Mkapa ashukuru Mungu hakuwa Mara


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 11 April 2012

Printer-friendly version

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa kafanya kosa kubwa sana. Matusi ya reja reja aliyoyatoa Arumeru Mashariki angeyatamka popote pale mkoani Mara iwe Zanaki, Ikizu, Ikoma, Bunchari, Nyabasi, Nyamongo, Bukira, Bwiregi, Busweta au Ngoreme angesababisha balaa kubwa.

Mtu hawezi kutukana ukoo mkoani Mara na wanaukoo wakamwachia hivi hivi. Hapana haiwezekani, utapigwa kwa marungu na mapanga mpaka “nzi wakukatae” yaani hadi usitamanike.

Nasema hivi kwa sababu hakuna kosa kubwa kule kwetu mkoani Mara kama kumtukania mtu, na hiki ndicho alichokifanya Mkapa kwa kudai, Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere si ukoo wa Nyerere.

Tafsiri ya kauli hiyo ya Mkapa,  nadhani bila kufahamu, ni kwamba mama yake Vincent hakuwahi kuolewa katika ukoo wa Nyerere.

Kule kwetu mkoani Mara, mtoto ni wa bwana aliyetoa mahari na si vinginevyo. Kule Mara hawajali nani kazaa na nani kibayolojia au nani kamlea nani; wanachojali ni nani alitoa mahari na huyo ndiye mwenye mtoto. Mkapa alipaswa kulijua hili.

Akina Chacha, Mwita, Marwa, Wambura, Nyamhanga na Ryoba au Waryoba wakicheza ngoma ya iritungu au embegete au irirandi lazima kila mmoja ataje yeye ni nani, ndugu zake ni akina nani na ukoo wake ni upi bila kuhoji kama mzazi alikuwa hawara wa mama yake au la.

Kitu muhimu mkoani Mara ni kuoa na mtu ambaye ameshindwa kuoa ndiye pekee anayeitwa mjinga. Hata ungekuwa na stashahada au shahada ziwe za uzamili au uzamivu kama hujaoa wewe ni mjinga. Na kuna methali isemayo moteti atana mokangi ikamaanisha hakuna mtu aliyeoa ambaye ni mjinga.

Kwa ushahidi, kuna mwalimu mmoja wa chuo kikuu aliomba ubunge mara mbili akakataliwa kwa hoja kwamba ni mjinga. Mwalimu wa chuo kikuu aliitwa mjinga kwa sababu tu hajaoa.

Suala la kuoa mkoani Mara ni muhimu sana na mtu atafanya kila iwezekanavyo kuoa na suala la nani anamzalisha mwanamke huyo si hoja kabisa kwa sababu kitanda hakizai haramu.

Kwetu Mara, kila mtu anaoa, hata mtu aliyekufa tunamwolea mke, hata mtu aliyekosa watoto wa kiume tunamwolea mke na kuiita enyumba mboke au enyumba ntobu kwa maana kuwa nyumba inayoamshwa kwa kukosa mtoto wa kiume kuendeleza ukoo.

Kwa hiyo, kumwambia mtu wewe si ukoo fulani ni matusi. Mwanamke anayekaa na bwana bila kutolewa mahari tunamwita umsimbe au umwikarani, ni mwanamke asiyeheshimika na siku akiondoka huondoka na watoto wote aliozaa naye ukitaka watoto umuoe kwanza.

Kwa hiyo, Mkapa ana maana mamake Vincent Nyerere nu umsimbe au nu mwikarani? Mkapa ana bahati sana aliyasema maneno hayo, matusi hayo ya kirejareja akiwa mbali na wenyewe tena.

Mkapa alipaswa kujua kuwa mwanamume akizaa na mke wa mtu kutoka Mara siku akiondoka ataondoka na watoto wote na akirudi kwa mumewe kule Tarime, Serengeti, Bunda na Musoma Vijijini atapokelewa yeye na watoto uliomzalia na watoto hao hawatabaguliwa kwa sababu wamezaliwa ndani ya ndoa.

Nakumbuka kijana mmoja ambaye tulisoma naye lakini mamake alikuwa hajaolewa. Siku mama yake alipoolewa tukiwa darasa la nne na siku ile ile jina la kijana yule lilibadilika akapata ubini wa baba huyu mpya ambaye kamtolea mahari mama yake.

Kufika hapa sasa tuulizane maswali. Hivi Mkapa tangu lini kawa mtaalamu wa vizazi na vifo kujua nani alizaliwa ukoo fulani na nani si wa ukoo huo? Na je, ubini au ukoo wa Vincent Nyerere unahusikaje na matatizo ya wananchi wa Arumeru kama vile maji, shule, madawati na zahanati?

Niwaulize mameneja wa kampeni za chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – walitarajia kunufaika vipi na hoja ya uzao au ukoo au ubini wa Vincent Nyerere?

Na tangu lini Mkapa kasomea utaalamu wa vinasaba au DNA kiasi cha kufahamu ni nani wa uzao halisi katika ukoo wa Nyerere?

Arumeru wanakabiliwa na tatizo la maji yenye fluoride inayoozesha meno, hivyo walitarajia kampeni za CCM zijielekeze huko, namna watakavyopata maji safi na salama siyo nani kazaliwa na nani na nani si wa ukoo upi! Matatizo ya barabara, madawati, zahanati ndiyo muhimu kuzungumzia siyo uzao wa watu.

Na hili la Mkapa ni patigazeti tu bado gazeti lenyewe ni  Stephen Wassira, Waziri Ofisi ya Rais Sera na Uratibu, “Tyson” au Mzee wa Usingizi.

Tyson yeye kaleta mpya Arumeru. Eti alisema Katibu mkuu wa CHADEMA, Padri mstaafu Dk. Wilbroad Slaa aliwahi kuliibia Kanisa Katoliki!

Inaelekea CCM wana namna yao ya kufikiri kwa hili la Mkapa na ukoo wa Nyerere na Wasira na wizi wa pesa za kanisa kwenye kampeni za Arumeru. Sina uhakika Meya wa Jiji la Dar es Salaam Didas Masaburi ataiitaje aina hii ya kufikiri ya akina Mkapa na Wassira.

Hivi kweli Tyson anataka kutuambia Watanzania kuwa chama chao kinakerwa sana na wizi wa pesa za kanisa kuliko wizi wa pesa za umma?

Yaani mameneja wa kampeni za CCM kule Arumeru walituambia kwamba ni bora mtu akaliibia taifa pesa za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT), Richmond, Meremeta, Deep Green, machinjio ya Jiji Gongo la Mboto na kadhalika lakini si kuliibia Kanisa Katoliki!

Hata kama Kanisa Katoliki limekanusha kuwa liliwahi kuibiwa na padri Slaa bado tunayo haki ya kuwahoji CCM na mameneja wao wa kampeni kama walitaraji kunufaikaje na hoja ya wizi wa pesa za kanisa katika kampeni za ubunge wa Arumeru. Wizi wa pesa za kanisa unaongezaje kura?

Na bado katokea kijana mmoja kutoka jimbo la Mtera anaitwa Livingstone Lusinde, alimwaga matusi yasiyoandikika katika harakati za kusaka kura huko huko Arumeru.

Hili likanikumbusha jinsi huko nyuma CCM na serikali yake bila kusahau Msajili wa Vyama walivyokuwa wakikemea matusi. Lakini safari hii hata msajili hasikiki tena kuhoji matumizi ya matusi kwenye kampeni! Huu ni ushahidi tosha kuwa CCM imefilisika.

Tusubiri kampeni za Arusha tusikie makubwa zaidi ya haya.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: