Mkapa amepanda mbigili Igunga; atapuuzwa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 14 September 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa amejitosa katika kampeni za uchaguzi mdogo jimboni Igunga, mkoani Tabora kwa makeke na tambo za kila aina.

Akihutubia umati wa watu kwenye viwanja vya Sokoine, mjini Igunga, kwenye ufunguzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jumamosi iliyopita, Mkapa ameeleza tabia yake ikiwa ni pamoja na lugha ya kibabe kama “kukanyaga” wapinzani.

Mkapa alitumia muda mwingi kuponda wanaopinga hatua yake ya ubinafsishaji na uuzaji wa makampuni na mashirika ya umma; hasa ubinafsishaji tata wa iliyokuwa Benki ya Biashara (NBC 1997).

Amejitetea kuwa hatua hiyo ilikuwa sahihi kwa maelezo kuwa “ilikuwa mzigo kwa taifa.”

Amesema, “Wakati naingia madarakani kulikuwa na benki moja ya biashara ambayo ni NBC, lakini ilikuwa inaomba ruzuku serikalini, kitu ambacho hakikuwa sahihi. Tukaibinafsisha kwa kuwa huwezi kuwa na benki ya biashara inayoomba ruzuku.

“Lakini siyo yote, tukabaki na asilimia za serikali. Wanasema nimeuza benki yetu, siyo hivyo. Nimeuza madeni yetu na kuisaidia nchi,” ameongeza.

Hadi sasa, hakuna anayejua kilichomsukuma Mkapa kuzungumzia ubinafsishaji wa NBC 1997 Ltd., kwenye kampeni za ubunge jimboni Igunga. Wala hakuna anayejua, iwapo kama Mkapa alifanya mashauriano na wenzake ndani ya chama kabla ya kuliibua upya jambo hilo.

Mkapa na chama chake wanajua kuwa uuzwaji hisa za NBC ni moja ya vitu vinavyotajwa kama doa kubwa la serikali ya CCM katika mchakato mzima wa ubinafsishaji, ukodishaji menejimenti na uuzaji hisa wa mashirika na makampuni ya serikali chini ya sera ya ubinafsishaji iliyoratibiwa na utawala wa Mkapa.

Wala Mkapa na chama chake hawawezi kusema kilichofanyika hawakuwa wanakifahamu. Ndiyo maana pamoja na madhira yote yaliyotokea katika ubinafishaji, Mkapa bado anatetea uporaji wa rasimali za taifa kwa kudai eti NBC ilikuwa mzigo kwa taifa.

Wala Mkapa hawezi kusema pia kwamba kilichofanyika kilitekelezwa kwa mujibu wa sheria na katiba ambayo yeye aliapa kuilinda na kuitetea.

Mkapa anajua kama wengine wengi wajuavyo, kuwa uuzaji wa NBC ulijaa utata na ulitawaliwa na ghiriba. Kwamba serikali yake iliridhia benki iliyosheheni rasilimali, yakiwamo majengo na wateja, kuuzwa kwa bei ya kutupa ya Sh. 15 bilioni kwa kampuni ya kigeni – ABSA kutoka Afrika Kusini.

Muda mfupi baadaye uchunguzi ukaonyesha katika tawi moja pekee la Samora, jijini Dar es Salaam, kulikuwa na deni la Sh. 31 bilioni.

Je, kama benki iliulizwa kwa Sh. 15 bilioni iweje tawi moja tu la Samora katika kipindi cha muda mfupi liwe na deni la Sh. 31 bilioni? Hii inaonyesha thamani halisi ya NBC ilikuwa kubwa kuliko fedha ilizonunuliwa. 

Ni ufisadi katika mchakato wa uuzwaji wa NBC uliomsukuma Dk. Harrison Mwakyembe, kujiuzulu ujumbe wa bodi kwa kile kilichodaiwa kuwa ni “kutoa nje siri za vikao.”

Katika taarifa yake ya ukurasa mmoja baadaye, Dk. Mwakyembe alisema, “….naondoka kwenye bodi hiyo nikiwa na dhamira safi ya kwamba nimetimiza wajibu wangu wa kizalendo na ahadi ya nane ya Mwana-CCM isemayo: Nitasema kweli daima, fitina kwangu ni mwiko.”

Dk. Mwakyembe hivi sasa, ni mbunge wa Kyela na naibu waziri wa ujenzi.

Kabla, wakati au baada ya Mkapa kuridhia ubinafishaji wa NBC, taarifa zilieleza kuwa menejementi ya ABSA iliipa mkopo wa Sh. 500 milioni, kampuni ya ANBEM Ltd., inayomilikiwa na Benjamin W. Mkapa na mkewe, Anne Mkapa.

Kampuni ya ANBEM Ltd., haikuweka dhamana yeyote benki wakati inachukua mkopo huo. Badala yake, fedha zilizokopwa zilitumika kununulia nyumba ambayo baadaye Mkapa aliigeuza kuwa dhamana kwa benki. Yote haya akiwa ikulu.

Swali moja kuu la kujiuliza ni hili: Je, Mkapa amefanikiwa kuzima kelele za wananchi wanaolalamikia uporwaji wa rasilimali za taifa?

Je, ameweza kushawishi wananchi wa Igunga na Watanzania kwa jumla, kwamba katika kusimamia uuzaji wa NBC alifuata sheria, katiba na maadili ya viongozi wa umma? Jibu ni: Hapana.

Ibara ya 7(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano imeeleza wazi majuku ya kiongozi mkuu wa nchi kama Mkapa wakati akiwa madarakani.

Kwamba ana “…wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi…”

Vilevile viongozi wote wa umma “…watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya Nchi, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.”

Licha ya masharti hayo ya kikatiba, Mkapa anabanwa na masharti ya sheria nyingine za nchi. Kwa mfano, sheria ya maadili ya viongozi wa umma inayomtaka rais, katika kutekeleza wajibu wake, kutojiweka katika hali ambamo maslahi yake binafsi yatagongana na wajibu wake kama kiongozi wa umma; pamoja na kutojihusisha na mambo yenye migongano na maslahi binafsi.

Sheria ya maadili ya viongozi wa umma vilevile inataka kiongozi wa umma anapokuwa madarakani, kuwa mwadilifu, mwenye huruma, mtulivu, makini na anayetekeleza viwango vya juu vya maadili ili kujenga na kuendeleza imani ya umma kwa uadilifu wa serikali.

Je, ubinafishaji wa NBC ambao Mkapa anautetea ulitimiza viwango hivyo? Ulifanywa kwa kufuata maadili na uadilifu unaotajwa? Je, hauna harufu ya ukiukwaji maadili ya viongozi wa umma?

Kama yote hayo yalifanyika kwa uwazi bila hila wala ghiliba, hicho ambacho Dk. Mwakyembe aliita, “Naondoka kwenye bodi hiyo nikiwa na dhamira safi ya kwamba nimetimiza wajibu wangu wa kizalendo na ahadi ya nane ya Mwana-CCM isemayo: Nitasema kweli daima, fitina kwangu ni mwiko,” kimelenga nini?

Kwamba Mkapa hakumuita Dk. Mwakyembe, kumkanya kwa kauli yake hiyo, waweza kuwa sehemu ya ushahidi kuwa wote wawili hawakutaka mlipuko mkubwa wa kilichokuwa kinaendelea.

Kama ubinafishaji ulifuata maslahi ya umma, inakuwaje serikali iuze benki hii, ambayo ilikuwa na matawi nchi mzima kwa bei ya kutupa ya Sh. 15 bilioni?

Kama Mkapa anasema serikali iliangalia maslahi ya umma, inawezaje kudanganya kuwa benki haikuwa na thamani, wakati siku chache baadaye ikathibitika kuwa tawi moja la benki linadai zaidi ya Sh. 30 bilioni?

Kama Mkapa anasema alifanya haya kwa maslahi ya umma, ilikuwaje fedha ambazo ABSA walidai walizitoa kununua benki, zirejeshwe kwa mlango wa nyuma kwa kile kilichokuja kuitwa baadaye, “deni kutokana na kuudwa kwa benki ya NMB?”

Mkapa anajua kwamba agenda ya ufisadi ndiyo iliyosababisha kufanyika kwa uchaguzi mdogo katika jimbo la Igunga. Haikutarajiwa yeye awe wa kwanza kuendeleza mjadala huu unaobeba mustakabali wa taifa.

Lakini inafahamika kuwa historia ya Mkapa inafunikwa na kiwingu cha yeye mwenyewe kutoshikilia misingi ya utawala bora katika siku zake za mwisho za utawala wake.

Kazi nzuri aliyoifanya akiwa ikulu ilikuja kuharibiwa na yeye mwenyewe kuingia katika biashara akiwa bado ikulu; na kuibuka kwa mlolongo wa kashfa za wizi ndani ya Benki Kuu (BoT) wakati wa utawala wake.

Kuhusika kwake katika biashara hizo kulianza kuibuliwa na wapambe wa serikali ya awamu ya nne, jambo ambalo lilimfanya awe na wakati mgumu sana wa kujitokeza hadharani.

Alihangaika chinichini, akilalamika kwa viongozi wenzake wastaafu na hata kwa baadhi ya viongozi wa dini, kwamba serikali ya awamu ya nne ilikuwa “inafukua makaburi” na wakati mwingine alidai serikali hii “inajaribu kufunua uchi wa mzazi” na kwamba ingelaaniwa.

Kinachoonekana kimetokea ni kuwa, kutokana na kuelemewa na matatizo mengi, yakiwamo tuhuma za ufisadi, serikali hii imeamua kutengeneza muafaka na Mkapa ili kupeana unafuu wa muda.

Naye Mkapa, amelazimika kupanda jukwaani ili kujaribu kuwashawishi au kuwalazimisha wananchi kupuuza madai ya upinzani kuhusu ufisadi.

Hapohapo Igunga, Mkapa aliongelea serikali kufanya shughuli zake kufuatana na taratibu.

Kauli hii haiendani na yale yanayotendeka ndani ya serikali. Kila uchao, wananchi wanashuhudia wizi wa mabilioni ya shilingi ukitekelezwa na watendaji wa serikali na baadhi ya viongozi wa umma.

Kama kasi ya ufujaji wa rasimali za taifa ingekuwa kasi ya kutekeleza miradi ya maendeleo, basi taifa hili lisingekuwa ombaomba.

Kwa mfano, katika kipindi cha miaka mitatu – 2004 hadi 2006, watawala walikuwa tayari wamenyamazia wizi wa mabilioni ya shilingi kwa njia ya udanganyifu.

Wizi huu ulihusisha Sh. 133 bilioni katika akaunti ya madeni ya nje (EPA); Sh. 532 bilioni katika ujenzi wa majengo ya BoT ya Mtaa wa Mirambo, Dar es Salaam na Gulioni, visiwani Zanzibar.

Kulikuwa pia na wizi mkubwa wa mabilioni ya shilingi uliofanywa na makampuni ya Tangold Limited, Deep Green Finance Company na benki ya Nedbank ya Afrika Kusini.

Aidha, serikali ilinyamazia wizi wa dola za Marekani 118 milioni zilizopelekwa katika akaunti isiyojulikana ya Benki ya Nedbank Ltd., kama malipo ya madeni ya kampuni muflisi ya Meremeta Ltd., iliyokuwa inachimba dhahabu katika eneo la Buhemba wilaya ya Musoma, Mkoni wa Mara.

Ni katika kipindi hicho, serikali iliruhusu mkopo usio na riba wa dola za Marekani 5,512,398.55 kwa kampuni ya Mwananchi Gold Co. Ltd. 

Kati ya fedha hizo, deni la dola 2,807,920 limedhaminiwa kwa dhahabu ghafi ambayo ingenunuliwa kutokana na fedha za mkopo zilizotolewa na Benki Kuu yenyewe!

Kwa maana rahisi ni kwamba kampuni ya Mwananchi Gold haijatoa dhamana yoyote inayoeleweka kwa mabilioni ya shilingi ilizokopeshwa na BoT chini ya Gavana Dk. Daudi Balali anayedaiwa kufariki nchini Marekani.

Kwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, hadi kufikia mwezi Desemba 2006 Mwananchi Gold Co. Ltd., ilikuwa imeshindwa kulipa hata riba ya mkopo huo kwa kiasi cha dola za Marekani 62,847.91.

Sasa iwapo fedha hizo zingeelekezwa kwenye maendeleo, taifa hili lingekuwa wapi?

Kama Mkapa anasifia barabara ya kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam, miaka 50 baada ya uhuru, basi hapa kuna tatizo kubwa kwa viongozi wetu.

Ilitarajiwa Mkapa aeleze, kwamba taifa hili halihitaji kujikongoja kutokana na rasilimali lilizonazo na siyo kuporojea kwa kuomba wananchi wasisikilize ujumbe wa wapinzani.

Hapa rais huyu wa awamu ya tatu, amepanda mbigiri. Aweza, yeye na chama chake, kuvuna mbigiri.

Wananchi wana kiu ya mabadiliko – ikiwa ni pamoja na kuona CCM ikikaa pembeni ili wapate utawala mpya na bora zaidi, kwa njia ya sanduku la kura.

0
No votes yet