Mkuchika "kanyea" kambi, atalala kwa nani?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 19 May 2009

Printer-friendly version
Gumzo
WAZIRI wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika

WAZIRI wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika, amekoromea waandishi wa habari wanaoripoti kuzomewa kwa vigogo wa chama chake.

Mkuchika yupo Busanda kunadi Lolensia Bukwimba wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayewania ubunge katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.

Uchaguzi wa Busanda unafanyika baada ya kifo cha Faustine Kabuzi Rwilomba aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo.

Rwilomba alikuwa mbunge wa Busanda kuanzia mwaka 2000 na alifariki miezi miwili iliyopita nchini India alikokwenda kwa ajili ya matibabu.

Akiongea na waandishi wa habari katika hoteli ya Zakaria mjini Katoro, Mkuchika alisema chama chake kinakubalika, lakini kinafitinishwa na waandishi wa habari kwa kuripoti matukio ya kuzomewa kwa viongozi wake.

Alisema, “Andikeni mnavyotaka, hata kwenye TV (Televisheni) onyesheni. Lakini mfahamu kwamba lazima CCM itashinda. Kwanza, watu wa Busanda hawaoni Televisheni kwa vile hata umeme hawana.”

Alihoji, “Kama watu wa hapa hawana umeme, sasa hizo TV zenu watazitazamia wapi?”

Hakuishia hapo. Aligeukia waandishi wa magazeti kwa kusema, “… Huku magazeti hayafiki na hata yakifika wananchi hawana uwezo wa kuyanunua. Sasa watasomea wapi hizo fitina zenu? Hayo mnayoandika yanabakia kuwa yenu na wamiliki wa vyombo vyenu.”

Mbali na kuwa waziri wa habari, Mkuchika ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Tanzania Bara.

Hatua ya Mkuchika kukoromea waandishi wa habari inathibitisha ukweli kwamba CCM imeemewa katika uchaguzi huo kwani si kawaida kwa chama hicho kukoromea waandishi katikati ya uchaguzi.

Ni kutokana na kuemewa huko, Mkuchika anataka kutumia uwaziri wake kutisha waandishi wa habari na vyombo vya habari. Anataka vyombo vya habari visiandike hata kile kinachoonekana kwa wengi au wote.

Anataka viandike na kutangaza kuwa mgombea wa CCM na wapigadebe wake wameshangiliwa, wakati wamezomewa. Kama si hivyo, kwa nini Mkuchika anatuhumu waandishi wakati kilichoandikwa ndicho kimetokea.

Ni muhimu Mkuchika afahamu kuwa kazi ya vyombo vya habari ni pamoja na kuripoti na kuibua, na mpaka sasa hakuna mashaka yoyote kwamba kazi hiyo imefanyika vema.

Bali mchawi mkubwa wa CCM siyo waandishi na vyombo vya habari. Ni hulka ya ukinyonga ya sura na tabia ya CCM kwa miaka nendarudi.

Uchaguzi wa Busanda unaelekea kudhihirisha upeo wa baadhi ya viongozi. CCM imeshindwa kuangalia mahali alipojikwaa, badala yake inalaumu pale ilipoangukia.

Kwa muda sasa, kuna madai kutoka kwa wananchi, kwamba CCM imesaliti wananchi na imekumbatia kundi fulani la watu wachache.

Serikali ya chama hiki imeamua kunyamazia kundi fulani la watuhumiwa wa ufisadi, hata kama baadhi yao tuhuma zao ziko wazi.

Bahati nzuri tabia hii ya CCM inafahamika hadi kwa wananchi Busanda, hata kama Mkuchika na wenzake wameamua kupora haki yao ya kikatiba na kimamlaka ya kupata na kutoa habari.

Wananchi wanawafahamu watendaji wa serikali, kwamba wanafanya kazi kiusanii. Ndiyo maana Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja anasema atapeleka umeme Busanda, mara baada ya bajeti ya serikali ya mwaka 2009/2010 kupitishwa na Bunge.

Lakini hasemi serikali ilikuwa wapi muda wote huo, hadi wasubiri mbunge afariki na uchaguzi mdogo ufanyike?

Ngeleja anasema wananchi wakichagua mgombea wa CCM watapata maendeleo. Anasema wizara yake italeta umeme Busanda hasa katika mji wa Katoro.

Ngeleja anaonekana tayari amesahau kwamba rais wa nchi hii ambaye amemteua yeye kuwa waziri wa nishati na madini, amekula kiapo cha kulinda na kutetea katiba.

Amesema ataongoza nchi hii kwa mujibu wa katiba. Kwamba atahudumia wananchi wote bila ubaguzi wa aina yoyote.

Wananchi wanamuona Ngeleja kama anaficha ukweli. Kwamba atapeleka umeme Busanda, wakati hata umeme uliopo sasa hautoshi kwa matumizi ya Dar es Salaam ambako kuna ofisi kuu ya nchi – Ikulu.

Ngeleja anasema atagawa maeneo ya machimbo kwa wachimbaji wadogo mapema mwezi Juni mwa huu. Uchaguzi wa Busanda unafanyika 24 Mei 2009.

Hapa ndipo wananchi wanapoiona serikali yao kuwa inaendeshwa “kisanii.” Kwani wananchi wanajiuliza: Inahitaji miaka mingapi kukamilisha kazi ya ugawaji wa maeneo hayo? Miaka kumi, ishirini, au thalathini? Kwa nini hilo halikufanyika kabla ya uchaguzi?

Kama kweli hilo linaweza kufanyika, kwa nini wachimbaji hao wamekuwa wanabughudhiwa na wale wanaoitwa wawekezaji?

Kwa nini wanaswagwa kama ng’ombe na kutupwa mahabusi wakati ardhi ni mali yao? Ngeleja alikuwa wapi muda wote huo? Hivi ni kweli alikuwa hajazaliwa?

Kutokana na hali hiyo, hoja ya Mkuchika kwamba “vyombo vya habari vinafitinisha wananchi,” hapa haina mashiko.

Ni CCM inayojifitisha yenyewe kutokana na hulka na tabia yake sugu ya kukumbatia ufisadi na kulinda baadhi ya watuhumiwa.

Pili, Mkuchika ameanza kuona hatari inayokikabili chama chake; hatari ya CCM kuanza kupoteza mwelekeo. Zile porojo za miaka nenda rudi, kwamba “CCM kinapendwa na kukubalika,” sasa zimeanza kutoweka.

Hata kama chama hiki kitashinda uchaguzi wa Busanda, bado hakiwezi kujitapa kuwa hatua yake ya kukumbatia watuhumiwa wa ufisadi haijakiathiri.

Busanda imeongozwa na mbunge wa katika chaguzi zote tatu zilizopita baada ya mfumo wa vyama vingi kurejeshwa. Wakati huo hakukuwa na upinzani. Leo upo upinzani, tena wa uhakika. Tusubiri.

Bali Mkuchika ameshindwa kuelewa nafasi yake katika Tanzania na Busanda. Ilitarajiwa akiri udhaifu wa serikali ya chama chake ya kushindwa kupeleka umeme Busanda badala ya kurukia waandishi wa habari.

Akiri kuwa CCM imekamua wananchi si Busanda pekee, bali nchi mzima. Ni sera na mipango mibovu ya CCM inayosababisha wananchi kushindwa kumudu kupata hata mlo mmoja kwa siku, achilia mbali kuweza kununua gazeti.

Kushindwa kuyaweka haya bayana, hakuwezi kusaidia CCM. Kunaweza kusaidia kuahirisha tatizo. Inawezekana hivyo ndivyo Mkuchika na wenzake wanavyotaka.

Wananchi wa Busanda wanajua nani kawaweka katika mazingira haya hata hawawezi kumiliki TV? Nani kawafikisha hapa hadi wanashindwa kuwa na umeme wala kusoma magazeti?

Nani amewaweka wananchi katika mazingira haya yanayoweza kufananishwa na yale ya wafungwa wasioweza kufurukuta?

Waziri mwenye kusimamia wizara ya habari, kazi yake ni ipi hasa? Ni kufungia magazeti tu, au kuhakikisha kuwa kila raia anafurahia haki yake ya kupata na kutoa habari?

Waandishi wananukuu matukio. Waziri asiwazuie kufanya hivyo, tena kwa rekodi sahihi kwa walioko sasa na wajao. Ni ukweli mtupu utakaojenga taifa la watu wanaofikiri na kutenda kwa uhuru.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: