Mkapa kutinga kortini


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 27 April 2011

Printer-friendly version
Ni katika kesi ya Prof. Mahalu
Ikulu yahaha kumwokoa Kikwete
Rais mstaafu  Benjamin Mkapa

HATIMAYE rais mstaafu Benjamin William Mkapa atatinga mahakamani mjini Dar es Salaam.

Hili likitokea, itakuwa mara ya kwanza kwa rais au aliyewahi kuwa rais kuitwa mahakamani kutoa hati au ushahidi katika moja ya kesi za wanaotuhumiwa ufisadi.

Mkapa atatinga mahakamani kuhusiana na kesi inayomkabili aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu.

Prof. Mahalu anakabiliwa na mashitaka ya kufanya udanganyifu katika ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini humo. 

Kuingia kwa Mkapa katika hatua hii ya kesi, ingawa wachunguzi wanasema kumechelewa mno, kunalenga kumnusuru Mahalu ambaye amekuwa akiingia na kutoka mahakamani kwa karibu miaka minne sasa.

Katika hati ya kiapo ya 31 Machi 2011, chini ya sheria ya usajili wa nyaraka (The Registration of Documents Act, Cap. 117 R.E. 2002), Mkapa anaweka utetezi kuwa kila kilichofanywa na Mahalu kilikuwa halali.

Kwa hati ya kiapo ya Mkapa, akieleza jinsi kila kitu kilivyofanyika chini yake akiwa rais mtendaji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, upande wa mashitaka sharti ujiandae kuanza kukunja jamvi la mashitaka.

Mkapa anasema katika hati yake kuwa mchakato mzima wa ununuzi wa nyumba ya ubalozi, ulifuata “misingi ya sheria” na kwamba ununuzi “ulifanywa kwa maslahi ya taifa.”

Jengo ambalo Mahalu anatuhumiwa kufanya udanganyifu, liko katika Mtaa wa Vialle Cortina d’Ampezzo 185 mjini Roma.

Hati ya kiapo ya Mkapa, ambayo MwanaHALISI limeona katika ofisi ya serikali, inaanza kwa kusema, “Mimi Benjamin William Mkapa, mtu mzima, mkristu, mkazi wa Dar es Salaam, ninaapa hapa kama ifuatavyo:

“Kwamba, nilikuwa rais mtendaji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vipindi viwili mfululizo yaani kuanzia 1995 hadi 2005 na nina uhakika wa yote nitakayosema hapa chini.”

Mkapa anaanza kwa kusema kuwa jengo la ofisi ya ubalozi mjini Rome lilinunuliwa kipindi ambacho alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anasema, manunuzi ya jengo hilo yalikuwa kwa mujibu wa sera ya serikali ya kumiliki au kujenga ofisi za kudumu na makazi kwa mabalozi wetu nje ya Tanzania ikiwa njia ya kupunguza gharama.

Mkapa anaeleza katika kiapo chake, kwamba alijulishwa na watendaji serikalini jinsi mchakato ulivyofanyika na ripoti za uthamini za serikali zilivyotumika katika kufikia uamuzi wa kununua jengo hilo.

Tathimini ya jengo la ubalozi ambako Mahalu anatuhumiwa kufanya udanganyifu kwa kulipa fedha kinyume na ilivyotajwa katika mkataba, ilifanywa na serikali kupitia wizara mbili – Ujenzi na Ardhi na Maendeleo Mijini.

Katika hili, Mkapa anasema, tathimini zilitambuliwa na serikali kwa kiwango cha dola za Marekani milioni tatu tu – kwa mujibu wa tathmini ya wizara ya ujenzi na Euro milioni 5.5. kwa tathmini ya wizara ya Ardhi.

Anasema kupitia mchakato wa vyombo vya serikali, “…nilijulishwa vilivyo kwamba jengo la ubalozi lilinunuliwa kwa dola za Kimarekani milioni 3 wakati huo ikiwa ni sawa na Euro  3,098,741.40.”

“Kwamba kupitia mchakato wa mfumo wa serikali, nilijulishwa na hivyo kuidhinisha mchakato mzima na taratibu zilizotumika kununua jengo la ubalozi lililoko Vialle Cortina d’Ampezzo 185 Rome.”

Mkapa anaeleza katika kifungu cha nane cha kiapo chake, “Kupitia mchakato wa vyombo vya dola nilijulishwa kuwa balozi wa Tanzania, Rome alipewa mamlaka kamili kusimamia na kutekeleza mchakato mzima uliopelekea – kwa nguvu za kisheria alizopewa na serikali - hadi ununuzi wa jengo la ubalozi.”

Katika kifungu cha tisa cha hati ya kiapo, Mkapa anasema kwamba, mchakato ulioainishwa hapo juu, ulijumuisha kusainiwa kwa makubaliano ya aina mbili (moja rasmi/kawaida na moja ya kibiashara), kwa mujibu wa taratibu za Italia na kwamba hilo lilifanywa kwa uelewa na idhini ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Mkapa anasema utaratibu wa makubaliano ya aina mbili uliishawahi kufanywa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pale ilipoonekana muhimu kwa kuzingatia maslahi ya taifa.

Aidha, Mkapa anasema kuwa ni yeye aliyezindua jengo hilo la ubalozi tarehe 23 Februari 2003.

Kwa njia ya msisitizo, Mkapa anasema alikuwa anakumbuka na bado anakumbuka “…taarifa ya serikali iliyotolewa bungeni, tarehe 3 Agosti 2004 iliyosema na kuthibitisha kuwa taratibu zote zinazohusiana na manunuzi ya jengo kwa mujibu wa maelekezo ya serikali, zilifuatwa kikamilifu na kwamba muuzaji alilipwa kiasi chote.”

Akimzungumzia balozi Mahalu, Mkapa anasema, “Kwa kipindi chote nilichofanya kazi na balozi (Costa Mahalu) katika nyadhifa mbalimbali za utumishi wa umma, ameonyesha kuwa na tabia thabiti ya ukweli, uaminifu, unyenyekevu na uchapaji kazi.”

Amesema ni sifa hizo ambazo zilipelekea kutunukiwa tuzo ya heshima na rais wa Jamhuri ya Italia katika siku ya kumbukumbu ya taifa, siku nyingi baada ya kuondoka kwake nchini humo.

Kupatikana kwa hati ya kiapo ya Mkapa kumekuja mwezi mmoja tokea mawakili wa Prof. Mahalu wawasilishe ombi mahakamani kumkataa hakimu aliyekuwa anasikiliza shauri lake kwa madai kuwa hawana imani naye.

Kauli ya Mkapa kuhusu msimamo wa serikali inadhihirika katika kumbukumbu za bunge (hansard) za tarehe 3 Agosti 2004.

Katika kumbukumbu hizo, aliyekuwa waziri wa mambo ya nchi za nje, Jakaya Kikwete aliripoti katika Bunge la Jamhuri, ununuzi wa jengo la ubalozi mjini Rome na kueleza kuwa mchakato mzima ulifanyika kwa misingi ya uwazi na ulifuata taratibu zote zilizotakiwa.

“Mheshimiwa naibu spika, mwaka 2001/2002 wizara ilinunua jengo la ubalozi counsel katika ubalozi wa Rome katika jitihada za kuondokana na tatizo la kupanga majumba ya watu huko nje na pia kupunguza gharama za kuendelea kulipa pango la nyumba kila mwaka,” alieleza Kikwete.

“Ununuzi wa jengo hili ulifuata taratibu zote za manunuzi ya majengo ya serikali kwa kuzishirikisha wizara za ujenzi, ardhi na maendeleo ya makazi, pamoja na wizara ya fedha,” alisema.

Alisema, “Jengo lilifanyiwa tathimini na wataalamu wetu na kukubaliana na ununuzi wa Euro 3,098,781.40. Tarehe 6 Machi 2002, fedha za awamu ya kwanza katika ubalozi wa Rome zilipelekwa, nazo zilikuwa Sh. 700,000,000, tarehe 28 Juni 2002 zilipelekwa Sh. 120,000,000.

“Mwishoni mwa tarehe 26 Agosti 2002 zikapelekwa Sh. 1,000,000,000. Jumla ya fedha zilizokuwa zimepelekwa zikafikia Sh. 2, 900,000,000, na baada ya hapo ubalozi wetu ulitekeleza taratibu zote za ununuzi wa jengo na kumlipa mwenye nyumba kiasi hicho cha fedha.”

“Mheshimiwa naibu spika, kulitokea hoja ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa serikali, hoja 142.6.7 aliyehoji wizara kuwa alipofika ubalozi wetu Rome hakuona hati yeyote ya jengo hilo. Lakini napenda kueleza kuwa hati ya jengo hivi sasa iko ubalozini; nakala imeletwa wizarani kwa ajili ya hifadhi na pia mdhibiti mkuu amepelekewa nakala ya hati hiyo,” inarekodi hansard.

Nyumba iliyonunuliwa imo katika uwanja wenye ukubwa wa mita za mraba 1865, eneo la Via Cortina Ampezzo na Condomium of 110, Via della Mendola.

Kikwete aliwahi kuthibitisha kuwa jengo la ubalozi lilijengwa kwa mujibu wa taratibu zilizopitishwa na manispaa ya Jiji la Rome na kupewa hati Na. 258/AR.

Haijafahamika iwapo upande wa mashitaka utahitaji kuendelea na kesi hii baada ya hati ya Mkapa na kuibuliwa kwa taarifa ya Kikwete inayoonyesha kuwa kufunguliwa kwa kesi iliyopo mahakamani huenda kulifanyika haraka na bila ushauriano.

Naye Prof. Mahalu hakuweza kupatikana kwenye simu ya mkononi. Mwandishi alipokwenda nyumbani kwake aliambiwa kuwa “yuko Mwanza.”

Mwandishi hakuweza kumpata mwendesha mashitaka wa serikali kutokana na ofisi kuwa zimefungwa kwa sikukuu ya Pasaka na Muungano. Simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa.

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: