Mke wa Zuma azua balaa Afrika Kusini


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 09 June 2010

Printer-friendly version
Nompumelelo Ntuli, mke wa Jacob Zuma

MAZONGE makubwa ya kifamilia yamemzonga Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini. Baada ya kuandamwa mara kwa mara na kashfa binafsi za ngono ambazo yeye ndiye aliyekuwa mtendaji, safari hii mambo yanaonekana kumgeukia mwanasiasa huyu mtata zaidi barani Afrika kwa sasa.

Hii ni baada ya vyombo vya habari vya nchi hiyo kuibua kashfa mbili kubwa za kimapenzi dhidi ya mkewe anayedaiwa kuwa kipenzi chake, Nompumelelo Ntuli maarufu kwa jina la MaNtuli.

First Lady huyo wa Afrika Kusini amekumbwa na kashfa kubwa mbili ndani ya mwezi mmoja. Moja ni kubainika kwamba alimdanganya Zuma kuwa hakuwa na mtoto wakati alikuwa naye na pili kugundulika kwake kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mmojawapo wa walinzi wa mumewe.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 35, anadaiwa kuwa na mtoto mwenye umri wa miaka 13 ambaye alimfanya siri wakati wa ndoa yake na kiongozi huyo.
Vyombo vya habari vya Afrika Kusini vimedai wiki hii kwamba mtoto huyo ni wa mwanamuziki maarufu wa nchi hiyo, Joe Mafela.

Hapa nchini, mwanamuziki huyo anafahamika zaidi kwa wimbo wake wa Cebeleza (Shebeleza) unaoonyeshwa sana katika luninga hapa nchini akiimba na watoto kwenye jukwaa kwa kuzungukazunguka (Mhariri).”

Magazeti ya Afrika Kusini, hususani Mail & Guardian, yameandika kwamba watoto wa Zuma ndiyo waliokuwa wa kwanza kubaini kuhusu hilo lakini hawakutaka kumwambia kuhusu hilo kwa kuhofia kumuumiza roho.
MaNtuli aliolewa rasmi na Zuma Januari mwaka 2008, lakini tayari alikuwa amezaa naye watoto wawili kufikia wakati huo.

Watoto hao ni Thandisiwe aliyezaliwa mwaka 2002 na Siqobile aliyezaliwa mwaka 2006, miaka miwili kabla ndoa hiyo haijafungwa rasmi kwa taratibu za kabila la Wazulu.

Vyanzo mbalimbali vya habari vimedai kwamba Mafela alikuwa akifahamika kwenye ukoo wa Zuma kama rafiki wa kawaida wa MaNtuli na alikuwa akiruhusiwa kumtembelea First Lady huyo walau mara moja kila baada ya miezi sita.

Mtoto huyo amekuwa akiishi na bibi wa upande wa mama yake na familia ya Zuma ilikuwa haijaambiwa chochote kuhusu mtoto huyo.

Magazeti hayo ya Afrika Kusini yaliandika kwamba kabla habari hizi hazijavuja kwenye vyombo vya habari, Zuma hakuwa akijua chochote kuhusu mtoto huyo.

Habari hizi mpya zimedaiwa kuichanganya familia ya Zuma kiasi kwamba kikao cha wanafamilia kiliitishwa nyumbani kwao Kwa Zulu Natal wiki iliyopita.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Nompumelelo alidaiwa kuzua kizaazaa ndani ya familia ya Zuma baada ya kubaini kwamba mumewe alikuwa mbioni kuongeza mke mwingine.

Mwanamama huyo alifanya fujo za kila aina kiasi kwamba alipewa adhabu ya kumlipa mumewe mbuzi mmoja kwa mujibu wa desturi za kabila lao la Wazulu.

Inadaiwa kwamba kabla ya kuoa mkewe wa tano, Thobeka Stacey-Madiba, mapema mwaka huu, yeye ndiye aliyekuwa kipenzi cha Zuma na alidhani pengine yeye ndiye angekuwa wa mwisho.

Mwezi uliopita, yaliibuka madai nchini Afrika Kusini kwamba kutokana na hasira aliyokuwa nayo, MaNtuli aliamua kuanza uhusiano wa kimapenzi na mmojawapo wa walinzi binafsi wa rais Zuma.

Mlinzi huyo, Pipha Thomo, inadaiwa aliamua kujiua mwezi uliopita baada ya kubaini kwamba uhusiano wake wa kimapenzi na MaNtuli umesababisha mama huyo apate ujauzito.

“Ni kweli MaNtuli alipata ujauzito kutokana na mahusiano yake na Thomo. Alifanya hivyo kama kulipa kisasi kwa mumewe. Ila mwenzake alipofahamu kuhusu mimba hiyo aliamua kujiua. Alijua angeleta aibu kubwa kwa Zuma,” kilisema chanzo kimoja cha habari.

Hakuna mtu aliyekuwa tayari, ndani na nje ya familia ya Zuma maarufu kwa jina la JZ, kuthibitisha kuhusu taarifa hizi za MaNtuli, huku msemaji wake binafsi akisema hawezi kuzungumzia mambo ya kifamilia ya bosi wake na vyombo vya habari.

Tayari Zuma amekwisha kufunga ndoa na wanawake watano katika maisha yake ya utu uzima na mmoja alifariki dunia kwa kujiua.

Wake zake Zuma ni Gertrude Sizakele Khumalo, aliyekutana naye mwaka 1959 lakini wakaja kuoana mwaka 1973 baada ya mwanaharakati huyo kumaliza kutumikia kifungo chake jela.

Wengine ni Nkosazana Dlamini-Zuma ambaye hata hivyo waliachana mwaka 1998. Mwanamama huyu amekuwa waziri katika serikali ya Afrika Kusini kuanzia mwaka 1999 hadi sasa. Amezaa naye watoto wanne.

Mwanamke wa tatu wa JZ ni Kate Mantsho, raia wa Msumbiji ambaye naye alizaa naye watoto watano. Mwanamke huyo alijiua Desemba nane mwaka 2000 kwa sababu ambazo bado hazijawekwa wazi.

Miezi michache iliyopita, Zuma alijikuta katika kashfa nzito baada ya kubainika kuzaa nje ya ndoa na mwanamke ambaye ni mtoto wa rafiki yake kipenzi.

Mwanamke huyo, Sonono Khoza, mwenye umri wa miaka 38, ni binti wa Irvin Khoza, mmoja wa matajiri wakubwa weusi nchini Afrika Kusini.

Mwaka juzi, Zuma pia alikutwa na kashfa nyingine mbaya ya kufanya ngono na mtoto wa rafiki wa familia yake ambaye ilithibitika alikuwa ameathirika na virusi vya Ukimwi.

Zuma, baada ya kashfa hiyo kubainika, alikiri kwamba alifahamu mwanamke huyo alikuwa ameathirika na Ukimwi lakini alikwenda kuoga mara baada ya tukio hilo ili kujikinga na virusi vya Ukimwi.

Hata hivyo, Zuma mwenyewe amepambana vikali na wote wanaomlaumu kwa kusema kwamba wazungu wamekuwa na kawaida ya kudhani mila zao ni bora zaidi kuliko za wengine.

0
No votes yet