Mkapa kikaangoni


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 12 May 2009

Printer-friendly version
Achota mabilioni NSSF
Ashindwa kuyarejesha
Rais mstaafu, Benjamin  Mkapa

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amemwanika rais mstaafu, Benjamin Mkapa kwa kuonyesha kuwa alitumia vibaya fedha za mkopo kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Kampuni ya Mkapa ilichukua mkopo wa Sh. 8.1 bilioni ili kuendeleza mradi wa mkaa wa mawe wa Kiwira mkoani Mbeya.

Lakini kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ya Januari mwaka huu, hakuna maendeleo yoyote yaliyofanywa kwenye mgodi huo wala mashine mpya zilizonunuliwa.

Huu ni mkopo wa pili kutolewa kwa kampuni ya Mkapa. Mkopo wa kwanza wa Sh. 17. 7 bilioni ulitoka CRDB Benki, kwa ajili ya kuendeleza mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira.

Mbunge wa Kyela, Dk. Harisson Mwakyembe (CCM) alimtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wakati wa kipindi cha maswali na majibu ya papohapo wiki mbili zilizopita iwapo serikali ingeweza kuwalipa wafanyakazi wa Kiwira ambao hawajapata mishara yao kwa miezi kumi sasa.

Katika ripoti yake ya 26 Machi, mwaka huu, CAG anasema mkopo huo wa muda mfupi uliotolewa kwa kampuni ya Mkapa, 5 Julai 2007  ulipaswa kulipwa ndani ya miezi sita, lakini hadi sasa hakuna hata senti moja iliyorejeshwa.

Kiasi kamili cha mkopo ambao Mkapa alichukua ni Sh. 8,127,000,000. Kiasi hiki kimekuwa kikiongezeka kwa njia ya riba na hadi 30 Juni mwaka jana kililimbikiza riba ya Sh. 840,450,000.

Hadi hapo kampuni ya Mkapa ilikuwa inadaiwa na NSSF jumla ya Sh. 8.9 bilioni. Ripoti ya CAG inasema riba pamoja na mkopo vilitakiwa kuanza kurejeshwa kwa mkopeshaji tangu Januari 2008, lakini MwanaHALISI limethibitisha kuwa hadi sasa hakuna marejesho yoyote yaliyofanyika.

Mkopo anaodaiwa Mkapa umedhamiwa kwa asilimia mia moja na serikali. Kwa mujibu wa kanuni za Benki Kuu (BoT), kawaida serikali haidhamini mtu binafsi.

Mkapa anahusishwa na umiliki wa mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira kupitia kampuni yake ya ANBEM anayosadikiwa kumiliki na mkewe, Anna, ikiwa miongoni mwa makampuni matano yaliyoingia ubia na kampuni ya TanPawer Resources Company Limited.

Pamoja na mikopo hiyo ya NSSF na CRDB, bado hakuna kilichofanyika katika kuurejeshea uhai mradi huu wa kufua umeme.

Ulipobinafsishwa, mradi wa Kiwira ulikuwa na uwezo wa kufua umeme wa megawati 200 za umeme kwa awamu mbili, ikiwa ni megawati 50 kufikia mwaka 2007 na megawati 150 kufikia Machi mwaka huu.

Lakini hivi sasa mgodi unazalisha megawati moja ambayo haiingizwi hata kwenye gridi ya taifa.

Kwa mujibu wa CAG, fedha ambazo NSSF imezitapanya kwa makampuni na watu mbalimbali, zinakaribia Sh. 50 bilioni, jambo ambalo linaweza kuuweka mfuko huo katika mazingira magumu katika siku za usoni.

 “Licha ya juhudi ya menejimenti ya NSSF kufuatilia urejeshwaji wa mikopo hiyo, kwa maoni yetu, baadhi ya mikopo na riba ulipwaji wake ni wa mashaka,” inasema ripoti ya CAG ya ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha wa 2007/08.

Iwapo mkopo kwa kampuni ya Mkapa hautarudishwa, na kwa kuwa alidhaminiwa na serikali, basi ni serikali itakayolazimika kulipa au kufuta deni.

Hata hivyo, CAG anasema hakuna nyaraka zozote zinazothibitisha kuwa serikali ilidhamini mkopo huo.

Mkataba wa mkopo huo ulitiwa saini 10 Julai 2007. Hata hivyo kuna udhaifu. CAG hakuona hati miliki ya mali iliyowekewa dhamana, jambo ambalo ni kinyume cha mwongozo wa NSSF juu ya vitegauchumi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: