Mkullo na makengeza ya fikra


Isaac Kimweri's picture

Na Isaac Kimweri - Imechapwa 01 April 2008

Printer-friendly version
Waziri wa Fedha  Mustafa Mkullo

KAULI ya Waziri wa Fedha Mustafa Mkullo, kwamba eti nchi wahisani wanawasilikiliza sana wapinzani kwa sababu wanao marafiki wao wanaowaambia mambo mengi ya humu nchini, ni kauli ya kushangaza.

Mkullo alikuwa akizungumiza uamuzi wa nchi wafadhili kukataa kuthibitisha iwapo watasaidia bajeti ya mwaka 2008/09 ikitaka kwanza mafisadi wote wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na kashfa ya Richmond wachukuliwe hatua za kisheria.

Alisema serikali imefikia mahali pazuri katika mazungumzo yake na wafadhili hasa kutokana na hatua ilizokwisha chukua dhidi ya mafisadi wa EPA na kashfa ya Richmond, na kwamba huenda wakachangia kiasi kinachohitajika katika bajeti.

Serikali inataka wafadhili wachangia zaidi ya Sh. 970 bilioni katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2008/2009.

Ingawa Mkullo anaonyesha kuwa mambo yanakwenda vizuri sasa baina ya serikali na wafadhili ikiwa ni zaidi ya miezi mitatu kupita bila wafadhili kueleza bayana kama wanagefadhili bajeti hiyo au la, kuna hisia kwamba wafadhili wanawasikiliza wapinzani na kuweka masharti ya kutoa fedha zao.

Anaonyesha kwamba wahisani wana mahusiano mazuri na wapinzani kiasi cha kuwaamini na kuwasikiliza.

Kwa maneno mengine, Mkullo anakili kwamba hali hiyo huipa serikali wakati mgumu kutokana na wahisani kuweka masharti ya kusaidia bajeti kwa kufuata taarifa wanazopewa na wapinzani.

Kwa tathmini ya haraka, Mkullo anayeisemea serikali anadhani kwamba kama si wapinzani basi wafadhili wasingepata taarifa za ufisadi wa EPA na kwa maana hiyo kusingekuwa na masharti katika utoaji wa fedha hizo.

Kwamba wapinzani wamesababisha serikali kuhangaishwa na wafadhili kiasi cha kuishurutisha kufanya mengi.

Moja, kuchunguza kashfa ya Richmond na kushinikiza hatua kali kuchukuliwa dhidi ya wote waliohusika.

Pili, kuchunguza ufisadi wa EPA, pamoja na kung'ang'ana kwamba wahusika wote waliotafuna mabilioni hayo ya shilingi wanaswagwa mahakamani.

Wafadhili na hata wapinzani hawakubaliani na hoja ya serikali ya kurudisha fedha hizo, huku watuhumiwa wakiendelea kukata mitaa. Wanataka fedha zirudi na watuhumiwa wapelekwe mahakamani.

Tatu serikali sasa imeshikwa kooni na wahisani na wananchi kwa jumla wakitaka wote waliohusika na EPA wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria. Haya yote ni sababu ya ukaribu wa wapinzani na wahisani!

Mkullo ni Waziri wa Fedha. Hii ni nafasi kubwa sana katika nchi. Kwa wenzetu waliopiga hatua za kimaendeleo kama Uingereza, waziri wa fedha ni kiongozi namba mbili kwa madaraka.

Wakati wa utawala wa Waziri Mkuu, Tony Blair, hakukuwa na sababu ya kujiuliza hivi mtu wa pili katika madaraka ya serikali ya nchi hiyo ni nani? Mara moja jibu lilipatikana kuwa ni, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Gordon Brown ambaye sasa ndiye waziri mkuu kwa sasa.

Kwa maana hiyo, wizara ya fedha katika mataifa mengi ni nyeti. Waziri wa fedha ni waziri wa ngazi za juu kabisa katika ngazi ya mawaziri.

Unyeti wa wizara ya fedha ndio unatoa changamoto kwa mtu anayekabidhiwa wizara hiyo awe ni kiongozi aliyepevuka vilivyo.

Wizara ya fedha hapewi waziri anayejifunza kazi kwa sababu ni rahisi sana kudondosha uchumi wa nchi kwa maamuzi ya ovyo.

Kati ya mwaka 1990 na 1994 taifa hili lilikuwa na waziri wa fedha wa ovyo mno kiasi cha nchi kukosa heshima kabisa mbele ya wafadhili kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Serikali ya wakati huo, si tu kwamba haikusimamia sera za fedha za nchi, bali haikuwa na ubavu hata wa hata wa kukusanya kodi.

Hatimaye wafadhili walisimamisha misaada kwa sababu ya uzembe wa dhahiri wa kushindwa hata kukusanya kile kidogo kilichokuwako.

Hiki ndicho kipindi ambacho wafanyabiashara walitawala nchi kwa kupewa misamaha ya kodi na wengine hata kukiuka sheria kwa kukataa/kukwepa kulipa kodi.

Kwa hiyo Mkullo kusema kwamba eti wafadhili wanawasikiliza sana wapinzani kwa sababu wana marafiki wao huko wanaowapa habari, anataka kuwaeleza Watanzania kwamba kama si wapinzani habari ya EPA na Richmond zisingefika hapo zilipo leo.

Kwamba kama si wapinzani wahisani wasingeibana serikali kuhusu EPA na Richmond kama inavyofanya sasa; kama si wapinzani serikali isingekuwa na wakati mgumu kama ilivyo kwa sasa mbele ya wahisani.

Kauli hii kwa hakika naweza kusema imetoka kwa bahati mbaya kwa kiongozi wa ngazi ya Mkullo. Kwamba kwake kinachomsumbua ni jinsi wahisani walivyojua habari ya EPA na Richmond au si jinsi EPA na Richmond ilivyoaibisha taifa hili kufika ngazi ya juu kabisa ya mataifa yanayokumbatia ufisadi.

Mkullo hasumbuki na jinsi rasilimali za nchi zinavyotokomea, jambo ambalo limesababisha kwa kiwango kikubwa serikali kuwa tegemezi na ombaomba. Kwemwe Mkullo hilo halimsumbui.

Ni dhahiri kauli ya Mkullo inazidi kuthibitisha hisia ambazo zimekuwako kwa muda sasa, kwamba serikali haikuwa radhi kushughulikia suala la EPA hasa kutokana na wahusika wakuu kuwa sehemu ya watawala walioko sasa na wa serikali ya awamu iliyopita.

Kwa Mkullo na watawala wa awamu ya nne kwa ujumla, EPA imefika hapo kwa sababu ya kelele za wapinzani na mahusiano yao na wahisani. Ndiyo maana serikali inajikuta katika wakati mgumu wa kuwashughulikia mafisadi.

Nilidhani serikali inayoongozwa kwa miiko ya utumishi wa umma, iliyoapa kukabiliana na rushwa kwa nguvu zake zote, iliyochaguliwa kwa kura za kishindo ingekuwa na kila sababu ya kufurahia harakati zinazofanyika za kuwashughulikia mafisadi. Kwa bahati mbaya serikali badala ya kuwashughulikia inatafuta njia za kuwatakasa.

'Mguno' wa Mkullo na jinsi serikali inavyolinda mafisadi pamoja na hatua ya serikali ya kujadiliana nao, ni kielelezo tosha cha kukosekana kwa utayari wa kuwakabili watu hawa walioangamiza uchumi wa taifa hili kwa sababu ya mahusiano yao na watawala.

Kauli ya Mkullo inaongeza aibu juu ya aibu kwamba serikali inashughulikia mafisadi wa EPA kwa sababu tu wahisani wameonyesha kutokufurahishwa na wizi uliofanya.

Ni aibu zaidi kwamba serikali inajitahidi kufunika mafisadi wasijulikane kwa kuwa inajua wapo viongozi serikalini watakaoumbuka kutokana na kunufaika na wizi huo.

Hata hivyo, wakati sasa umewadiwa kwa watu kama Mkullo kukubali tu kwamba wahisani wanaisaida serikali kujisafisha.

Wala Mkullo hana sababu ya kuzungumzia uhusiano wa wahisani na wapinzani kwa sababu tu serikali imeambiwa inanuka na ijisafishe; ikitaka isishurutishwe.

Ni vema Mkulo kama analitakia mema taifa hili, akalaumu uchafu wa serikali, badala ya uhusiano wa wapinzani na wahisani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: