Mkapa alimtosa Mwandosya


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 03 June 2008

Printer-friendly version
Alimzunguka katika maamuzi
Mwenyewe alitaka kujiuzulu
Mark Mwandosya

MCHAKATO wa ubinafsishaji wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL), chini ya serikali ya Rais Benjamin Mkapa ulighubikwa na vitimbi na nusura umng'oe Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi.

MwanaHALISI limegundua kuwa uuzaji huo, na ununuzi wa rada, vilifanywa kwa amri "kutoka juu" badala ya taratibu zilizofahamika.

Mara kadhaa mawaziri wanaohusika waliwekwa pembeni na mchakato kuendeshwa na watu wanaosadikiwa kuwa karibu na rais.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya serikali zimeeleza kuwa huo ndio mtindo uliotumika pia kuongeza mkataba wa kampuni ya makontena ya TICTS ambapo waziri husika alipelekewa nakala ya barua "kwa taarifa tu."

Serikali iliuza asilimia 35 za TTCL kwa kampuni ya MCI ya Uholanzi kwa dola za Marekani 120 milioni, lakini kampuni ililipa dola 60 milioni tu, hivyo kuzua mgogoro mkubwa ulioshughulikiwa na wasuluhishaji wa kimataifa.

Kampuni ya MCI iliongeza malipo kwa dola 4.5 milioni na kukabidhiwa menejimenti ya TTCL kwa kipindi cha miaka minne kuanzia Februari 2001 hadi Februari 2005 ambapo ilichukuliwa na kampuni ya simu za mkononi ya Celtel International.

Kwa mujibu wa taarifa za ikulu, watu wawili waliokuwa karibu na Mkapa walipewa jukumu la ufuatiliaji uuzaji wa TTCL hadi ilipopata mnunuzi.

Mmoja wa watu hao ni mfanyabiashara mashuhuri wa Dar es Salaam na mwingine ni mmoja wa watu mashuhuri waliokuwa katika timu ya kutafuta urais wa Mkapa mwaka 1995.

Ilikuwa wakati wa mchakato huo wa kuuza TTCL, aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Prof. Mark Mwandosya, baada ya kuona amewekwa pembeni, alipanga kujiuzulu kwa kile wakati huo aliita "heshima yake."

"Waziri aliita familia yake na kuwaambia kuwa anataka kujiuzulu. Akawaita hata ndugu na marafiki zake wa karibu na kuwataka ushauri. Hakika alitaka kuacha kazi," ameeleza mmoja wa walioitwa kutoa ushauri.

Taarifa zinasema miongoni mwa waliomshauri kubaki kazini alikuwa mke wake na mmoja wa marafiki zake waliosema kuwa tayari aliishajuzulu nafasi ya Katibu Mkuu wakati wa Utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi na kwamba kujiuzulu kwake hivi sasa kusingemsaidia kisiasa.

Imefahamika kuwa katika kikao cha baraza la mawaziri, Mwandosya alipinga hoja ya kubinafsisha TTC kwa nguvu zake zote. Haikueleweka mara moja ilikuwa kwa hoja zipi.

Alipopigiwa simu juzi Jumatatu, kuulizwa juu ya suala hili, Mwandosya alisema hakuwa na muda wa kujadili suala hilo, lakini aliongeza, "Umepata wapi taarifa hizo? Basi muulize huyo aliyekupa taarifa za awali."

"Mimi ni waziri. Wakati huo pia nilikuwa waziri. Nimekula kiapo cha kutunza siri za Baraza la Mawaziri. Siwezi kuvuja hata neno moja la taarifa za vikao," alisema kwa kumkatisha tama mwandishi wa taarifa hizi.

Mawaziri wengine wawili waliokuwa katika Baraza la Mawaziri na wanadaiwa kupinga ubinafsishaji wa TTCL, hawakupatikana kutoa maoni yao.

Imefahamika pia kwamba ununuzi wa rada iliyogharimu Sh. 70 bilioni, ulifanywa bila kuhusisha waziri wa mawasiliano na uchukuzi; badala yake mchakato uliundiwa kamati maalum.

Kwa upande wa mkataba wa TICTS na nyongeza ya miaka 15 hata kabla mkataba wa kwanza haujamalizika, imefahamika kuwa waziri huyo alikwepwa; badala yake alipelekewa nakala ya barua kwa taarifa tu.

Kwa mujibu wa nyaraka za wizara ya fedha, alikuwa Waziri wa Fedha Basil Mramba aliyemwandikia barua Kamishena Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akimweleza kuwa ameagizwa na rais kuhusu nyongeza ya miaka 15 ya mkataba wa TICTS.

Ni nakala ya barua hiyo, inayoitaka TRA kutekeleza tu maagizo kutoka juu, ilipelekwa kwa waziri.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: