Mkataba wa mabilioni LAPF wavunjwa


Editha Majura's picture

Na Editha Majura - Imechapwa 30 December 2009

Printer-friendly version

MKATABA wa Sh. 5,292,466,898 kati ya Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF) na Kampuni ya Uhandisi ya Derm Electrics (T) Limited umevunjwa, MwanaHALISI limebaini.

Taarifa zinasema kampuni hiyo ilikuwa iweke miundombinu ya umeme na viyoyozi kwenye jengo la kitega uchumi la LAPF, lililopo Makumbusho, Dar es Salaam.

Kampuni ya Derm Electrics ingelipwa Sh. 5,292,466,898 badala ya Sh. 4,992,466,898. Hiyo ni nyongeza ya Sh. 300 milioni kwenye fedha zilizokuwa zimetajwa kwenye tenda.

Mkataba huo ulisainiwa baada ya Derm Electrics kutangazwa kuwa mshindi wa zabuni hiyo ndogo, ambayo ilikuwa moja ya miradi saba midogo katika zabuni Na. PA/095/HQ/2008/09/W/24 iliyotangazwa Oktoba 2008 na kufunguliwa 20 Aprili 2009.

Kwa mujibu wa taarifa za uhakika, ni kampuni ya Cool Care Services Limited, iliyokuwa miongoni mwa washindani iliyolalamikia wa”washindi” ambao ni kampuni ya Derm Electrics (T) Limited.

Cool Care Services Limited ilifungua shauri la kupinga uamuzi wa LAPF kuipa kampuni ya Derm Electrics kazi ya kuweka mfumo wa viyoyozi kwenye jengo hilo. Shauri hilo liliwasilishwa Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA).

Hata hivyo, mamlaka hiyo haikushughulikia shauri hilo kwa kuwa zabuni ilishatolewa na mkataba kusainiwa kati ya mzabuni na LAPF.

Kwa mujibu wa Sheria Na. 21 ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004, zabuni ikishafikia hatua hiyo, chombo kinachostahili kisheria kusikiliza malalamiko ni Mamlaka ya Rufaa ya Manunuzi ya Umma (PPAA).

MwanaHALISI limeelezwa kuwa rufaa Na. 55 ya mwaka 2009 ilisajiliwa PPAA na Cool Care Services Limited dhidi ya LAPF.

Kampuni hiyo ililalamika kuwa Derm Electrics haikushiriki hatua ya awali ya zabuni husika na kwamba haikustahili kushiriki shindano la zabuni. LAPF ilikanusha madai hayo na kusisitiza kuwa Derm Electrics ilishiriki hatua zote za zabuni.

Wajumbe watatu wa PPAA, chini ya uenyekiti wa Jaji Mstaafu Augusta Bubeshi, baada ya kusikiliza pande zote mbili na kupitia kumbukumbu muhimu za hatua tofauti za ushindani wa zabuni hiyo, walijiridhisha kuwa Derm Electrics haikushiriki hatua ya awali.

Tarehe 27 Oktoba, mwaka huu, PPAA ilitoa uamuzi wa kubatilisha ushindi wa Derm Electrics (T) Limited na kuagiza LAPF iandae tangazo jipya la zabuni ndogo ya kuweka miundombinu ya umeme na viyoyozi na kuitangaza.

0
No votes yet