafuta, madini na ina eneo linalofaa kwa kilimo. Katika mazingira hayo, nchi zitakazokuwa na uhusiano mzuri na nchi hiyo, ni lazima zitanufaika.

Ndiyo maana jirani zetu wa Kenya tayari wametumia kiasi cha Sh 5 bilioni (dola milioni tano za Marekani), kuisaidia Sudan Kusini kuboresha sekta yake ya utumishi wa umma.

Kwamba pamoja na ukweli kuwa Kenya yenyewe bado inategemea ufadhili wa wahisani katika bajeti yake, imeona kuna haja ya “kuisaidia Sudan Kusini kujiendeleza.”

Tayari nchi ya Kenya imeanza ujenzi wa bandari ya Lamu inayokadiriwa kugharimu zaidi ya dola za Marekani 1 bilioni (sawa na Sh. 1.5 trilioni), ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka nchi hiyo mpya.

Hivi sasa, Sudan Kusini inatumia bandari ya Port Sudan iliyopo umbali wa kilomita 1600 kutoka Juba, mji mkuu wa Jamhuri ya Sudan, lakini ile ya Lamu itakapokamilika, umbali utakuwa kilomita 1400 kutoka Juba.

Kenya inajua kwamba fedha wanayoitumia sasa, itakuja kujilipa yenyewe kwa muda mfupi ujao, mara pale Sudan Kusini itakapoanza kutumia bandari hiyo.

Uganda, ambayo haina bandari ya bahari, tayari imekamilisha ujenzi wa barabara kutoka Gulu hadi Juba, ambayo itatumiwa na bidhaa zitakazokuwa zikisafirishwa kutoka Kenya.

Ukienda Sudan Kusini wakati huu, utakuta majeshi ya Kenya yakitoa mafunzo kwa majeshi ya Sudan Peoples Liberation Army (SPLA), litakalokuwa jeshi la nchi hiyo mpya.

Kwa ufupi, wenzetu katika ukanda huu wa mashariki ya Afrika, wameanza kujiandaa na ujio wa Sudan Kusini na mafuta ya Uganda.

Kuna mkubwa mmoja wa Afrika Mashariki bado amelala usingizi wa pono katika eneo hili – Tanzania!

Nina imani isiyo na shaka kwamba Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lina uwezo mkubwa wa kutoa mafunzo kwa SPLA kuliko lile la Kenya.

JWTZ ina historia ya kutoa mafunzo kwa majeshi ya wenzetu. Wamefanya hivyo Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Msumbiji, Zimbabwe na kwingine.

Tatizo kubwa ambalo naliona kwa nchi yetu ni namna tunavyoshindwa kutumia ushawishi wetu wa kidiplomasia na kijeshi kwenye kuiletea maendeleo nchi yetu.

Tanzania imekuwa na kazi ya kusaidia nchi kujikomboa na kisha kuondoka zake. Wenzetu wanasaidia huku wakiwa na jicho la pili la namna gani watafaidika kiuchumi.

Kama viongozi wetu wangekuwa na macho ya kiuchumi, leo hii, mizigo ya nchi kama Uganda, Zambia na DRC ingekuwa inapitia katika bandari yetu ya Dar es Salaam badala ya ile ya Mombasa na ya Afrika Kusini.

Tungekubaliana mapema na akina Yoweri Museveni kwamba sisi tutamwaga damu yetu kumng,oa nduli Iddi Amin na tutalifundisha jeshi lenu bure, lakini mtatumia bandari yetu kwa miaka 30, mkiwa na amani, wasingekataa.

Tungezungumza maneno ya namna hii na wenzetu wa Angola na Msumbiji (hawa wana bandari yao, lakini tungeweza kufaidika kwenye maeneo mengine), leo nchi ingekuwa inavuna matunda ya damu zetu zilizomwagika.

Ukiondoa Zambia na Msumbiji, pengine sisi ndiyo nchi ya Afrika iliyopata shida sana na harakati za ukombozi nchini Afrika Kusini, na baada ya akina Nelson Mandela kuingia madarakani mwaka 1994, tungekuwa tukifaidika leo. Lakini wapi.

Sisi kazi yetu imekuwa kwenda kumwaga damu, kuzaa watoto na kupukusa vumbi na kurejea zetu kwetu. Tumemaliza ! Hii ni mbaya.

Kwa bahati nzuri, inaonekana bado tunaheshimika. Watu wenyewe wa Sudan wamemwambia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon, amteue Benjamin Mkapa, rais mstaafu wa Tanzania, awe kiongozi wa jopo la kuangalia namna upigaji kura huo utakavyoendeshwa.

Watu wa Sudan hawakuona Mkenya wala Mganda anayefaa kwa kazi hiyo. Wamemwambia Ban kuwa wanamtaka Mtanzania kwa vile wanajua sisi ndiyo tuliyomlea kiongozi wao mpendwa, hayati John Garang.

Kwa bahati mbaya sisi ndiyo tumelala usingizi wa pono. Tunajua kukaa na akina Garang na kunywa nao chai kisha basi.

Nafikiri wakati umefika sasa ambapo nchi yetu inatakiwa kubadilika. Kwa nafasi hii ambayo Mkapa amepewa, serikali inaweza kuamua kuangalia ni kwa namna gani nchi yetu inaweza kunufaika na taifa hili jipya.

Kama watu wa Sudan Kusini watapenda chochote kutoka kwetu, huu ndiyo wakati wa kuingia nao mkataba. Kama watahitaji msaada wowote wa kujiweka sawa, tuwape ili tuwekeze kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Mara tu Mkapa atakapoanza rasmi shughuli zake hizi mpya za UN, ni muhimu kwa nchi yetu kufuatana naye. Ni kazi ya serikali kubaini ni kwa namna gani.

Huu ni wakati wetu kuanza kutumia vizuri ushawishi wetu wa kijeshi na kidiplomasia. Wakati wa kukalia sifa zisizo na maana ya kiuchumi umepita. Tubadilike.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: