Mkapa unavuna ulichopanda


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 02 December 2009

Printer-friendly version
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa

RAIS mstaaafu  Benjamin Mkapa anajifanya hamnazo. Anatuhumu na kushutumu wananchi na vyombo vya habari, kwamba anasakamwa bila makosa.

Mwanafalsafa wa kale wa China katika karne 6 kabla ya ujio wa Kristo, Confucius anasema, “Kuna vitu vitatu ambavyo haviwezi kufichika daima – jua, mwezi na ukweli.”

Si kweli kwamba Mkapa hakufanya mazuri. Kusema hivyo ni kutomtendea haki. Katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi (1995-2000) kuna mengi mema aliyafanya.

Aliweza kuongeza makusanyo ya kodi kutoka Sh 25 bilioni kwa mwezi hadi Sh 120 bilioni. Ni wachache wanaoweza kumlaumu Mkapa katika kipindi hiki. Hata katika suala la ufisadi katika kipindi cha kwanza cha utawala wake, Mkapa ananusurika.

Ni Mkapa aliyeunda Tume ya kuchunguza rushwa chini ya Jaji Joseph Warioba. Lakini mambo yalianza kumharibikia katika kipindi cha chake cha pili cha uongozi – 2000-2005. Ni mara baada ya baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kufariki dunia.

Hapo ndipo ufisadi wa hali ya juu ulifanyika – na haikubaliki kwamba Mkapa alikuwa hajui kile kilichokuwa kinaendendeka. Alijua.

Alijua kwamba uchotaji katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ulikuwapo. Ununuzi wa rada ya kijeshi isiyo na kichwa wala miguu, uchotaji wa Deep Green Financial Limited, Meremeta na Minara Pacha ya BoT, vilikuwapo.

Lakini kwa bahati mbaya yote haya Mkapa hayataji kila anapojaribu kujisafisha. Hili ni jambo la ajabu kwa kiongozi aliyesifika katika kufuatilia masuala kwa karibu, anakwepa kuzungumzia tuhuma hizi.

Hata siku moja Mkapa hajasikika kutaja neno “EPA,” “Kiwira” au “Minara Pacha” katika maelezo yake ya kutaka kujisafisha. Bali anajitapa kuwa aliendesha nchi kwa mafanikio na anazo sifa za uongozi.

Lakini kila mmoja anajua kuwa Mkapa alipoteza sifa za uadilifu. Na tukio moja la kukosa uadilifu kwa kiongozi wa nchi hufuta mema na mazuri yote aliyoyafanya na hutokomea kwa aibu kubwa.

Mwaka 1974 aliyekuwa Rais wa Marekani, Richard Nizon, alijiuzulu urais kutokana na kashfa ya Watergate baada ya kugundulika kutaka kuficha ukweli. Mema yote aliyotenda Nixon kama rais kwa miaka 9 yalifutika.

Mkapa analifahamu tukio hilo vyema kabisa. Lakini hakuna mfano mzuri kama ule wa kashfa iliyomkumba Helmut Kohl, aliyekuwa Chancellor (Waziri Mkuu) wa Ujerumani (kuanzia ile Ujerumani ya Magharibi) kwa miaka 17.

Alibwaga manyanga mwaka 1998 kwa aibu kubwa pamoja na mengi makubwa aliyoyafanya kwa nchi yake na Bara la Ulaya.

Ni yeye aliyeziunganisha Ujerumani mbili (ya Mashariki na ya Magharibi) mwishoni mwa miaka ya 1980 na hivyo yeye kuwa Chancellor wa kwanza ya Ujerumani iliyoungana upya.

Pili alihusika katika kuumarisha umoja wa nchi za Ulaya (EU) kuwa katika mfumo ulivyo sasa – hasa katika suala la sarafu ya pamoja (euro) iliyoanza kutumika rasmi mwaka 2001.

Kashfa iliyomkumba Kohl kuhusu michango ya fedha ya chama chake – pale alipopokea michango bila ya kutangaza kama  sheria inavyoagiza. Mazuri yote yalifutika. Kosa la Kohl ni dogo sana kulinganisha na Mkapa.

Bwana huyu ana “madudu” mengi. Akiwa Amiri Jeshi Mkuu, polisi waliwafyatulia risasi na kuwaua wafuasi 27 wa chama cha Wananchi (CUF), kisiwani Pemba 26 Januari 2001.

Mwaka 1996 mamia ya wachimbaji wadogo huko Bulyanhulu walifukiwa kwenye mashimo katika zoezi la kuwahamisha kupisha kampuni ya kigeni ya Barrick Gold kutoka Canada.  Yapo mengi mengineyo.

Kuna mauwaji ya wananchi katika msikiti wa Mwembechai, Magomeni, Dar es Salaam. Katika tukio hilo, polisi walipiga risasi raia wasiokuwa na hatia, kujeruhi na wengine kufariki dunia.

Haya yote wananchi bado wanayakumbuka na wanaendelea kuyaangalia kwa jicho pana. Inawezekana Mkapa amesahau. Lakini waliopoteza ndugu zao, wake zao na waume zao, bado wanakumbuka. 

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: