Mkapa: Anakwenda Igunga kuvuna aibu


Jacob Daffi's picture

Na Jacob Daffi - Imechapwa 07 September 2011

Printer-friendly version
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa

PAMOJA na majigambo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwamba kitashinda uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni Igunga, mkoani Tabora, Rais mstaafu Benjamin Mkapa anayekwenda kuzindua kampeni zake anaweza kuvuna aibu.

Tayari vyama vya upinzani, hususani Chama cha Demokrsia na Maendeleo (CHADEMA), vimeapa kueleza wananchi wa Igunga na Watanzania kwa jumla, yaliyotendwa na Mkapa katika kipindi chake cha miaka 10 ya utawala.

Nguvu ya CHADEMA hivi sasa, inafanana na ile kiliyokuwa nayo chama cha NCCR-Mageuzi katika kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni Temeke, Dar es Salaam, mwaka 1996.

Katika uchaguzi huo, rais na karibu viongozi wake wote wa ngazi ya juu, walikwenda Temeke kushiriki kampeni, lakini mgombea wa NCCR-Mageuzi, Augustine Mrema alishinda mikononi mwa Mabere Marando na wenzake.

Hoja za kupambana na Mkapa kwa ngazi ya Igunga na ngazi ya taifa ni nyingi. Pamoja na kuwa chini ya Rostam Azizi kwa karibu miaka 15, jimbo hilo ni kama maeneo mengine nchini ambako ufukara bado unatawala na hawana cha kujivunia.

Kinachoonekana ni kwamba, mara baada ya ufunguzi wa kampeni, na kama Mkapa atakuwa amekubali kwenda, viongozi wa CCM watakaobaki uwanjani Igunga, watakuwa wamebeba mzigo mkubwa wa kujibu tuhuma kuliko kunadi mgombea wao.

Mkapa anaweza kushambuliwa kwa tuhuma za kuuza nyumba za serikali kiasi kwamba kodi za wananchi sasa zinatumika kulipia mawaziri na viongozi wengine kukaa kwenye mahoteli, kwa miezi mingi. Baadhi ya mahoteli hayo yanadaiwa kuwa mali ya viongozi.

Mkapa aliidhinisha uuzaji huo kwa wafanyakazi wa serikali mithiri ya mtu aliyeshikiwa kiboko; upinzani umejiandaa kueleza wananchi, kwamba nyumba hizo zilizouzwa hazikaliwi na wafanyakazi hao.

Aidha, Mkapa atashambuliwa kwa hatua yake ya kuruhusu kukwapuliwa kwa mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), ndani ya Benki Kuu ya taifa (BoT).

Miongoni mwa fedha zilizoibwa, inadaiwa zilisaidia CCM kuingia madarakani katika uchaguzi mkuu wa 2005.

Taarifa za ndani ya Timu ya Rais zinaonyesha, Kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd., inadaiwa kumilikiwa na Rostam Aziz, ilichotewa mabilioni ya shilingi hata kabla haijasajiliwa kwa maagizo ya Mkapa.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, uhusiano kati ya Kagoda na BoT ulianza mapema 2005 lakini mtiririko wa mawasiliano na shinikizo la kulipwa vinaanza kuonekana kuanzia 10 Septemba 2005. Hiki ni kipindi ambacho Mkapa alikuwa Rais Mtendaji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kama hiyo haitoshi, upinzani waweza kumbebesha Mkapa tuhuma, kwamba ameshiriki katika ubinafishaji wa mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya, ambako serikali chini yake ilibinafsisha kwa watu binafsi kwa gharama ya kutupa, huku baadhi wakihusihwana watu kutoka ukoo wa rais mwenyewe.

Madai mengine, ni wizi wa mabilioni ya shilingi ndani ya BoT ukihusisha makampuni ya Tangold Limited, Deep Green Finance Company na benki ya Nedbank ya Afrika Kusini.

Kwa mfano, Mkapa alikubali ombi la Tangold na kununua “hati hewa” za dhamana kutoka BoT. Kwa mujibu wa nyaraka Na. 001/2005 ya BoT, Tangold Limited ilinunua na kupewa hati ya dhamana yenye thamani ya Sh. 25 bilioni, tarehe 1 Mei 2005.

Mkapa anajua kuwa hati hizi zilitolewa siku ya Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Dei) ambayo huwa ni siku ya mapumziko kwa ofisi zote za serikali, lakini hadi anaondoka madarakani hakuwahi kuchukua hatua.

Vilevile kwa taarifa Na. 002/2005 ya BoT, Tangold ilinunua na kupewa hati ya dhamana ya thamani ya Sh. 25 bilioni, tarehe hiyohiyo.

Kufuatana na masharti ya mkataba, Tangold ilipaswa kulipwa na serikali riba ya asilimia 10 kila mwaka, kwa mikataba yote miwili kwa kipindi cha miaka 10 hadi mwaka 2015. Hadi sasa, hakuna fedha iliyorejeshwa.

Hata huko Igunga ambako Mkapa anakwenda kufungua kampeni, wananchi wanamtuhumu kwa kushindwa kutekeleza ahadi aliyoitoa ya kukamilisha ujenzi wa daraja la Mbutu, lililopo mpakani mwa wilaya ya Meatu, mkoani Shinyanga na Igunga.

Mkapa anakwenda Igunga wakati pia kukiwa na madai ya kuwapo kwa mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho. Taarifa zilizopatikana juzi Jumatatu zinasema, Nape Nnauye, katibu wa Itikadi na Uenezi aliyeingia mjini humo kimyakimya akitoka Singida ametishia kumfukuza kazi, katibu wa CCM wilaya ya Igunga, Neema Adam.

Nape anaelezwa kutoa tishio la kumfukuza Neema katika mkutano wa ndani aliofanya Jumapili iliyopita. Amemtuhumu kuwa ndiyo chanzo cha CCM kufanya vibaya.

Katika mkutano huo, Nape aliahidi kulipa kila balozi wa shina wa CCM, kiasi cha Sh. 50,000. Jimbo la Igunga lina zaidi ya mabolozi wa shina 5,000.

Aidha, CCM kimepanga kutumia zaidi ya Sh. 35 milioni kulainisha baadhi ya waandishi wa habari na wahariri wa vyombo vya habari katika uchaguzi huo. Lengo ni kiweze “kupambwa vizuri” wakati wa uchaguzi huo.

Waraka ulioandaliwa na kitengo cha mawasiliano na umma, makao makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam unaonyesha, fedha hizo zitatumika “kuhonga” baadhi ya vyombo vya wa habari yakiwamo magazeti, televisheni na mitandao ya kijamii.

Magazeti ambayo CCM imepanga kuyatumia katika mradi huo, ni Mwananchi, Mtanzania, Nipashe, Jambo Leo, Majira na Habari Leo.

Kwa upande wa vituo vya televisheni, walenga wakuu ni waandishi na wahariri wa vituo vya vya ITV, televisheni ya taifa (TBC-1) na Channel Ten.

Waraka unasema, “…katika kuhakikisha CCM inashiriki vema katika uchaguzi huo…ni lazima kuwepo na ufuatiliaji wa habari katika vyombo vya habari moja kwa moja ili kujiridhisha na aina ya taarifa zinazoripotiwa. Lengo ni kuwa na waandishi watakaokuwa wakiwajibika moja kwa moja kwetu.”

Mwandishi wa waraka anasema katika kuhakikisha mkakati unafanikiwa, “Wahariri wahusishwe ili kuwepo uandishi wa makala na maoni ya wahariri yanayolenga masuala ya msingi badala ya kuzungumzia watu.”

Anasema, “Mpango huu unalenga kuhakikisha ni habari nzuri tu ambazo zinaandikwa na kusambazwa. Kitengo cha mawasiliano na umma kiko chini ya Nape.

Kwa mujibu wa waraka huo, idara hiyo imeomba kupatiwa gari moja litakalotumika kubebea waandishi wa habari watakaoratibiwa na CCM. Amependekeza gari hilo litoke katika wilaya zilizo karibu na Igunga.

Idara ya Nape imeorodhesha matumizi ya fedha hizo, ni Sh. 17,000 milioni kama posho ya waandishi wa habari; Sh. 13.7 milioni kampeni za njia ya mtandao (Online campaigning); Sh. 1.7 milioni malipo ya mawasiliano na Sh. 3.4 milioni kwa ajili ya matumizi mengine ambayo hayakutajwa.

“Kazi ya kuwashirikisha wananchi haiwezi kukamilika bila kuhakikisha wanatoka kwenda kupiga kura. Hivyo basi, wajumbe wa mashina pamoja na viongozi ambao walishiriki kuwaandaa wananchi katika kipindi cha kampeni wahakikishe kuwa wanawafuatilia na kuwakumbusha watoke waende kupiga kura na kuichagua CCM. Uzoefu wa uchaguzi uliopita umetuonesha kuwa katika hatua hii hatukufanya vizuri na hivyo kuwa moja kati ya sababu zilizosababisha watu wachache wajitokeze kupiga kura,” inasema sehemu ya waraka ambao MwanaHALISI inao.

Kiasi cha fedha – Sh. 35 milioni – ambazo Nape amepanga kuzitumia kulainisha waandishi, ni sawa na asilimia hamsini ya fedha zilizoruhusiwa na sheria ya uchaguzi.

Sheria mpya ya uchaguzi imetoa ruhusa ya kila chama kinachoshiriki uchaguzi wa Igunga, kutumia si zaidi ya Sh. 80 milioni.

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: