Mkataba TRL ungefutwa


editor's picture

Na editor - Imechapwa 21 January 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

HATIMAYE serikali imezinduka. Rais Jakaya Kikwete amesikia ingawa hakuweza kuchukua hatua iliyotarajiwa kuhusu uendeshaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).

Kwa karibu mwaka mmoja sasa, wafanyakazi wa TRL wameshitaki, kupitia vyombo vya habari, kwamba waendeshaji wa kampuni hiyo hawana uchungu na reli ya Tanzania.

Wameeleza kuwa kampuni ya RITES kutoka India inayoendesha kampuni inachota mishahara minono (kati ya Sh. 30 milioni na 50 milioni kwa mwezi kwa ofisa mmoja) huku ikikataa kulipa kima cha chini cha wafanyakazi cha Sh. 200,000.

Wafanyakazi wamelalamika kuwa mafundi wazuri wazalendo hawatumiwi. Wanafanyiwa vitimbi ili wakiona hawakupewa kazi, basi wajiuzulu.

Kuna masimulizi juu ya madreva wa treni ambao wamenyiwa kazi au wamewekwa benchi kwa nia ya kuwakatisha tamaa.

Kumekuwa na madai ya wafanyakazi kuwa baadhi ya injini za treni zilizokuwa zikitumika nchini miaka ya nyuma, zilipelekwa nje ya nchi kwa kile kilichoitwa matengenezo lakini hazikurudishwa.

Baadhi ya mafundi mahiri wa matengenezo ya treni kwenye karakana ya Morogoro, ambayo kwa miaka nendarudi wamekuwa wakihudumia treni na reli za Tanzania, wanaripotiwa kukatishwa tamaa.

Wafanyakazi wamedai, tena mara nyingi, kuwa baadhi ya vyuma kutoka karakana za reli vimeuzwa au kusafirishwa nje ya nchi kama skrepu.

Wametaarifu kwamba kuna mpango wa kung’oa reli katika maeneo kadhaa kwa madai kuwa reli katika maeneo hayo “hailipi.”

Sasa baada ya Rais Kikwete kuzungumzia TRL na kutoa maonyo, wafanyakazi wameelewa kuwa kilio chao kimefika mahali pake ingawa wahusika walichelewa sana kuchukua hatua.

Hata hivyo, kauli ya rais haijaleta uhakika wa mishahara kila mwezi. Haijaondoa kinachoitwa unyanyasaji wa mafundi na wataalam wengine ambao wanadai kukatishwa tamaa.

Kauli ya rais haijarejesha thamani na ubora wa karakana ya treni mjini Morogoro. Bado haijarekebisha pengo katika mapato kati ya menejimenti na wafanyakazi.

Hakika wafanyakazi waliposikia Rais Kikwete atajadili suala la menejimenti ya TRL, walitarajia atasema, “Sasa mkataba basi!” Bahati mbaya haikuwa hivyo.

Wafanyakazi walitarajia rais atamke kuwa “menejimenti ya reli inarudi mikononi mwa serikali.” Haikuwa hivyo.

Ni matumaini yetu kuwa haitachukua muda mrefu tena kwa serikali kuangalia kipi kinafanyika TRL na ikibidi, ifanye mabadiliko makubwa kwa manufaa ya taifa na si kwa wawekezwaji wa RITES.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: