Mkulo punguza vipaumbele vya bajeti


Sophia Yamola's picture

Na Sophia Yamola - Imechapwa 13 April 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

WAZIRI wa fedha Mustafa Mkulo ametaja vipaumbele 12 katika utekelezaji wa bajeti ya serikali ya mwaka 2011/2012.

Vipaumbele vya waziri Mkulo ni kilimo/mifugo/uvuvi; elimu; nishati; miundombinu; maendeleo ya viwanda; afya; maji; ardhi/nyumba/makazi; raslimali watu; sayansi/ teknolojia; huduma ya fedha na masuala mtambuka. Ni vingi mno.

Vipaumbele hivi vya sasa, ni nje ya ahadi ambazo Rais Jakaya Kikwete aliahidi wananchi wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu uliyopita. Katika kipindi hicho pekee, Kikwete aliahidi kutekeleza miradi mikubwa 67 nchi mzima.

Serikali makini, huja na vipaumbele vichache na kuvitengenezea mpango mkakati wa kuvitekeleza. Kwanza, hubainisha vyanzo vyake vya fedha; hufanya makadirio ya mapato yake na huja na mpango kabambe wa kuhakikisha nyufa zote za uvujaji mapato zinazibwa.

Unapokuwa na mambo mengi ya kuyashughulikia kwa wakati mmoja, huku uwezo wa kuyasimamia ukiwa mdogo, unalazimika kuchagua yapi ya muhimu kwa wakati ule.

Kwa mfano, serikali haina uwezo wa kutekeleza bajeti ya maendeleo bila msaada wa wahisani. Wahisani wanachangia asilimia 40 ya bajeti ya serikali.

Lakini wakati serikali inategemea wahisani kutunisha mfuko wake wa mapato, rais Kikwete amenukuliwa akisema asilimia 30 ya bajeti zinazotengwa kila mwaka hutafunwa. Asilimia 30 nyingine hugharamia utawala.

Angeniuliza, ningempa vipaumbele vichache kumuonesha njia. Elimu, afya, miundombinu, kilimo na ukusanyaji mapato.

Vinne vinavyotangulia kufuatana, vinahitaji uwekezaji mkubwa. Cha tatu kikifanikiwa, cha nne kitachochewa kufana. Kipaumbele cha nne, kilimo, chenyewe ni eneo zalishaji ambalo likifanikiwa, litakuza viwanda hasa vidogo vinavyotoa ajira nyingi, rasmi na zisizo rasmi.

Ukusanyaji mapato, ndiyo msingi mkuu wa uchumi wa nchi. Ungesema kiwe cha kwanza.Bila serikali kusimamia vizuri ukusanyaji mapato, haiwezi kuendesha shughuli zake.

Ni sawa na familia. Mkuu wake asipozalisha, haitakula. Haitamea. Itasinzia. Mwishowe, itakufa.

Serikali ikikusanya kila shilingi inayoingia wigoni, na ikiongeza maeneo ya ukusanyaji, itajenga nguvu za kutekeleza vizuri vipaumbele vinne vya kwanza.

Elimu ni ufunguo wa maisha. Ukijenga mtandao mzuri wa elimu, unazalisha wataalamu, nyenzo muhimu katika kupanga na kusimamia mipango ya maendeleo.

Sekta hii ni pana, inahitaji fedha nyingi. Majengo, madawati, vitabu vya kiada na ziada, walimu wenye ujuzi, maslahi bora na nyumba za kuishi.

Serikali isipotenga fedha za kutosha kuhudumia elimu, itabaki kutoa ahadi tu zisizotekelezeka kama ilivyofanya mwaka uliopita iliposhindwa kujenga nyumba 21,000 za walimu.

Kufikia sasa, imemudu nyumba 260 tu, sawa na asilimia 5.46 ya lengo.

Ilipoanzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) mwaka 2002, ililenga kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za serikali. Ilitoa ruzuku ya Sh. 10,000 kila mwanafunzi kwa mwaka ili kuziba pengo la ada lililoondolewa.

Sera ilikusudiwa kuendana na mahitaji ya taifa katika kutekeleza moja ya malengo ya milenia: Kuhakikisha kila mtoto anayestahili kusoma anapelekwa shule.

Malalamiko. Fedha zilicheleweshwa. Matokeo yake shule zikalazimika kuomba wazazi/walezi wa watoto wachangie.

Utafiti wa taasisi ya HakiElimu na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), zinazofuatilia sera za serikali kuhusu elimu, unaonesha kushuka kwa kiwango cha kufaulu wahitimu wa kidato cha nne kwa asilimia 22 mwaka 2010. Haya ni matokeo ya propaganda za kisiasa kutawala mipango ya elimu.

Lakini elimu itaimarika iwapo watoto wana afya nzuri. Sekta hii nayo ni pana inayohitaji bajeti ya kutosha.

Huduma za afya ni duni. Hospitali, vituo vya afya na zahanati hazitoshi, zilizopo zina msongamano wa wagonjwa, uhaba wa madaktari na wauguzi, vitanda, vitendea kazi, uchakavu wa majengo na madawa.

Tunahitaji kuimarisha huduma za kinga na tiba. Hili litafanikiwa iwapo hospitali zitaenea hadi vijijini, tutapata madaktari wanaojiamini kiujuzi na kimaslahi, na vitendea kazi vya kisasa, maabara na usafiri.

Huduma za mama na mtoto zimezorota na kusababisha vifo vingi.

Kila mwaka watoto 237,000 wa umri wa chini ya miaka mitano hufariki kwa magonjwa yanayotibika. Utafiti wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) unaonyesha zaidi ya asilimia 60 ya watoto hao hufia majumbani bila kufikishwa hospitali angalau mara moja.

Katika kila watoto 100 wenye umri huo, 44 wanakosa lishe bora; hivyo kupata utapiamlo. Hawatajenga kinga ya mwili na ubongo wao hautakua vizuri.

UNICEF inasema Tanzania inaongoza duniani kwa vifo vya wajawazito kwani inakadiriwa wanawake 21,000 hufa kila mwaka kwa matatizo ya uzazi. Ni asilimia 46 tu ndio hujifungulia hospitalini.

Takwimu za sensa za afya mwaka 2004, zinaonyesha vifo vya kinamama vinavyotokana na uzazi vimeongezeka hadi zaidi ya 600 kutoka 578 kwa kinamama 100,000.

Ni ukatili kwa wanawake kwa sababu vifo hivyo vinaweza kupunguzwa kwa zaidi ya asilimia 75 ikiwa wanawake wajawazito watapata huduma bora kwa wakati stahili, wakati wa kulea mimba na wanapotarajia hadi wanapokwisha kujifungua.

Zaidi ya kinamama 250,000 hupata vilema vya kudumu kila mwaka kutokana na matatizo hayo.

Katika bajeti ya serikali, kilimo kimetengewa asilimia 7 ya bajeti yote.Hakuna uchambuzi kuhusu matumizi.Masuala ya utafiti yametengewa asilimia moja tu.

Asili ya Watanzania ni kilimo. Kikipewa msukumo vizuri kwa kuwapatia wakulima pembejeo na masoko, watazalisha zaidi. Taifa litapata chakula cha kutosha na kingine kukiuza nje.

Kilimo cha kutegemea mvua na jembe la mkono hakitatuvusha. Lipo tatizo jipya: Ufisadi kutawala mfumo wa ununuzi na usambazaji wa pembejeo.

Baada ya utekelezaji wa Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA) kutoleta matunda kwa kiwango kilichotarajiwa katika awamu ya kwanza, serikali imekuja na kaulimbiu mpya: Kilimo kwanza.

Hata hivyo, kuna wasiwasi kama mapinduzi ya kilimo yatafanikiwa iwapo hakutakuwaa na nia njema na utashi wa kisiasa. Panahitajika nidhamu katika matumizi ya raslimali watu, ardhi, fedha na matumizi ya sayansi na teknolojia.

Leo, waziri Mkulo anajua bajeti ijayo imepungua kwa Sh. 510,417 milioni (Sh. 510 bilioni) maana mapato yameshuka. Serikali itatekeleza vipi vipaumbele 12?

Ndiyo maana anatamba hawawezi kuokoa wananchi na maisha magumu. Anataka, “kila mtu ale kwa jasho lake.” Kauli ya kiburi na kudhalilisha.

Ni vizuri akaeleza ni vipi raslimali ya madini itatumika kukuza pato la taifa kutoka mchango wa asilimia isiyozidi 3 ya sasa. Je, ataendeleza misamaha holela ya kodi ambayo inapoteza mapato?

Mbona hasemi kama serikali imeshaamua kuwafutia wawekezaji misamaha kwa miaka mitano ya kwanza wakati anajua fursa hiyo inatumiwa vibaya?

Aseme sasa serikali itatekeleza vipi vipaumbele 12 iwapo inaogopa kudhibiti ufisadi na mafisadi? Nadhani serikali inaamini ndoto.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: