Mkapa anasimangwa kwa mafao haya


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 18 April 2012

Printer-friendly version

NILIPOANDIKA mwezi uliopita ubaya wa viongozi wakuu wastaafu wa aina ya Benjamin Mkapa, kufanya kampeni majukwaani kutetea chama tawala, na kupendekeza wafutiwe mafao, nilipata meseji kedekede, zikiashiria kuniunga mkono.

Hoja yangu ilikuwa kwamba kauli za rais mstaafu Mkapa jimboni Arumeru Mashariki wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo mwezi uliopita, zilimshusha hadhi, na alivyokuwa akiwaandama baadhi ya Watanzania wanaogharamia mafao yake.

Nikatoa mfano wa Zambia, walivyotunga sheria ya kubana viongozi wa aina hiyo, wanaolipwa pensheni nono kwa fedha za walipa kodi, lakini wakitumika kutetea maslahi ya kisiasa yanayonufaisha wachache.

Ujumbe huo pia uliwagusa wanasiasa wa upinzani. Sasa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kujua maana pana ya nilichokieleza, imeanza kueneza dhana hiyo kama sehemu ya mkakati wake kisiasa wakati huu wa mchakato wa katiba mpya.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, kwa nyakati tofauti, wamekaririwa wakizungumzia suala hili katika miji ya Arusha, Dar es Salaam na Dodoma.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Barafu mjini Dodoma wiki iliyopita, Mbowe alisema inasikitisha kuona serikali inatumia fedha nyingi za maendeleo kwa ajili ya kuwatunza watumishi wa ngazi ya juu walioitia hasara nchi.

“Wapo viongozi walitumia vibaya mali ya nchi lakini kutokana na kuwekewa kinga ya kutoshitakiwa bado wanaendelea kulipwa fedha nyingi pamoja na huduma mbalimbali kwa kutumia fedha za walipa kodi ambazo zingeweza kusaidia Watanzania katika masuala ya afya na elimu,” alisema Mbowe.

Mjadala huo umeibua kiu nyingine ya wasomaji kutaka kujua ni fedha kiasi gani za walipa kodi ambazo vigogo hao wanalipwa kwa mujibu wa sheria, lakini zinakwenda kunufaisha chama kimoja badala ya umma.

Sheria ya Mafao ya viongozi wa umma ya mwaka 1999 iliyorekebishwa mwaka 2005 ili kubainisha mafao hayo inasema Rais mstaafu anapomaliza kipindi chake cha uongozi, anaondoka ofisini na mafao ya mkupuo.

Mafao hayo yanakokotolewa kwa kuzingatia mshahara wa juu aliowahi kupata katika miezi aliyofanya kazi, kwa kutumia kanuni (percentage rate) itakayopangwa na mamlaka husika.

Kiwango cha mafao haya si rahisi kukitambua kwa kuwa kinaendana na mshahara wa rais ambao hapa Tanzania “ni siri kali”. Katika nchi nyingine mshahara huu unajulikana kwa kuwa rais ni mtumishi wa umma na analipwa kwa fedha za umma.

Kwa mfano, nchini Marekani, mshahara wa rais unajulikana tangu mwaka 1789 kiongozi wa nchi hiyo alipokuwa analipwa dola 25,000 kwa mwaka.

Tangu 2001 hadi sasa rais wa Marekani analipwa dola 400,000 (Sh. 640 milioni) kwa mwaka, sawa na Sh. 53.3 milioni kwa mwezi.

Wacha mshahara. Mbali na malipo ya mkupuo anayopata rais mstaafu, anapewa pasi ya kusafiria ya hadhi ya kidiplomasia yeye pamoja na mke/mume au wake/waume zake, na kulipiwa matibabu ndani na nje ya Tanzania.

Analipiwa matengenezo ya magari mawili yenye uzito usiopungua tani tatu, ambayo yanatolewa na serikali na kubadilishwa kila baada ya miaka mitano.

Kiongozi huyo anajengewa nyumba mpya (bila kujali kama aliuziwa ya serikali). Nyumba hiyo inatakiwa iwe ya angalau vyumba vinne, viwili kati yake vikiwa ni vyenye huduma zote muhimu (self contained).

Pia nyumba hiyo inakuwa na ofisi iliyokamilika na nyumba kwa ajili ya mfanyakazi.

Rais mstaafu analipwa posho ya kila mwezi ambayo ni sawa na Sh. 80 kwa kila 100 za mshahara wa rais aliyepo madarakani. Anapewa ulinzi unaostahili kwake na kwa familia yake.

Mafao mengine anayopata rais mstaafu ni msaidizi, katibu muhutasi, mhudumu wa ofisi, mpishi, mfuaji nguo, mtumishi wa ndani, mtunza bustani, madereva wawili, haki ya kutumia chumba cha watu mashuhuri (VIP Lounge) na gharama za mazishi atakapofariki.

Viongozi wengine wa juu – makamu wa rais, waziri mkuu, spika wa bunge, naibu spika, mawaziri na naibu mawaziri na mwanasheria mkuu – nao wana mafao si haba kuzingatia sheria hiyo.

Wabunge wana utaratibu wao mbali wa mafao. Hivi karibuni, serikali pia iliandaa utaratibu wa mafao kwa ajili ya majaji wastaafu.

Kanuni ya kulipa mafao ya makamu wa rais na waziri mkuu wastaafu, inaendana na ile ya rais, isipokuwa tu hawa hawajengewi nyumba, gari wanapata moja, na wanapewa fedha za kulipa mishahara ya watumishi, yaani msaidizi, mpishi, mfuaji nguo, mtumishi wa ndani, mtunza bustani na dereva kwa viwango vya kima cha chini cha mshahara.

Mafao ya viongozi hao baada ya kustaafu, yamewakinga pia wategemezi wao hasa wajane wa marehemu. Tarehe 24 Juni 2005, miezi mitano tu kabla ya kumaliza ngwe yake ya urais, Mkapa alitia saini Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali, ikiwamo ile ya mafao ya viongozi wa siasa ya mwaka 1999.

Marekebisho yaliyojumuishwa katika sheria hiyo ni kuongezwa kwa vifungu vya kuwalipa mafao wanawake wajane wa viongozi wakuu wa kitaifa, pale itakapotokea wamefariki dunia. Viongozi hao wastaafu ni rais, makamu wa rais na waziri mkuu.

Rais mstaafu akifariki dunia, mke au mumewe atapewa nyumba aliyopewa rais mstaafu, posho iliyo sawa na asilimia 40 ya mshahara wa rais aliye madarakani, matibabu ndani ya nchi, matengenezo ya gari linalotolewa na serikali, na baada ya miaka mitatu umiliki wake utahamishiwa kwa mjane mhusika.

Mjane huyo anapewa fedha za kulipa mishahara ya kima cha chini kwa dereva na mtumishi wa ndani, usafiri wa kwenda mahali atakapoishi maisha yake yaliyosalia, na mazishi yake kugharamiwa.

Pia mabadiliko yalilenga kuhakikisha kuwa kama kiongozi husika alishika uongozi wa kitaifa akiwa tayari analipwa pensheni (kwa ajira ya awali), basi malipo hayo yataendelea kulipwa, ikiwa ni nyongeza ya pensheni mpya atakayolipwa kwa uongozi wa kitaifa.

Malipo haya ndiyo yanawafanya wanasiasa wamuone rais mstaafu kama “mali ya taifa” kwa kuwa linamgharamia badala ya kugeuka na kuwa “mali ya chama” kilichomwingiza madarakani.

Vilevile utamu wa mafao haya, pamoja na mambo mengine ya kimamlaka, ndiyo kisa urais umekuwa unapiganiwa kwa gharama yoyote hata ikibidi kuua raia.

0788 346 175
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: