Mkutano wa Leon Sullivan: Watanzania tumejifunza nini?


Joseph Mihangwa's picture

Na Joseph Mihangwa - Imechapwa 17 June 2008

Printer-friendly version

MKUTANO wa Leon H. Sullivan uliokutanisha watu weusi wenye asili ya Kiafrika waliotawanyika kote duniani (Diaspora) na ambao Tanzania iliwekeza kwa njia ya kuugharamia, umemalizika mjini Arusha na kuacha swali ambalo halijajibiwa: Watanzania tumevuna nini?

Kuja kwa watu wenye ushawishi mkubwa Marekani, kumethibitisha mantiki ya wimbo wa kale wa watumwa usemao: "Afrika nakutamani; nikikumbuka sifa zako? Tuliuzwa kama samaki?..nikikumbuka Afrika?."

Hata hivyo, ni mapema kupata jibu la lengo la kwanza la mkutano. Tujipe muda; tutaanza punde kuona mitaji ya uwekezaji ikitiririka na mito kufurika asali na maziwa mithili ya nchi ya ahadi- "Kanaani".

Lakini pamoja na hayo, wana ushawishi gani kwa ubepari wa kimataifa kuweza kuiokoa Tanzania na Afrika ikiwa ni juzi juzi tu nao walikuwa wakitoka jasho kupigania haki zao dhidi ya ubaguzi wa rangi?

Lengo la pili, linaweza kuwa na mantiki zaidi kwa sababu ushirikiano uliopo una historia ndefu, kuanzia mkutano wa kwanza wa Manchester mwaka 1945.

Mkutano huo ndiyo uliokuwa chimbuko la harakati za ukombozi wa mtu mweusi zilizochochewa na watu weusi kama Dakta William Du Bois na mwangwi wake kuitikwa na kina Kwame Nkrumah, Jomo Kenyatta na wengineo.

Umuhimu wa jumuiko la mkutano wa Leon H. Sullivan unaweza kuelezewa kwa usahihi zaidi kama juhudi za kuunganisha Waafrika popote walipo katika kutetea hadhi na heshima ya bara lao dhidi ya dharau na kejeli za nchi zilizoendelea, zinazomchukulia kama juha katika zama hizi za utandawazi.

Afrika imeitwa "bara la giza" kama ilivyo ngozi nyeusi ya Mwafrika. Imeitwa bara lisilo matumaini wala utamaduni wa kutoa au kuigwa na mabara mengine.

Afrika imeitwa bara la "utupu na ukimya" wa kutisha wanaloishi kwamba ni viumbe waliolaaniwa, waliokata tamaa, wanaohitaji kuvumbuliwa na kukombolewa.

Lakini linapokuja suala la uporaji malighafi na raslimali, Afrika ni "kipenzi" cha weupe. Lester Thurow, mmoja wa wasomi wapendao utandawazi, katika kitabu chake alichokiita, "Head to Head: The Coming Economic Battle Among Japan, Europe and America" anasema: "Kama Mungu angekupa bara hili na kukufanya dikteta wake kiuchumi, njia nzuri ni kumrudishia."

Naye mvumbuzi na msafiri wa kizungu Sir Richard Burton, anamuelezea Mwafrika kuwa "akifikia mtu mzima akili yake hudumaa; huanza kukua kinyumenyume badala ya kwenda mbele; anaweza kuiga na kuigiza kama nyani, lakini hawezi kuvumbua wala kuunda kitu hata (namna ya) kukitumia."

Dharau hii inatokana na historia ya Mwafrika ya utumwa na kutawaliwa. Hata mwalimu alililamikia hilo. Alisema, "Mila nyingi za kizungu zimeingia zikafuta za kwetu na hata kuharibu utaifa wetu. Angalia, ule umoja na mshikamano wetu wa Kiafrika unakwisha. Ule msemo wetu wa zamani kwamba "Niko kwa vile tuko" unakufa."

Mwalimu, licha ya kuwa Mkristo mzuri, hakuchelea kuzikosoa dini za kigeni. "Ukristo umeathiri sana mila zetu, umevuruga utamaduni wetu wa kuabudu eti kwamba huo ni upagani. Huu ni upuuzi mtupu; ni dharau kwa Mwafrika?. Wamishonari walikosea walipotuhukumu kwa kutuangalia Kizungu."

Kwa sababu hii, ilizuka dhana potofu ikadumu hadi enzi za uhuru, kwamba kadri Mwafrika wa "kisasa" alivyojiweka mbali na watu (wake) wa vijijini (na hofu ya kuitwa "mshamba"), ndivyo alivyojiona au kuonekana amestaarabika zaidi.

Baadhi ya viongozi wa harakati za uhuru walionaswa na mtego huu ni pamoja na Dakta Hastings Kamuzu Banda (Malawi), Leopold Sedar Senghor (Senegal), Felix Houphouet Boigny (Ivory Coast), Jean Bedel Bokassa (CAR) na hata Charles Njonjo (Kenya), aliyekataa kupanda ndege aliyorusha rubani Mwafrika.

Basil Davidson (The Black Man's Burden) anasema, hata marehemu Jomo Kenyatta (Kenya) alikuwa hivyo hadi alipogeuzwa fikira na wanamapinduzi kama kina Tom Mboya, Jaramogi Oginga Odinga.

Kanyata alipendelea kuiona Kenya hata ikijitawala inabaki chini ya himaya ya Malkia wa Uingereza kama zilivyo Canada, Australia na New Zealand.

Aliamini matatizo ya Afrika yangeweza kutatuliwa kwa njia zilezile zinazotumika kutatua matatizo ya nchi za Ulaya.

Kanyata na wenzake walichotaka si uhuru wa kweli, bali kile walichokiita "haki yao ya kuchukua nafasi ya Wakoloni na kutawala kwa maelekezo ya Wazungu walioondoka kwa maana ya "Ukoloni mamboleo."

Ndiyo maana, zaidi ya miaka 40 ya Uhuru sasa, Afrika ni masikini kuliko hata kabla ya uhuru; uchumi wake umedumaa na mwingine unayoyoma haraka.

Baadhi ya Wazungu wanaoipenda Afrika na Waafrika, wameandika mengi kuelezea chimbuko la matatizo ya Afrika na kuumbua wale wasioitakia mema, na ambao wangetaka kuona Mwafrika akitekwa kiroho, uhuru wake na azma ya ukombozi. Wazungu hao wema ni pamoja na Basil Davidson.

Tunatarajia wenzetu wa Leon H. Sullivan watatoka ndani ya tumbo la "Dudu" kama watu waliotakasika na dhambi kuu ya Dudu, linalojiona kama mteule wa Mungu wa kuwaokoa wengine.

Falsafa hii sio mpya, ni ya tangu enzi za ukoloni, Mkataba wa kuundwa kwa Ushirika wa Mataifa (League of Nations), Umoja wa Mataifa (UN) hadi watetezi wa sasa akina Jeffrey Sachs na Waziri Mkuu wa sasa wa Uingerza, Gordon Brown.

Tanzania inashabikia falsafa ya Sachs katika kufufua uchumi, na tumewahi kumwalika nchini kusoma "Injili" yake ambayo Profesa Easterly anaiita "uropokaji wa Sachs na Brown", kwamba mipango yao ya kibeberu na kinyonyaji haijasaidia nchi masikini kwa sababu haiwagusi wala kuwahusisha watu wa chini (wa mashenzini) na ambao ndio wengi. Misaada haiondoi umasikini bali kupunguza tu maumivu.

Easterly, Mchumi mstaafu wa Benki ya Dunia anaamini misaada haiwezi kuwa motisha wala tija ya kuondoa umasikini; itashindwa kama ilivyoshindwa kwa miaka 50 iliyopita na hivyo nchi masikini ziachane na njozi hizo.

Anasema kukua haraka kwa uchumi wa nchi kama Japan, China, Indonesia, India, Korea Kusini na Taiwan kuliwezekana tu kwa wao kukataa "Injili" ya IMF na Benki ya Dunia, kupokea misaada na hazikuwahi kutawaliwa Magharibi, vinginevyo uchumi wake nao usingeweza kung'oa nanga.

Zaidi ya asilimia 80 ya wanamtandao wa Leon H. Sullivan wanaishi katika nchi za ubepari uliokomaa na wamekuwa sehemu ya utamaduni huo. Sasa ni kwa kiwango gani wanayaona matatizo yetu ni yao ili wathubutu kusema "damu ni nzito kuliko maji"?

Kama hilo hawalioni (na hivyo ndivyo tunavyohisi), basi, Mkutano wa Nane wa Leon H. Sullivan ulikuwa ziara nyingine ya kitalii kwa watu waliong'olewa mizizi katika bara lao la asili.

0
No votes yet