Mkapa, Kingunge acha kulalama


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 19 October 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

NI msimu wa malalamiko. Kila mmoja ni mlalamishi. Rais Jakaya Kikwete analalamika. Mtangulizi wake, Benjamin Mkapa analalamika.

Waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba analalamika. Bernard Membe, waziri wa mambo ya nje analalamika. Hata Kingunge Ngombale-Mwiru analalamika.

Wanasema umoja wa nchi uko hatarini kutokana na migawanyiko kwa misingi ya udini na ukabila na kutokana na kusutana ndani ya  Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wanakiri kushindwa kwa viongozi wa umma kusimamia maadili ya taifa, kushindwa kusimamia mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi nchini, hivyo kuhatarisha umoja na mshikamano wa taifa.

Hata hivyo, hakuna hata mmoja miongoni mwao, anayekubali kuwa naye ni sehemu ya tatizo lililopo sasa. Hakuna anayekiri dhambi iliyotufikisha hapa; wala hakuna anayeelekeza njia ya kufuata baada ya iliyopo sasa kuonekana imeshindwa.

Badala yake, wanaishia kusema vijana “chukueni hatua.” Swali: Kipi kimewasibu viongozi hawa hadi kukubali kuwa watumwa, wakati ndani ya mioyo yao wanaamini kuwa waliopo madarakani wameshindwa?

Sababu ni moja. Kwamba hakuna hata mmoja miongoni mwa wanaolalamika, mwenye uwezo wa kujilinganisha na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere au mwenye uwezo wa “kuvaa kiatu chake.”

Tuanze na Benjamin Mkapa. Anasema watu wanatuhumu kwa hisia. Ni kweli hilo?

Mkapa hawezi kujinasua katika tuhuma na lawama za uuzaji wa nyumba za serikali. Wala Mkapa hawezi kusema haya ni majungu.

Wananchi wana macho na wanasikia. Mawaziri na watumishi wa serikali wanaishi kwenye mahoteli; serikali imeemewa na mzigo wa madeni unaotokana na pango la watumishi wake.

Mkapa hawezi pia kukana, kwamba naye amejichukulia moja ya nyumba zilizouzwa. Kama ilivyo kwa watumishi wengine, hawezi kusema anaishi katika nyumba aliyonunua. Anajua nasi tunajua, kwamba haishi katika nyumba aliyojiuzia.

Aidha, Mkapa hawezi kusema ni majungu kudai kulikuwa na ukwapuaji mkubwa wa mabilioni ya shilingi uliotokea ndani ya Benki Kuu ya taifa (BoT), wakati wa utawala wake.

Wananchi wameshuhudia wizi ukifanyika. Wameona nyaraka zilizotumiwa kuhalalisha wizi. Wameona kesi zimefunguliwa mahakamani. Wameona baadhi ya watuhumiwa, ingawa mapapa yenyewe hayajakamatwa.

Kwa haya ambayo yamefanyika, Mkapa hawezi kusema wananchi wanatuhumu kwa hisia.

Ni Mkapa ambaye, ama alipuuzia, alidharau au alinyamazia wizi wa mabilioni ya shilingi ndani ya BoT kupitia makampuni ya Deep Green Finance Company, Tangold Limited na benki ya Nedbank ya Afrika Kusini.

Wananchi wamemuona Mkapa akiwa Igunga “akimtakasa” Rostam Aziz kwa kusema ni “mchapakazi na mwadilifu.” Wakati anatenda yote haya, Mkapa anajua jinsi Rostam anavyohusishwa na wizi uliofanywa na kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd.

Vilevile, Mkapa hawezi kusema ni majungu kudai kuwa yeye aliingiza nchini kampuni ya iliyoshindwa kazi ya Net Group Solution na kuikabidhi kazi ya kuendesha TANESCO.

Je, ni majungu kusema kwamba katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa kampuni hiyo,  TANESCO iliishia kutumia mapato yake yote kuilipa Net Group badala ya kujiongezea uwezo wa kujiendesha?

Nyaraka za serikali zinaonyesha, kwamba ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Net Group, TANESCO ilishindwa kujipanua. Ilishindwa kujiendesha. Iliingizwa katika mgogoro mkubwa wa madeni.

Hata hili la giza na mikataba ya kinyonyaji ya sasa, chanzo chake ni utawala wa Mkapa kuingiza Net Group nchini kwa “mtutu wa bunduki.”

Mkapa hawezi kusema pia ni hisia, kwamba yeye akiwa ikulu alitenda kinyume na maadili ya urais. Aliongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kupitisha ubinafsishaji wa mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya.

Kwamba baada ya uamuzi wa ubinafishaji wa Kiwira kupitishwa, akamilikisha mgodi huo kwa kampuni waliokaribu na familia yake na aliyekuwa waziri wake wa Nishati na Madini, Daniel Yona.

Mkapa alichanganya mamlaka ya dola na ujasiriamali, kwa kuunda kampuni wakati akiwa madarakani. Akiwa ikulu alianzisha kampuni ya AN-BEN Limited. Kwa yote haya, Mkapa hawezi kusema ni hisia.

Wananchi wameona tangazo katika gazeti la Daly News, lililotolewa na Benjamin Mkapa na mkewe, Anne Mkapa likieleza adhima ya wanahisa wa kampuni hiyo kufungua kampuni yao. Mpaka sasa, Mkapa hajakana tangazo lile.

Je, hadi hapa Mkapa anapata wapi ujasiri wa kulalamika na kusema, “Wananchi wanatuhumu watu kwa hisia?

Hata Ngombale anayesema, “Tunataka chombo cha kuongoza, si suala la maneno, ila msimamo wa dhati na vitendo vyake,” hana hadhi ya kukemea wenzake.

Ni mmoja walioshiriki katika kuzika Azimio la Arusha, ambao ndiyo msingi wa uadilifu kwa viongozi wa umma.

Ndiye familia yake inatajwa kunufaika isivyo halali katika zabuni ya kukusanya ushuru wa maegesho ya magari jijini Dar es Salaam na mradi wa ushuru kwenye kituo kikuu cha mabasi ya mikoani, kilichopo Ubungo.

Akiwa mjumbe wa kamati ya mwafaka, baadhi ya wenzake ndani ya chama, wanamtuhumu kukwamisha miafaka mitatu kati ya chama chake na Chama cha Wananchi (CUF), Tanzania Zanzibar. 

Kukwama kwa mwafaka wa Zanzibar, ndiko kulikosababisha taifa kuingia katika mauaji ya watu zaidi ya 24, tarehe 26 na 27 Januari 2001.

Kukwama kwa mwafaka ndiko kulikoingiza taifa kwenye historia mpya ya taifa hili kuzalisha wakimbizi, badala ya kuwa kimbilio la wakimbizi.

Naye Warioba, ameishia kuwa mtu wa maneno, kuliko kuchukua hatua kubainisha malalamiko yake. Pamoja na kulalamikia umoja wa nchi kuwa hatarini kutokana na migawanyiko ya kidini na ukabila, hataji wanaosababisha uporomokaji huo.

Haelezi wanaochochea udini; wanaoleta siasa za makundi; wanaosababisha taifa kupoteza mwelekeo ulioasisiwa na Nyerere. Haelezi kuwa  ni serikali ya CCM na viongozi wake. Haijulikani kigugumizi cha Warioba kinatokana na nini.

Kwa upande wake, waziri Membe anasema, “Rais Kikwete anahujumiwa na watu aliowaamini na waliopata kuwa marafiki zake.”

Kama madai haya yana ukweli, basi Kikwete hana udhibiti. Anaogelea badala ya kusimama.

Inadaiwa kuwa wanaomhujumu ni viongozi waandamizi ndani ya chama, serikalini na bungeni. Je, kwa nini hawatajwi hadharani?

Tatizo linaloonekana kwa wengi, ni kwamba wote wanaolalamika wanaipenda CCM kuliko taifa. Wanataka kubebwa na chama. Hawana ujasiri wa kusema, “CCM siyo baba, siyo mama.”

Ni tofauti na Nyerere. Yeye alitanguliza maslahi ya taifa. Alisema “CCM si baba yangu.”

0
Your rating: None Average: 5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: