Mkullo, si TRA pekee wanaostahili maisha mazuri


Alloyce Komba's picture

Na Alloyce Komba - Imechapwa 31 March 2009

Printer-friendly version
WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Mstapha Mkullo

WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Mstapha Mkullo amenukuliwa akiwaeleza wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mjini Mwanza wajitahidi kukusanya kodi zaidi na iwapo wanadhani kikwazo ni mishahara midogo, atamuomba Rais Jakaya Kikwete awaongeze.

Lakini katika hafla hiyohiyo, Kamishna mmoja wa TRA, alisema biashara ya magendo na uwezo mdogo wa utambuzi wa bidhaa zinazoingizwa vituo vya mipakani, ni miongoni mwa vikwazo vya ukusanyaji kodi zaidi.

Kamishna alieleza mambo mengine aliyoyaita ni vikwazo lakini kwa anayeelewa wajibu wa kisera na kisheria wa TRA tangu ilipoundwa mwaka 1996, atajiuliza shughuli yake nini hasa kama mishahara minono wanayolipwa haijaongeza nguvu ya ukusanyaji kodi huku wakisifiwa kisiasa.

Mwanzilishi mmojawapo wa TRA, Mushengezi Nyambele, mweledi na mzoefu wa masuala ya kodi, ananiambia halikuwa lengo la TRA kuendelea kuimarisha mishahara ya wafanyakazi wake, bila ya kufikia hatua ya kujenga maslahi ya watumishi wengine wa serikali wenye mchango mkubwa wa kodi kutoka mishahara yao.

Kumbe wanaopaswa kulipwa vizuri ni watumishi wengine pia ambao mchango wao wa kodi unaokatwa moja kwa moja kupitia Wizara ya Fedha au Hazina, ni mkubwa! Ndio maana hivi karibuni viongozi wa vyama vya wafanyakazi walipokutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, waliomba wapunguziwe makato kwenye mishahara yao.

Wataalam na washauri wa masuala ya kodi kama Nyambele ambaye ni mwanasheria mzoefu, wanasema TRA ingepaswa sasa iwe inakusanya kodi ya kati ya Sh. 400 bilioni na Sh. 600 bilioni badala Sh. 300 bilioni. Wigo wa ukusanyaji kodi bado ni mdogo mno, ukwepaji kodi unakua hasa katika bidhaa ya mafuta na rushwa na misamaha holela inaongezeka.

Kwa kifupi, TRA haijabuni vyanzo vipya vya mapato na hili limekuwa likisemwa na Kambi ya Upinzani kila mwaka wakati wa mkutano wa bajeti.

TRA haipati kodi inayostahili kutoka wafanyakazi wa makampuni ya nje yaani ma-TX wanaojifanya kulipa mishahara na marupuru haba kwa shilingi ilhali wanawekewa au kulipwa kwenye akaunti zao katika mabenki ya nje. Mishahara halisi yao haitozwi kodi. Sina hakika TRA wamechunguza hapa.

TRA wanawasiliana kiasi gani na Wakala wa Usajili wa Makampuni [BRELA] kujua ni mangapi yamesajiliwa nchini hivyo kulazimu yalipe kodi pamoja na wafanyakazi wake? Hii ndiyo kazi ya TRA badala kusubiri tu kodi za makampuni makubwa yenye ubia na Serikali kama TBL, viwanda vya saruji, mabenki na mashirika mengine yaliyobinafsishwa.

Lakini TRA ilipoanzishwa na wafanyakazi wake kuondolewa katika mfumo wa kawaida wa utumishi wa umma, bado ikapewa mishahara minono, mazingira mazuri ya kazi, kutukuzwa na kunyenyekewa. Historia inasema kumekuwa na harakati tangu baada ya uhuru za kuongeza mapato ya serikali kupitia makusanyo ya kodi.

Mwanzoni kodi zikikusanywa na idara tofauti Wizara ya Fedha na wahusika walikuwa watumishi wa kawaida. Kuna wakati ulikuwepo mfumo chini ya Jumuia ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977.

Bado makusanyo hayakuongezeka hata ilipoanzishwa Bodi ya Mapato mwaka 1993. Mwaka 1996 ikaanzishwa TRA kwa sheria ya mwaka 1995 ikiigwa ile iliyoanzisha Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA) iliyokuwa imefanikiwa kutokana na Rais Yoweri Museveni kutumia wataalam wa masuala ya kodi na uchumi wa Tanzania akiwemo Profesa Ibrahim Lipumba.

Serikali iliunda TRA nje ya mfumo wake wa utumishi ili kutoa uhuru wa mamlaka hiyo kuboresha maslahi ya watumishi wake na kuwapa nyenzo za kutosha ili kuwawezesha kukusanya kodi zaidi. Nia njema hiyo haikuenda sanjari na uwezo wa kifedha wa Serikali ya Awamu ya Tatu. Ilimudu kukusanya mapato Sh. 43 bilioni kwa wastani kwa mwezi.

Kilichofanyika, ambacho kifahamike kwa wafanyakazi wakiwemo wa TRA wanaojiona ni bora zaidi kuliko watumishi wengine kama walimu, madaktari na mahakimu, ni kuwa TRA chini ya Kamishna Mkuu, Melkizedeck Sanare (sasa marehemu) na Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Benno Ndulu (Gavana wa Benki Kuu), ilipata ufadhili kupitia Benki ya Dunia.

Benki hii ilishirikisha wafadhili wengine kugharamia mradi maalum wa kujenga uwezo wa TRA katika kusimamia sheria za kodi na kukusanya kodi ipasavyo; uliotengewa dola 75 milioni (sawa na zaidi ya Sh. 77 bilioni za Tanzania) kwa miaka mitano ya kwanza.

Baada ya mradi kukamilika kwa mafanikio makubwa, wafadhili waliongeza dola 33.6 milioni (sawa na Sh. 35 bilioni kipindi cha mwisho cha Rais Benjamin Mkapa kuelekea kuanza Serikali ya Awamu ya Nne – 2000/2001 – 2005/2006). Wanaoisifia TRA hawaelezi siri hii ya kihistoria.

Hapo TRA ikibebwa kwa asilimia 90 na wafadhili, wapi ilitoka asilimia 10 ya kujiendesha? Maana wafadhili waligharamia vifaa na vitendea kazi: kompyuta, mafunzo, ukarabati na ujenzi wa majengo. Hawakuhusika na mishahara na gharama nyingine za uendeshaji.

Kwa hiyo wajibu wa Serikali (ikijumuisha wafanyakazi wengine wote hasa walimu ambao ndio wengi) ulichangia kwa njia ya kodi “mishahara minono” ya wafanyakazi TRA wakitumaini watakapojiimarisha kimapato, watawezesha watumishi wenzao kuongezewa maslahi.

Kinachotokea sasa ni Mkullo kama mawaziri waliomtangulia kutoimarisha mishahara ya watumishi wengine ila kupigia debe TRA waendelee kuneemeka. Hakumbuki ni zamu ya TRA kujengea wenzao mazingira ya kulipwa vizuri kama wao. Iweje wao tu? Tunazungumzia TRA wepi? Hawa ambao rushwa imekithiri?

Ieleweke wajibu wa Serikali kwa TRA tangu ianzishwe, imekuwa ni kulipa mishahara na gharama nyingine za uendeshaji. Kwa mfano katika mpango wa pili wa TRA kwa mwaka 2006/2007, kasma ya mishahara na matumizi mengine ya kawaida ilipangiwa Sh. 47,926 milioni, kati yake, Sh. 34,047 milioni zikilenga mishahara na posho.

Ninataarifa kwamba kwa kuwa TRA ilikuwa na takribani wafanyakazi 3,200 kipindi hicho cha 2006/2007, inamaanisha kila mfanyakazi wake alikuwa ametengewa Sh. 10,639,687 kwa mwaka (sawa na Sh. 833,333 kila mwezi kwa mishahara na posho tu. Mapato makubwa ajabu kwa kiwango chochote.

Basi tukubaliane kuwa wafanyakazi wa TRA wamekuwa wakinufaika bila jasho kutokana na fedha za miradi ya wafadhili ikichagizwa na Benki ya Dunia huku ikichotewa pia kutoka bajeti ya serikali. Hii imekuwa rahisi kwake kubadili sura ya utawala wa kodi iliyokuwepo awali kwani mazingira ya kazi, nyenzo na maslahi ni mazuri.

Ni zamu yao kurudisha mapato ya kutosha serikalini bila kuomba malipo zaidi kutoka wanayopata. Wafanyakazi wake lazima wakusanye mapato mengi ili kuimarisha uchumi wa nchi na maslahi na mazingira mazuri ya kazi ya watumishi wenzao wa serikali. Tija kwa taifa itaongezwa na wote si TRA peke yao.

Haina maana yoyote Waziri Mkullo kuomba kwa Rais wafanyakazi wa TRA waongezewe mishahara. Hja hiyo haipaswi hata kuingia Baraza la Mawaziri maana ni ya kishikaji tu. Waziri aende kumkumbusha Rais changamoto kwa TRA sasa ni kukusanya mapato zaidi ili kustawisha hali za Watanzania wote.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: