Mkapa kubali makosa uliyofanya


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 18 April 2012

Printer-friendly version

BENJAMIN Mkapa inabidi aanze kukubali makosa ya utawala wake. Akubali kuwa maamuzi mbalimbali aliyochukua yamechangia kulifikisha taifa letu hapa lilipo, hivyo asikae katika wingu la udanganyifu kuwa sera zake zilikuwa nzuri kwa taifa.

Akizungumza katika kongamano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, kati ya mengi aliyozungumzia Mkapa huku aking’aka, alisema kushindwa kwa sera ya ubinafsishaji kuokoa viwanda vyetu vilivyobinafsishwa (hata kama si vyote) siyo “tatizo” lake.

Alisema “kubinafsisha kulikuja ili kuhuisha uzalishaji! Sasa kama waliobinafsishiwa walikwenda kurudia utumbo ule ule uliokuwepo kabla hatujabinafsisha, hayo siyo matatizo yangu mimi (mguno na minong’ongono)…soko lilikuwepo, viwanda vilikuwepo menejiment ndio ilikuwa ovyo!” alisema Mkapa.

Anaamini kabisa kuwa suluhisho pekee la matatizo ya menejimenti lilikuwa kuuza viwanda vyetu vyote! Tukiangalia maneno hayo ya Mkapa na kumulika kwa karibu tunaweza kuona mambo kadhaa ambayo yamefichika na ambayo naamini wakati umefika kwa watu wenye nia na uwezo kuanza kuyaonesha wazi.

Baadhi ya mambo yalidokezwa vizuri sana na Mwalimu Nyerere katika hotuba yake maarufu ya Mei Mosi, 1995 kwenye uwanja Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya. Nataka nidokeze mambo kadhaa na niyapendekeze kuwa yanapaswa kuangaliwa tena katika mwanga wa kauli hizi za Mkapa.

Pendekezo la I - Ubinafishaji ulifanywa kuwaridhisha wakubwa wa kimataifa.

Wengi wetu tunakumbuka kuwa wakati vuguvugu la ubinafsishaji linapamba moto, kampeni kubwa ya kusamehe madeni kutoka kwa wafadhili ilikuwa pia inaendelea.

Wakati huo huo kulikuwa na mazungumzo na taasisi mbalimbali za kimataifa (hasa IMF, WB, Paris Club, na nchi moja moja) ya jinsi gani nchi maskini kama ya kwetu zingeweza kusamehewa madeni yake kuelekea Jubilii ya mwaka 2000.

Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi ambazo ilisemwa kuwa zilikuwa na “madeni yasiyolipika.” Kwamba hata kama tungeamua, kwa uwezo wetu wote kulipa madeni yale yote, uwezo wetu ungetuzuia kuyalipa kwani hatukuwa na uwezo. Tukawa kwenye lile kundi la “Highly Indebted Countries” yaani nchi zenye madeni makubwa.

Sasa, mojawapo na inaweza kusemwa kubwa katika mazungumzo yale ilikuwa kuipanga serikali na kuiondolea mizigo isiyo ya lazima na hasa kwa kuifanya iondoke kwenye kuendesha mashirika “yasiyo na faida”.

Hili lilikuwa moja ya masharti makubwa ya kukubaliwa kusamehewa madeni au kupata unafuu mwingine katika madeni.

Katika kufanya hivyo serikali yetu ilitakiwa kwa haraka kuja na mpango wa kuiondoa katika kuendesha kampuni na matokeo ya hili ni sera ya ubinafsishaji ambayo ni kinyume na utaifishaji.

Tulipofanya utaifishaji tulifanya baadhi ya vitu na njia za uchumi kuwa za taifa lakini tulipofanya ubinafsishaji tulirudisha vitu hivyo kwa watu binafsi.

Pendekezo la II: Ubinafsishaji ulielezwa kwa Watanzania kuwa ni jambo jema ambalo walipaswa kulikumbatia bila kukosoa.

Januari 2004 kulifanyika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ambacho kilitanguliwa na semina juu ya ubinafsishaji. Semina hiyo kwa kweli naweza kusema ndiyo lilikuwa jaribio kubwa la kufanya utetezi wa kiakili wa sera ya ubinafsishaji.

Aliyetoa mada iliyochochea mjadala alikuwa Dk. Abdallah Kigoda ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Ubinafishaji. Dk. Kigoda ndiye alifanya utetezi mkubwa wa sera ya CCM ya ubinafsishaji.

Ikumbukwe kuwa sera ya ubinafsishaji ilikuwa ya CCM kama ilivyosemwa katika semina ile kuwa “Ubinafsishaji ni mwelekeo na sera ya CCM, kinyume na dhana inayojaribu kujengwa na baadhi ya duru za kijamii kwamba eti ni sera binafsi ya Mheshimiwa Rais Mkapa” na kuwa “hoja kuu za ubinafsishaji ni nzito na hazipingiki kama zinavyoimarishwa na mafanikio yaliyokwishapatikana.”

Kwa hiyo, Watanzania walitakiwa kuamini na kukubali bila kuhoja sera hii kwa sababu hoja za uzuri wake “hazipingiki” na ni kweli wasomi wetu wengi, na wanasiasa wengi wa CCM waligeuka kuwa manabii wa ubinafsishaji wakituonesha “mafanikio” mengi yaliyokwishapatikana nchini.

Pendekezo la III: CCM iliahidi kuwa ubinafsishaji ni zaidi ya kuuza tu mashirika!

Katika semina hiyo ambayo naweza kusema yapaswa kupitiwa na wasomi wetu CCM haikuahidi tu kuuza mashirika.

Dk. Kigoda alisema, “Ubinafsishaji si suala tu la kuuza Mashirika ya Umma, bali ni mfumo unaojenga ushirikiano wa kudumu baina ya wawekezaji wa nje, serikali na wawekezaji wa ndani kwa nia ya kuongeza ufanisi, kuboresha utendaji, kupanua wigo wa ajira, kuongeza ubora wa bidhaa na kuyapatia mitaji na utaalamu mashirika yaliyobinafsishwa”.

Sasa, tukiyaangalia maneno ya Mkapa kwa mwanga wa haya maono ya Kigoda tunaweza kuona kuwa kwa Mkapa ubinafsihaji ilikuwa ni “kuuza mashirika ya umma tu”.

Kimsingi, kama tukikubali hoja ya Kigoda tulitakiwa kuona kuwa serikali pamoja na kuamua kuuza ikifanya (a). kuboresha utendaji (b). kupanua wigo wa ajira (c). kuongeza ubora wa bidhaa na (d). kuyapatia mitaji na utaalamu mashirika yaliyobinafishwa.

Hivi kweli, tunaweza kusema kuwa Mkapa chini yake alijitahidi kuleta utendaji bora? Au ndio haya anayoyasema leo kuwa “sasa kama waliobinafsishiwa walikwenda kurudia utumbo ule ule uliokuwepo kabla hatujabinafsisha hayo siyo matatizo yangu mimi?”

Yawezekana kuwa Mkapa alitaka kuuza tu mashirika ili aonekane amewatii wakubwa na kuonekana anatekeleza “sera ya CCM” lakini bila kujali matokeo ya sera hiyo. Leo anaruka matokeo ya sera hiyo?

Pendekezo la IV: Kama Serikali ilikuwa haitaki kuendesha mashirika ya umma kwa kuwapa ruzuku kwa nini vyama vya siasa vinaendeshwa na serikali kwa ruzuku?

Mojawapo ya hoja laghai ambayo iliuzwa sana ya kwa nini serikali iondokane na mashirika ya umma ni ile ya ruzuku. Dk. Kigoda alitudokeza kuwa serikali ilikuwa inatoa ruzuku ya karibu Sh. 100 bilioni na zaidi kwa mwaka kwa mashirika ya umma.

Akasema kuwa mashirika hayo bado yaliingizia serikali hasara ya kama Sh. 300 bilioni hivi. Na akasema kuwa kwa kuyabinafsisha baadhi ya mashirika kodi ilianza kulipwa nzuri zaidi na kwa ufanisi zaidi.

Pendekezo la V – Waliharakisha ubinafsishaji kwa sababu wenyewe walikuwa wanufaika wakuu.

Ningeweza kuliendeleza pendekezo hili mbele kidogo lakini itoshe kusema kuwa kina Mkapa na wenzake walipokuwa wanajitahidi kutuimbisha wimbo wa “ubinafsishaji halleluya!” walikuwa wanajua wanachokifanya. Leo hii wahusika wote wa sera hii na walioisimamia wao wenyewe au jamaa zao ndio walikuwa wanaufaika wakuu wa ubinafsishaji! Walijiuzia wenyewe makampuni yetu, wakawagawiwa jamaa zao, na ushahidi upo wazi kuwa sera hii ililenga hasa kunufaisha makundi fulani – cha kushangaza kwenye kundi hilo waliojaa ni wana CCM!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: