Mkataba wa umeme Serikali na Wachina utata


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 28 September 2011

Printer-friendly version

SERIKALI imejitumbukiza katika mtego mwingine kwa kusaini mkataba na Wachina unaolenga kuzalisha umeme kutokana na makaa ya mawe ya Mchuchuma na chuma cha Liganga, Ludewa, mkoani Iringa.

Mkataba huo uliosainiwa ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, 21 Septemba, mbele ya Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, unahusu miradi miwili ambayo serikali itamiliki hisa asilimia 20 kwa 80 za wawekezaji – Sichuan Hongda Corporation Ltd (SHCL).

Kulingana na makubaliano, miradi hiyo itatekelezwa kwa uwekezaji utakaogharimu karibu Sh. 5 bilioni (zaidi ya dola bilioni 3 za Marekani).

Sichuan ni ushirikiano wa China Africa Development Bank (CADB) na China Africa Development Fund (CADF). Imepewa kazi hiyo baada ya kushinda zabuni iliyokuwa na ushindani ikiwa imetangazwa mpaka vyombo vya habari vya kimataifa. Mchakato wa zabuni ulianza kwa waombaji 21.

Serikali imeingiza Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) ambalo litatekeleza miradi hiyo kupitia kampuni tanzu itakayoundwa ili kusimamia maslahi ya taifa wakati wa utekelezaji wa miradi.

Lakini, vyanzo vya taarifa, vinaonyesha wataalamu wenyeji walielekeza miradi hiyo itekelezwe kwa utaratibu wa serikali inayomiliki raslimali, kumiliki asilimia 50 ya hisa na itekelezwe kila mmoja kwa utaratibu wake.

Haijulikani hasa kile kilicholazimisha mawaziri kuridhia pendekezo jipya la kumiliki miradi hiyo kwa asilimia ndogo, hivyo kuleta manung’uniko kwamba serikali inaendekeza utamaduni mbaya wa kusabilia raslimali za taifa kwa wageni kiholela.

Nyaraka mbalimbali zinaonyesha kuwa ushawishi wa wazi wa kubadilisha mgawanyo wa umilikaji wa hisa katika miradi hiyo ulifanywa kupitia waraka uliowasilishwa Baraza la Mawaziri na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami mapema mwaka huu.

Katika moja ya maelezo kwenye waraka huo, vyanzo vya taarifa vimeiambia MwanaHALISI, serikali imeshauriwa kukubali kutengua uamuzi wake kuzingatia waraka Na. 14/2007.

Uamuzi huo ulikuwa ni kuelekeza miradi hiyo itekelezwe kila mmoja na mwekezaji wake badala yake serikali iridhie miradi kutekelezwa kwa mfumo unganishi.

Taarifa zaidi za mchakato zinaonyesha suala la mgawanyo wa hisa lilileta mvutano wakati wa majadiliano kati ya wawekezaji na timu ya wataalamu wa serikali.

Timu hiyo ilitaka mgawanyo wa hisa uwe wa sawa kwa sawa (50x50) na kiwango cha chini kabisa, ikibidi kupunguza, kiwe asilimia 25.

Wachina walitaka mgawanyo uwe asilimia 25 kiwango cha juu na kati ya asilimia tano na isiyozidi asilimia 20 bila ya kujali kiwango cha uwekezaji au wingi wa madini ya chuma yatakayobainishwa baadaye wakati wa utekelezaji wa mradi.

Katika utaratibu huo, ilichukuliwa kuwa hisa hizo zitatokana na raslimali ya makaa ya mawe na chuma ambapo kwa gharama zitakazohitajika kwa ajili ya utafiti, serikali/NDC hawatawajibika kuwekeza fedha taslimu kwa zile hisa watakazomiliki.

Wakati waziri anapendekeza mgao wa asilimia 20 kwa 80, anabainisha katika waraka wake kuwa NDC lenyewe lina uzoefu wa kutekeleza miradi kwa ubia na makampuni ya nje kwa mgawanyo wa mpaka asilimia 30.

Kwa mfano, katika mradi wa Kasi Mpya wa kuzalisha chuma ghafi, NDC inamiliki hisa asilimia 25 huku mwekezaji – kampuni ya Intra Energy ya Australia, akiwa na asilimia 75. NDC na Intra wameunda kampuni ya TANCOAL Energy Ltd kuendesha mradi wa Ngaka wilayani Mbinga, Ruvuma unaolenga kujenga mtambo wa kufua MW 400 za umeme kwa kutumia makaa ya mawe.

Nyaraka zinaonyesha serikali imekengeuka umuhimu wa kumiliki kiwango kizuri cha hisa katika miradi ya madini unaotajwa katika Sheria ya Madini Na. 14 ya 2010, kipengele cha 10.

Japokuwa inakiri kuzingatia wakati wote sharti la kufikiria maslahi ya taifa inaposaini mikataba, baraza la mawaziri lilisukumwa kuridhia mgawanyo huo wa 20 kwa 80.

Waraka wa baraza la mawaziri unathibitisha kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara ilitumia uzoefu wa kidunia kuwa anayemiliki raslimali, wastani wa umilikaji wa hisa kwa miradi mikubwa huwa ndani ya asilimia 10 zilizobadilika kutokana na kiwango cha uwekezaji.

Jambo hilo limekuwa likipigiwa kelele nyingi hata bungeni. Wabunge waliojadili makadirio ya bajeti ya wizara mbalimbali ikiwemo Viwanda na Biashara, Miundombinu, Ujenzi, Nishati na Madini na Maliasili na Utalii, walihimiza kuzingatiwa kwa maslahi ya umma katika kufikia mikataba na wawekezaji.

Waraka wa Waziri Dk. Chami unaonyesha alishawishi serikali ikubali mkataba usainiwe kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa na Wachina kwa kuhofia watajitoa.

Inaonyesha alitahadharisha kuwa Wachina wakijitoa, mpango mbadala utakuwa mgumu kwani una gharama kubwa na uwezekano wa kuchelewesha miradi kwa vile itabidi kuanzisha upya mchakato wa kutafuta wawekezaji wengine.

Wakati wa mjadala wa makadirio ya matumizi ya wizara hiyo bungeni Julai mwaka huu, kambi ya upinzani ilihimiza taratibu ziharakishwe za kuwezesha mkataba huo kusainiwa ili miradi hiyo ianze kutekelezwa kwa manufaa ya taifa. Walitaka serikali ihakikishe kiwango cha umilikaji wa hisa kwa NDC kinapanda baada ya mradi kulipa gharama.

Msisitizo huo ulikuwa unalenga kuondokana na mazoea ya serikali kuganda katika kiwango kile kilichomo katika mkataba.

Serikali imepanga kutumia kiasi cha Sh. 2 bilioni kwa ajili ya kutekeleza wajibu wake kimkataba ikiwemo kuimarisha miundombinu ya barabara ili kurahisisha upelekaji wa mitambo maeneo ya miradi.

Kwa mujibu wa majadiliano, umeme kutokana na makaa ya mawe unatarajiwa kupatikana Julai 2014 wakati ule utokanao na chuma ghafi cha Liganga utapatikana Juni 2015.

Wakati mkataba umeshasainiwa, kuna uthibitisho wa kisayansi wa kuwepo akiba ya karibu tani 500 milioni za makaa ya mawe katika eneo la ukubwa wa kilomita 140 za mraba. Utafiti wa NDC uliofanywa kati ya 1995/96 na 2009/10, umebaini mashapo yapatayo tani 125 milioni ambako makaa ya mawe yatapatikana.

Ni utafiti huo uliothibitisha kuwa uchimbaji wa makaa Mchuchuma utakuwa na faida kubwa kibiashara kabla ya hazina hiyo kwisha baada ya miaka 150 ya uchimbaji kuanza.

Hakuna utafiti wa karibuni uliofanywa katika chuma cha Liganga zaidi ya ule wa mwaka 1898 uliogundua madini yakiwemo chuma cha kawaida, Titanium na Vanadium (yanayotumika katika viwanda vikubwa) katika maeneo matano.

Maeneo hayo ni Mkelema-Magaga Matitu; Magaga-Luhaha; Mgendiguruime-Mwaselenga; Liganga na Ng’ongwa-Marere. Kuna akiba ya madini ya kiasi cha tani 1,227 milioni ambapo tani 45 milioni zimethibitishwa na utafiti uliofanywa na Colonial Development Corporation (CDC) mwaka 1957.

Nyaraka zinaonyesha kunahitajika utafiti wa kujua wingi na ubora hasa wa miamba iliyopo Liganga inayoaminika ina akiba kubwa ya madini ya chuma na mengineyo.

Hata hivyo, NDC walifanya utafiti wa kijiolojia mwaka 2009/10 na kugundua eneo lote la Liganga likiwemo la nje ya vitalu vitano vinavyojulikana, yapo mashapo ya chuma yapatayo tani 10 milioni yanayomilikiwa na NDC.

Zinahitajika dola 1,103 milioni (zaidi ya Sh. 1,200 bilioni) kuwekeza ili kuzalisha megawati 600 za umeme kutokana na makaa ya mawe. Kunahitajika kujenga mgodi, kituo cha kuzalisha umeme na njia ya kusafirisha umeme wa msongo mkubwa wa Kilovoti 220 kutoka Mchuchuma kwenda Liganga.

Umeme utakaopelekwa Liganga, kiasi cha MW300, utatumika kwa mradi wa uchenjuaji chuma unaohitaji uwekezaji wa dola 1.7 bilioni.

Sichuan, iliyokuwa kati ya makampuni 14 yaliyoshinda hatua ya awali ya maombi, imesifiwa na serikali kwa uwezo mkubwa wa menejimenti, fedha na teknolojia.

Zaidi ya mapato, taifa linatarajia kunufaika na nafasi 4,300 za ajira za kudumu na utaalamu kwa wazalendo.

0
No votes yet