Mkurugenzi wa Uchaguzi asiyejua uchaguzi


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 28 July 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

KATIBA inampa haki kila Mzanzibari kuandikishwa ili apige kura. Haijabakiza chochote kama kikwazo cha kupatikana haki hii. Tumeona makala iliyopita.

Kwenye vituo vya uandikishaji wapiga kura, wa kuingizwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK), kunashuhudiwa vituko vya firauni.

Viongozi wanaoitwa masheha, wanatumwa kuzuia watu kuandikishwa. Visingizio tele, lakini cha kutokuwa na kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi, kinaongoza.

Kweli hawaandikishwi. Tayari watu wapatao 3,000 wamekosa kuandikishwa katika majimbo ya Mgogoni na Konde. Uandikishaji unaendelea majimbo mengine ya Pemba kwa sasa.

Msikilize Sheha wa Shehia ya Kifundi, Omar Khamis Faki: Siwezi kutoa upya fomu maana nimeshatoa huko nyuma. Kama mtu amepoteza kitambulisho chake, ni mzembe."

Bila ya barua ya sheha, mwananchi hapati kitambulisho. Ni sheha anayetoa fomu kwa mtu aliyekataliwa kitambulisho.

Aonavyo, mtu analiyepoteza kitambulisho ni mzembe. Anyimwe haki. Lakini sheria ya kitambulisho, licha ya kushurutisha lazima mtu awe nacho, inakubali anayekipoteza, apatiwe kingine na ikibidi akilipie.

Ofisi ya Usajili na Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, inatoza dola 5 kwa kitambulisho kipya. Hizi ni Sh. 5,000.

Kwa msisitizo wa Sheha ambaye imedhihirika anafanya kazi zake kwa kufuata amri za wakubwa kuliko utaratibu, hakuna aliyepoteza kitambulisho atapata kingine. Amenyimwa haki.

Mkuu wa Idara ya Usajili na Vitambulisho, Wilaya ya Micheweni, Hamad Shamata, naye anasema: Sisi tumepewa maelekezo na Mkurugenzi (wa Idara)."

Mkurugenzi wa Idara hii, Mohamed Juma, hakupatikana kutueleza juu ya jambo hili. Hapo nyuma, amepata kusema hakuna malalamiko kwake ya watu kunyimwa kitambulisho.

Lakini, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, Abdalla Ali Said, anaonyesha kwa waandishi wa habari waliofuatilia uandikishaji, stakabadhi za watu kumi waliokataliwa na bila ya kuelezwa sababu.

Walijaza fomu na kulipia lakini hawajakabidhiwa hadi maofisa wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) wanapita kuandikisha wapiga kura.

Hivyo ni vikwazo vya Mzanzibari kupata haki yake ya kuandikishwa katika daftari ili atambuliwe kama mpiga kura.

Kikwazo kingine: maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa wamezunguka kituo cha uandikishaji na wanafukuza watu waliofika kujiandikisha. Wanawataka waondoke. Hawataki waandikishwe.

Huku ni kuthibitisha uandikishaji wapiga kura unadhibitiwa na dola: Usalama wa Taifa, Polisi na vikosi vya ulinzi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, vinavyotajwa sana kwa kutumika vibaya.

Vikosi hivi vinatoa mchango mkubwa kufanikisha "ushindi wa kishindo" wa CCM.

Tume ya Uchaguzi katika ripoti yake ya 2005, ilieleza jambo hili. Ilisema vinatumiwa na viongozi wa serikali kuingilia sheria ya uchaguzi.

Juu ya mazonge yote haya, unakuta Mkurugenzi wa Uchaguzi, Salum Kassim Ali, anatoa majibu ya jeuri na yanayoonyesha hajui maana ya uchaguzi huru.

Kila akiulizwa ufumbuzi wa kadhia ya kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi kuwa turufu ya mtu kuandikishwa, anasema hilo si jukumu la Tume.

Anasema kazi ya Tume ni kumwandikisha yule mwenye sifa aliyefika kituo cha uandikishaji. Hajali kama baadhi ya wanaonyimwa kuandikishwa, ni wale waliopiga kura 2005 hivyo wanazo shahada zao.

Kwa utaratibu wa utendaji wa Tume, tayari imeshathibitika kwa mara nyingine, haina mamlaka ya kusaidia watu wanaokwama kupata kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi.

Hiyo maana yake maelfu kwa maelfu ya wananchi, na hasa vijana waliotimiza umri wa miaka 18 kutoka 2005, watakosa haki ya kupiga kura uchaguzi wa Oktoba mwakani.

Kuna tatizo jingine na kutengenezwa na mfumo. Tunaambiwa vituoni, wapo watu wamekataliwa kuandikishwa kwa sababu hawana kitambulisho; wengine wanacho kitambulisho lakini wamekataliwa; kisa? Hawana shahada ya kupigia kura ya 2005.

Kwa hivyo, kumbe tatizo si kitambulisho hiki tu peke yake. Lipo tatizo ambalo wanaodhibiti mfumo wa utawala ndio wanalijua. Tulio nje ya mfumo, tunaona ni ubaguzi na utawala mbovu.

Kwa hesabu za juujuu, iwapo majimbo mawili ya Konde na Mgogoni, yametoa zaidi ya watu 3,000 walionyimwa kitambulisho na hivyo kukosa kuandikishwa, uandikishaji ukimalizika katika majimbo yote 50, tutarajie watu wapatao 100,000 (laki moja) watakosa.

Tume haijali kamwe kama ina jukumu la kuondokana na mkwamo huo. Na hii ndiyo ile Tume ambayo mwenyekiti wake, Khatibu Mwinchande, kada wa Chama cha Mapinduzi, na baadhi ya makamishna wake, wameapa kutekeleza majukumu kwa kufuata sheria na taratibu.

Katika hali kama hiyo – ya maelfu ya watu kunyimwa haki ya kuandikishwa kama wapiga kura – Mkurugenzi wa Uchaguzi anasema uchaguzi utakuwa huru na wa haki.

Anasema, kama alivyonukuliwa na waandishi waliokuwepo vituoni, "kasoro hiyo haimaanishi kwamba uchaguzi visiwani hapa hautakuwa huru na wa haki."

Anapoulizwa na mwandishi kama haoni kunyima watu haki ya kuandikishwa na kuingia kwenye daftari, kutaathiri vigezo vya uchaguzi huru na wa haki, anabwatukia mwandishi:

"Usiseme uchaguzi hautakuwa huru na wa haki, wewe kama mwandishi andika unachokiona. Usirukie mambo kabla ya uchaguzi kufanyika. Nani kakuambia uchaguzi hautakuwa huru na wa haki kwa sababu tu watu hawakuandikishwa?"

Elimu aliyonayo mkurugenzi wa uchaguzi huyu, inampa imani kuwa uchaguzi huru na wa haki hupimwa siku ile tu watu wanapopiga kura.

Anaamini kabla ya siku ya upigaji kura, hakuna vigezo vya kuufanya uchaguzi uwe huru au kinyume chake. Huku ni kupotoka kwa kiwango cha juu. Haitarajiwi mtumishi wa umma aliyepewa jukumu la kusimamia uratibu wa uendeshaji uchaguzi hafahamu maana ya uchaguzi.

Hii ni fedheha kwake na kwa aliyemteua. Uchaguzi ni mchakato au hatua mbalimbali kabla ya siku ya kupiga kura. Na mtu anapotaja "uchaguzi huru na wa haki" basi yapasa afahamu kuwa kigezo cha kwanza ni ukataji wa majimbo.

Ndio maana hata hatua hii imeelezwa kwenye katiba na sheria ya uchaguzi. Uchaguzi huru ni ule ambao kila hatua ilitekelezwa bila shinikizo zozote za nje ya sheria na taratibu.

Uchaguzi huru na wa haki, ni ule ambao kila hatua yake katika mchakato, ilitekelezwa kwa uhuru unaostahili na kwa kumshirikisha – kwa maana ya kumpa haki – kila anayestahili kuipata haki ya kushiriki uchaguzi.

Walezi na waamini wa demokrasia ya kweli, wanasema uchaguzi huru na wa haki ni ule uliofanyika katika hali ya uwazi kwenye kila hatua yake. Iwapo yapo mambo yanafanyika kwa uficho; kwa mfano kuhesabu au kujumuisha kura kunafanywa ufichoni.

Mkurugenzi wa Uchaguzi lazima arudi darasani. Akaangalie "uchaguzi" maana yake nini. Halafu arudi maktaba ya ZEC, kupitia ule waraka wa "Maadili ya Uchaguzi Huru kwa nchi za SADC" ambao wenzake mwaka 2005 waliuridhia na kuahidi kuuzingatia.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: