Mkapa: Mwanampotevu jeuri


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 03 June 2008

Printer-friendly version
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa

KWA Wakristo wanafahamu simulizi ya mwanampotevu aliyemdai baba yake urithi. Baada ya kupewa akaenda kula na makahaba hadi alipomaliza kila kitu na kuwa fukara wa kutupa.

Simulizi hizo zinasema maisha yalipoanza kuwa magumu alikata shauri na kurejea kwa baba yake kuomba msamaha. Kwa bahati nzuri alisamehewa na baba yake na kufanyiwa sherehe kubwa.

Inakumbusha kuwa kwa kawaida mkosaji ana tabia ya kwenda kwao kuomba radhi. Huo ni uungwana – kuangukia wa nyumbani kwako ili kusalimika.

Wiki mbili zilizopita, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alikwenda kijijini kwake Lupaso, mkoani Mtwara kukabidhi vifaa vya hospitali vilivyotolewa na wafadhili nchini Canada.

Ilikuwa ni shughuli ya kukabidhi vifaa, lakini kwa mshangao wa wengi, alitumia fursa hiyo kujisafisha dhidi ya tuhuma zinazomkabili za kukiuka maadili ya utumishi wa umma.

Tuhuma dhidi ya Mkapa zimekuwepo kwa zaidi ya mwaka sasa zikielekeza jinsi alivyotumia vibaya ofisi ya umma kujilimbikizia mali. Anatajwa kuwa alifanya biashara akiwa Ikulu; alikopa kwa jina la urais kutoka benki; alijimilikisha kampuni ya umma; alijipa tenda ya kuuziaTanesco umeme; na mambo mengine mengi yasiyokubalika kufanywa na rais aliyeko Ikulu akiishi na kula jasho la wananchi.

Mkapa, mzee kutoka Lupaso, mwingi wa majigambo na kiburi, tangu habari za matumizi mabaya ya ofisi yafichuliwe hadharani, aliapa kutofungua kinywa kusema lolote, lakini baada ya moto kuwaka zaidi, akaamua kwenda kufanya hivyo kijijini kwake.

Amesema habari zote hizo ni za uongo. Ameshauri wanakijiji wake kupuuza habari hizo na wachanechane magazeti yanayomwandika vibaya! Kwangu namfananisha Mkapa na mwanampotevu wa kwenye Bibilia.

Amerejea kwao kuomba radhi, lakini badala ya kukiri udhaifu wake, ameendelea kuonyesha kiburi na ubabe wake. Amesema habari za ukiukaji wa maadili ya utumishi wa umma dhidi yake ni uongo; kwamba ni uongo yeye ni mkwasi; kwamba kila kitu kilichosemwa dhidi yake ni uongo.

Amerudi kwao kweli, lakini amekwama kuomba radhi. Maana yake, amepoteza fursa nzuri ya kupata msamaha kama mwanampotevu wa kwenye Bibilia. Mkapa ama kiburi cha fedha au hisia za kulindwa na sheria vinamfanya ashindwe kukiri udhaifu wake kuwa yu mkosaji na anastahili kuungama.
Hataki kukiri udhaifu huo kwa sababu kwake ni kujishusha, lakini anasahau kitu kimoja: kadri siku zinavyokwenda, lile gome alilokuwa amejizungushia linazidi kumomonyoka na muda si mrefu atabakia mtupu. Mkapa anataka kusadikisha wale wa nyumani kwake kwamba yu msafi. Anataka wamuamini kuwa anapakaziwa na wale aliowanyima vyeo!

Anataka wasadiki kwamba anaonewa na wenye chuki binafsi; lakini Mkapa huyu hataki kuingia kwa undani juu ya tuhuma dhidi yake. Hataki kutaja tuhuma moja mnoja. Kwa mfano, hataki kusema kama kweli alianzisha kampuni ya ANBEM wakiimiliki yeye na mkewe wakiwa Ikulu; hataki kusema kama ni kweli au la kwamba alijimilikisha mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira yeye na aliyekuwa waziri wake wa Nishati na Madini, Daniel Yona.

Hataki kusema kama ni kweli au uongo kwamba walianzisha kampuni ya Tanpower Resources Limited na kujichukulia tenda ya kuuza gesi yote ya Songosongo; hataki pia kusema kama ni kweli au uongo kwamba alikopeshwa zaidi ya Sh. 750 milioni na Benki ya CRDB na NBC bila ya kuwa na dhamana yoyote! Mkapa hataki kutaja tuhuma moja baada ya nyingine!

Kwa nini hataki kutaja tuhuma hizi moja moja na anabaki kukimbilia kutoa majibu ya jumla jumla tena yaliyo dhaifu kabisa kijijini Lupaso? Sababu ni moja, bado anaamini mfumo wa usiri aliouasisi ambao ulifukia mawaa yote yaliyokuwa yakifanywa na awamu ya tatu aliyoiongoza, bado unafanya kazi.

Bado Mkapa yu katika ulevi wa kutisha watu kwa kuwafokea kila walipohoji kuhusu utendaji usiokuwa sawa wa watendaji wake. Mkapa anawaza ya awamu ya tatu. Kwa bahati mbaya anadhani awamu ya nne nayo itaingia kwenye uzembe wa awamu ya tatu wa kulea wezi na mafisadi waliokubuhu.

Mkapa anadhani kwamba alitoa ?kitu kidogo' kwa awamu ya nne kwa maana hiyo hatakumbwa na yanayotekea kwa akina Fredrick Chiluba wa Zambia na Bakili Muluzi wa Malawi. Mkapa anashindwa kusoma vizuri historia ya Malawi na Zambia.

Mkapa kwa sababu ya kiburi, anashindwa kuona kwamba hata Rais Levy Mwanawasa alibebwa na Chiluba kuingia madarakani; kwamba hata Muluzi (rafiki yake mkubwa) alimbeba Bingu wa Mutharika. Pamoja na marais hawa kubebwa na watangulizi wao, bado wameendelea kuwawashia moto mkali ambao unawababua.

Kwa hali hii, Mkapa anapaswa kujiuliza na kutafakari kwamba kinga yake si kwa sababu labda alimsaidia Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani Desemba 2005, ila kinga yake ni kwa kutenda mambo kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma. La muhimu zaidi, Mkapa anapaswa kuanza kutambua kwamba kati ya utawala wa awamu yake na sasa, kuna tofauti moja ya msingi.

Kwamba zote ni serikali za CCM si hoja, kwamba Kikwete alikuwa kwenye awamu yake si hoja, kwani hata Mwanawasa na Mutharika walikuwako kwa Chiluba na Muluzi! Tofauti iliyopo hapa ni kwamba Kikwete hayupo radhi kutetea uchafu wa wasaidizi wake.

Kikwete ameonyesha hivyo kwa kukubali baraza la mawaziri lisambaratishwe bungeni; amekubali kuona mawaziri wake wanatiwa adabu (Edward Lowassa; Nazir Karamagi; Dk. Ibrahim Msabaha na Andrew Chenge) amewaacha wahukumiwe na umma.

Mkapa hakuruhusu mambo haya. Alitetea mawaziri wake na kuwatukana wananchi walipohoji utendaji wao. Mkapa alijaa ubabe hata kupuuza taarifa za vyombo vya habari. Awamu ya nne inafanyia kazi kila taarifa inayotoka ikiigusa serikali yake.

Ni katika hali hii, watu wanashindwa kujua kwanini Mkapa anakuwa mwanampotevu mtukutu asiyependa kuomba radhi hata pale maji yanapokuwa yamemfika shingoni? Muda utaamua hatima yake.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: