Mkataba wa kuuza Kongo huu


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 11 February 2009

Printer-friendly version
Ni ule wa Laurent Kabila na Rwanda
Laurent Desire Kabila

KINACHOITWA vita vya sasa nchini Kongo ni utekelezaji wa “Makubaliano ya Lemera” ya mwaka 1996 yenye shabaha ya kuigawa nchi hiyo kubwa kuliko yoyote ile Afrika Mashariki na Kati.

Makubaliano yalifanywa kati ya Laurent Desire Kabila, akiwa kiongozi wa chama cha “kuikomboa Kongo” kutoka utawala wa dikteta Mobutu Sese Seko, kwa upande mmoja; na wapiganaji wa Kinyarwanda kutoka Rwanda na Mashariki mwa Kongo.

Makubaliano ambayo yalifanyika kwenye vilima vya Lemera vilivyoko Kivu ya Kusini na kujulikana kwa jina hilo, yalitaka Kabila, baada ya kuwa rais wa Kongo, aruhusu mikoa miwili ya Kivu Kaskazini na Kusini kuwa makazi ya Wanyarwanda wa kabila la Kitutsi.

Taarifa zilizopo zinaonyesha makubaliano yaliandaliwa mapema mjini Kigali na pale Lemera yalikuwa yanazinduliwa tu. Ilikubaliwa wakati huo kwamba hiyo ndiyo ingekuwa “asante” kwa Rwanda “kwa ukombozi wa Kongo.”

Desire Kabila alikuwa tayari amechoka. Kwa takriban miaka 20 alikuwa akipambana na utawala wa Mobutu Sese Seko. Alikuwa amefikia hatua ya kukata tamaa na kutulia jijini Dar es Salaam.

Mwaka 1996, mjini Kigali, Rwanda kilikuwa kimeundwa kikundi cha wapiganaji waliojiita “wapinzani wa dikiteta Mobutu.” Hawa walikuwa Wakongomani na Wanyarwanda kutoka Rwanda na wengine waliokuwa wakiishi mkoa wa Kivu Kusini, Mashariki mwa Kongo.

Katika kundi hilo alikuwemo Mkongomani, Jenerali Andre Kisasi Ngando; askari mtaalam wa kusomea. Anadaiwa kupata mafunzo nchini Cuba, Ujerumani na Bulgaria. Alikuwa akiongoza Wakongomani wapatao 600 katika kikundi hicho.

Wakati kikundi hicho kinataka kuanza vita, kilitaka kuwa na msemaji. Mungu akupe nini! Hakuna uthibitisho wowote, lakini taarifa zinaeleza kiliomba ushauri wa Mwalimu Julius Nyerere “ambaye aliwapa Laurent Desire Kabila kuwa msemaji wa wapiganaji.”

Mwanzoni mwa vita ya kumg’oa Mobutu kikundi hiki kilijulikana kama cha Wanyamulenge. Dunia nzima ikaambiwa na kuaminishwa kuwa hayo yalikuwa “maasi ya Wanyamulenge.”

Wanyamulenge ni watu wanaodaiwa kutoka kwenye vilima vya Mulenge vilivyoko wilaya ya Uvira katika mkoa wa Kivu Kusini. Makabila ya asili ya hapa ni Wavira na Wafuliro. Wanaojiita Wanyamulenge ni Wanyarwanda wakuja.

Vita vilianza kwa propaganda kuu kwamba serikali ya Mobutu haitambui Wanyamulenge ambao walidai ni raia wa Kongo; inawanyanyasa na inawanyima uraia. Haya yalikuwa madai makubwa sana yaliyovuta hisia kali na huruma kwa wapiganaji.

Wapinzani, chini ya Jenerali Andre Kisasi Ngando, na msemaji mkuu wao Laurent Kabila waliteka, kama mchezo, mji mkuu wa Kivu Kaskazini, Goma. Wakavuka Ziwa Kivu na kuingia Kivu Kusini.

Ilikuwa baada ya kukamata mji wa Bukavu, makao makuu ya Kivu Kusini na sehemu nyingi za mkoa huo, wapiganaji wa Kinyarwanda waliingiza pendekezo la rais ajaye wa Kongo, kutoa Kivu Kaskazini na Kusini kwa Rwanda.

Lakini kabla suala hilo nyeti kupewa uzito unaostahili, wapiganaji wa Kinyarwanda, baada ya kuteka Bukavu, wanadaiwa kuanza kupora mali – magari, vifaa vya nyumbani, dawa katika maduka – hatua ambayo ilielezwa kuwa uhamishaji wa mali za wakazi wa Bukavu na maeneo mengine.

Alikuwa Jenerali Ngando anayeripotiwa kupinga uporaji usiomithilika, jambo ambalo lilimletea uhasama kwa baadhi ya wapiganaji. Kuona hivyo, Laurent Kabila akamwasi Ngando.

Ngando anasemekana kuuawa siku chache baada ya kutofautiana na wapiganaji juu ya uporaji. Inaelezwa kuwa alimiminiwa risasi na kuuawa na mwili wake kuchomwa moto katika mbuga ya wanyama ya Virunga.

Kabila aliulizwa mara nyingi juu ya Ngando. Alikuwa na majibu tofauti. Akiwa bado msituni alisema Jenerali Ngando amekamatwa na majeshi ya serikali na mara ametekwa na wanamgambo wa Mai Mai.

Baadaye Kabila alisema Ngando alijeruhiwa na kupelekwa Ujerumani kwa matibabu. Na wakati akiwa rais, aliwaambia waandishi wa habari mjini Kinshasa kuwa Ngando alikuwa askari kama askari wengine na kwamba alikufa kwenye mapambano.

Ilikuwa baada ya kifo cha Jenerali Ngando ndipo Kabila aliingizwa kwenye makubaliano ya kumega Kongo. Kwanza, kikundi cha wapiganaji kiligeuzwa kuwa chama – AFDL – Alliance de front Democratique pour la Liberation du Congo. Kabila akapanda cheo na kuwa kiongozi wa chama cha ukombozi wa Kongo kutoka kuwa msemaji tu wa wapiganaji.

Baada ya kuundwa kwa AFDL, jina la Wanyamulenge likatoweka kabisa. Wapiganaji wakaitwa waasi wa Kongo. Taarifa zinasema kabla wapiganaji kutoka Bukavu na kuanza safari iliyomfikisha Kabila madarakani, waliingia katika mkataba ambao ndio umekuja kuitwa “Makubaliano ya Lemera.”

Kuna madai kwamba viongozi wakuu wa wakati huo wa baadhi ya nchi walipata nakala ya makubaliano hayo ya kumega Kongo. Miongoni mwa nchi hizo ni Namibia, Uganda, Burundi, Zambia, Ethiopia, Eritrea, Zimbabwe, Angola, Namibia, Sudan na baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani.

Imeelezwa kuwa makubaliano ni pamoja na kufanya mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini kutawaliwa na Wanyarwanda wa Kitutsi kutoka mataifa ya Rwanda, Burundi na Uganda; na kwamba utawala huo ambao ungefanya kazi kwa ushirikiano na serikali ya Kabila, ungetekelezwa kwa awamu tatu katika kipindi cha miaka 10 kuanzia 1998.

Chini ya mpango huo, raia wa Kongo, wakazi wa Kivu Kaskazini wangehamishiwa Kivu Kusini, “taratibu na kwa utulivu huku makazi yao yakichukuliwa” na wavamizi.

Imeelezwa kuwa hatua ya kwanza isingekuwa ngumu kwani Rwanda ingedai kuwa inapambana na wanamgambo wa Kihutu walioitwa Interhamwe ambao itaelezwa kuwa wanatishia amani nchini Rwanda. Hivyo ndivyo imekuwa ikifanya hadi sasa.

Makubaliano yanadaiwa kueleza kuwa kuchukuliwa kwa miji ya Goma na Butembo mkoani Kivu Kaskazini, sharti iwe hatua ya kwanza kwa kuwa hayo ndiyo maeneo yenye upinzani mkubwa. Kufanikiwa kwa awamu ya pili, kungetegemea mafanikio ya awamu ya kwanza, makubaliano yanadaiwa kueleza.

Wafuatiliaji wa mahusiano ya Rwanda na Kongo wanasema ingawa mpango huo ulishindikana kutekelezwa kuanzia mwaka 1998, kuingia kwa majeshi ya Rwanda nchini humo hivi sasa, ni utekelezaji wa hatua ya kwanza ya Makubaliano ya Lemera; na tayari miji ya Goma na Butembo iko chini ya kile kinachoitwa “majeshi ya ushirikiano” ya Rwanda na Kongo.

Kwa mujibu wa masimulizi juu ya makubaliano hayo, awamu ya pili ingekuwa kujaza wakazi wa Kaskazini katika Kivu Kusini na kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo wazawa wangeenguliwa, kukosa uongozi na hivyo kunyimwa sauti.

Hatua nyingine ilikuwa kuanzisha benki ya kusaidia wavamizi katika Kivu mbili, kujenga nyumba zipatazo 600,000 na kujiimarisha katika nchi ya kigeni – Kongo.

Imeelezwa kuwa Kabila alikubaliana na masharti ya makubaliano kwa kuwa lengo lake lilikuwa moja tu: Kuingia ikulu ya Kinshasa kwa msaada wowote kutoka kwa yeyote; Mungu au shetani.

Ilikuwa baada ya makubaliano hayo, Kabila alisonga mbele na hatimaye kushinda na kuingia ikulu ya Kinshasa akiwa na wapiganaji wa Rwanda, akiwemo mkuu wa sasa wa majeshi wa Rwanda, James Kabarebe.

Baada ya kuingia ikulu, Kabila anadaiwa kuwageuka wenzake. Ilikuwa baada ya miaka miwili ya urais, alitangaza, tena kwa jeuri, kuwa wageni wote waondoke nchini. Aliongeza kwa kufafanua, kwamba Wanyarwanda warudi kwao na kusema anawashukuru kwa kazi waliyofanya.

Kabila alikuwa tayari amesoma mwelekeo wa makubaliano yake na kuona kuwa yanatoa mwanya kwa kile kilichoitwa “Nchi ya Ahadi” ya Watutsi kutoka Rwanda, Burundi, Uganda, Somalia, Ethiopia, Eritrea na Tanzania.

Alitakiwa atangaze, akiwa rais, kuwa Kivu mbili zote ni makazi ya Watutsi; ili hata wananchi wa Kongo watakaobaki humo, wawe wanafahamu kwamba siyo kwao.

Kabila alinukuliwa akisema kuwa hayo (Makubaliano ya Lemera) ni “makubaliano ya porini” na kwamba yeye hakuwa na madaraka ya kuuza nchi. Alisema hakatai kuwepo mkataba, lakini akataka hilo “lipelekwe kwa wananchi – kupitia bungeni – ili wananchi wenyewe waamue.”

Kilichomshangaza zaidi Kabila, baada ya kutangaza kuwa Wanyarwanda warudi kwao, ni kwamba aliyekuwa wa kwanza kuondoka na kukimbilia Afrika Kusini, alikuwa waziri wake wa mambo ya nje aliyeitwa Bizima Karaha (Bizimana Karahamuheto).

Katika mshangao na labda kejeli, Kabila alisema, “Kumbe nchi ilikuwa imevamiwa! Hata waziri wangu wa mambo ya nje alikuwa Mnyarwanda?”

Hiyo ilifuatiwa na kufukuzwa kwa James Kabarebe aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Kongo na sasa mkuu wa majeshi ya Rwanda. Hatua hizi na nyingine, ndizo zilisababisha kutotekelezwa kwa Makubaliano ya Lemera.

Lakini wachunguzi na wafuatiliaji wa mahusiano ya nchi hizi mbili wanasema, makubaliano yameandikwa na yapo; hayajafutika. Kilichofanyika ni “ukaidi wa Kabila” wa kutotaka kutimiza ahadi yake baada ya kuingia ikulu.

Kabila anasemekana alikuwa amesoma kitabu cha Raphael Ntibazokiza kikieleza mahusiano ya Watutsi na wabantu, kiitwacho Plan de la colonisation tutsi au Kivu et region centrale de l’Afrique – Mpango wa ukoloni wa Kitusi katika Kivu na eneo la Afrika ya Kati.

Raphael anaandika, “Mhutu ameumbwa kufanyia kazi watu wengine; hawezi hata kujaribu kupata uongozi. Chukua nafasi zote za mikoa na wilaya na atakayekuwa mtawala ahakikishe kuwa analinda maslahi yetu... Baadaye watakapokuja kustuka, watakuwa wamechelewa…”

Mmoja wa waliokuwa karibu na Laurent Kabila amenukuliwa akisema hakuna kitu kilichomsononesha Kabila kama kauli ifuatayo ndani ya kitabu cha Raphael:

“Tutumie ukarimu wao. Tujinyenyekeze kwao kama sisi ni watumishi wao. Tukiishachukua nafasi zao tuwatelekeze na ‘kuwalipa ujira wa nyani’- payez-les en monnaie de singe pour montrer leur incapacite – ili kudhihirisha kuwa hawana uwezo.”

Kabila aliuawa kabla hajamaliza kunyukana na Rwanda. Aliuawa na mmoja wa “watoto” wake – vijana wadogo waliokuwa watu wa karibu sana na waliomlinda tangu akiwa msituni.

Kuna maelezo tatanishi juu ya kifo chake. Kuna wanaodai aliyemuua alitumwa na waliokuwa wakitaka atekeleze makubaliano ya Lemera; lakini wengine wanadai ni karata za nchi za Magharibi.

Kwa kuwa Jonas Savimbi aliuawa katika wiki moja tu baada ya kifo cha Kabila, inadaiwa kulikuwa na mkono wa mataifa makubwa; hili likitaka kuingia Kongo na hivyo kuomba msaada wa kuondoshwa kwa Kabila huku likiwezesha kukamatwa na kuuawa kwa Savimbi. Siasa hizi hazijafafanuliwa.

Kuingia kwa Joseph Kabila, anayedaiwa kuwa mtoto wa kufikia wa Laurent Kabila, kunaonekana kuleta mgeuko mwingine kuelekea kule ambako “baba” yake alikataa.

Kinachoitwa makubaliano kati ya serikali ya Rwanda na ile ya Kongo kinaonekana wazi kuwa utekelezaji wa mpango wa awali ambao Laurent Kabila alikataa.

Aidha, kukamatwa kwa Jenerali Laurent Nkundabatware na kuhifadhiwa nchini Rwanda kunaelezwa kuwa sura kamili ya “kuheshimu kazi ya maandalizi aliyokuwa akifanya nchini Kongo.”

Kuna madai kuwa Nkundabatware, Mnyarwanda kutoka Rwanda, lakini Rwanda inasema ni Mkongomani, hakuwa na jeshi lolote nchini Kongo. Aliongoza majeshi ya Rwanda hadi hapo ilipoonekana kuwa mazingira yamekuwa mazuri kwa Rwanda kuingilia kwa kisingizio cha “kufukuza Interhamwe na kuweka usalama mpakani.”

“Hata akipelekwa Kongo leo hii, Kabila atamlinda Jenerali Nkundabatware, labda kama wakuu wa Kongo na Rwanda watakuwa wamegundua kuwa amewasaliti,” kimeeleza chanzo cha habari hizi mjini Goma.

Rwanda imeingia Kongo. Nani ataiondoa? Baadhi ya nchi jirani zimekuwa watazamaji tu wakati nyingine zikiwa katika maandalizi ya kunufaika kutokana na mgogoro wa nchi hii.

Moses Byaruhanga, waziri katika ofisi ya rais (Siasa) nchini Uganda, amesema nchi yake inaunga mkono “shirikisho la Kivu na Kisangani” na kwamba wanasubiri kuona serikali ya Kinshasa inalionaje suala hilo.

Katika siku za karibuni kumekuwa na taarifa za kukamilisha kumegwa kwa mikoa miwili ya Kivu Kaskazini na Kusini kutoka Jamhuri ya Kongo na kuzifanya muungano wa Jamhuri ya Kivu.

Kauli ya msemaji wa ikulu Uganda inaongeza uwezekano wa kuimega Kongo pale inapohusisha jimbo jingine la Kisangani ambako majeshi ya Uganda yanadai kuwinda waasi wa Lord’s Resistance Army (LRA).

Kiongozi wa LRA, Joseph Kony amekuwa akipambana na majeshi ya serikali ya Yoweri Museveni kwa zaidi ya miaka 15. Uganda sasa inadai kuwa Kongo inatumika kama kichaka cha waasi hao.

Kauli ya Uganda haipishani na mipango inayodaiwa kufanywa na Rwanda ingawa Rwanda, kupitia balozi wake mjini Dar es Salaam ilikaririwa ikisema haina mpango wowote wa kuigawa Kongo.

Jumuiya ya kimataifa imetekwa kwa propaganda za Interhamwe, Wanyamulenge, waasi wa LRA na kumbukumbu za mauaji ya kimbari.

Isipokuwa Barrack Obama ambaye angalau amesema anataka Kongo tulivu na kwamba atasaidia kuleta hilo, mataifa mengine, pamoja na Ufaransa, yanataka kuimega Kongo.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)