Mkapa atishia serikali


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 30 June 2009

Printer-friendly version
Watetezi wake wajipanga upya
Watuhumiwa ufisadi wamo
Rais mstaafu Benjamin Mkapa

MPANGO wa kumtetea rais mstaafu Benjamin Mkapa umelenga mbali. Umeandaliwa mahsusi kubeba wote wanaolalamika kuwa Rais Jakaya Kikwete amewatelekekeza, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa za ndani ya serikali zinasema mpango wa kumsafisha Mkapa, uliozinduliwa bungeni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Ijumaa iliyopita, umelenga orodha ndefu.

“Ndugu yangu, Mkapa naye ana ndugu na marafiki. Lakini pia anajua mengi juu ya kila aliyeko madarakani sasa. Akiamua kubwatuka asubuhi moja, nchi inaweza kutikisika,” ameeleza.

Pinda alilieleza bunge kuwa Mkapa ni mcha Mungu, mwadilifu, siyo fisadi na hana fedha nje ya nchi, katika kile ambacho wafuatiliaji wamesema ni “kupoza hasira za Mkapa na kuogopa ulipizaji kisasi wakati ukiwadia.”

Alikuwa akijibu baadhi ya hoja za wabunge ambao wamekuwa wakisisitiza kuwa Mkapa ahojiwe na hata kufikishwa mahakamani kutokana na kukiuka maadili ya utawala bora.

Kilio kikubwa cha wabunge kimekuwa juu ya miliki ya mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya ambao inadaiwa kampuni ya Mkapa na familia yake, ilijibinafsishia tena kwa bei ya “bure.”

MwanaHALISI limeelezwa kuwa hatua ya Pinda ya kumtetea Mkapa hadharani imekuja baada ya kukwama kwa mpango wa awali wa kumfanya rais huyo wa zamani kuwa Kamanda wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), ambao wangepewa jukumu la kumlinda.

“Kwanza angetangazwa kuwa Kamanda wa Vijana. Akasimikwa na Rais Jakaya Kikwete, na kwa kofia hiyo, angejitokeza kwa nguvu zote na kuvunjilia mbali tuhuma zote huku akibebwa na vijana,” kimeeleza chanzo cha habari hizi.

Imefahamika kuwa kiongozi wa vijana ambaye angebeba bango la Mkapa angekuwa yule anayeheshimika kwa vijana wengi; mwenye hoja nzito na ambaye hatiliwi mashaka na wengi katika umoja huo.

Hata kama kijana wa aina hiyo angepatikana, na taarifa zinasema alikwishatonywa, tatizo jingine lingekuwa jinsi ya kushawishi vijana kuwa kamanda wao siyo tena Mzee Rashid Mfaume Kawawa, na bila sababu yoyote nzito.

Hata hivyo, kutopatikana kwa kijana mwenye uwezo wa kuunganisha wenzake kumbeba Mkapa, kulifanya hata pendekezo jingine kukwama.

Hili ni lile lililohusu makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Samwel Malecela. Kumekuwa na ushawishi wa chini kwa chini, tangu mwaka jana kwa kuhusisha baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu (CC) kumfanya kamanda wa vijana.

Mkakati wa ukamanda wa vijana umekuwa ukienda sambamba na kauli za wabunge za kumtetea Mkapa; na hivi karibuni Chrysant Mzindakaya (Kwale-CCM) alilazimika kunukuu maandiko matakatifu kumtetea.

Kwa hiyo kuibuka kwa Pinda na utetezi ambao haukutarajiwa, kumechukuliwa na wachunguzi wa siasa za sasa kuwa Mkapa bado ana nguvu “nyuma ya pazia.”

Taarifa zinasema kinachofanyika hivi sasa ni mshikamano miongoni mwa wote ambao wanalalamika kuwa wametupwa nje ya duara la madaraka tangu Rais Kikwete aingie madarakani.

“Sasa hakuna sababu ya kuangalia nani ametupwa nje na kwa sababu ipi. Kila mtu aweza kuwa na sababu zake. Hawa wakiungana wana uwezo mkubwa wa kurudi kwa kishindo hata kama ni kwa sanduku la kura,” ameeleza mmoja wa wabunge.

Miongoni mwa walio kwenye foleni na wenye shauku kubwa ya kurejea madarakani, ni aliyekuwa waziri mkuu Edward Lowassa.

Wengine ni waliokuwa mawaziri wa zamani wa nishati na madini, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha waliojiuzulu kufuatia kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond ambayo ndiyo pia ilimng’oa Lowassa.

Mbunge wa Bariadi Magharibi Andrew Chenge, Katibu Mkuu wa zamani wa CCM Philip Mangula, mweka hazina wa zamani wa CCM, Rostam Aziz, ni miongoni mwa wanaoweza kuungana na yeyote ili kuhakikisha hadhi yao inarejea.

Kauli ya waziri mkuu Pinda sasa itatumika kama wito wa kuunganisha wote wenye malalamiko kuwa serikali ya Rais Kikwete imeshindwa kuwalinda na kuwatetea na wote ambao kwa muda sasa wamevikwa tuhuma za ufisadi.

Wachunguzi wanasema kinachotendeka ni maandalizi ya kutafuta muwafaka kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: