Mlimani City ‘si salama?’


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 21 March 2012

Printer-friendly version

MAEGESHO ya magari mbele ya masoko makuu ya Mlimani City yameelezwa kuwa “si salama.”

MwanaHALISI limeelezwa kuwa hivi karibuni, gari la Prof. Kulikoyela Kahigi lilivunjwa kioo cha dirisha na kompyuta yake ndogo kuibwa.

Naye Prof. Joseph Mbelle wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amewahi kuibiwa kompyuta yake ndogo kwenye maegesho hayohayo. Dirisha la gari lake lilivunjwa na wahusika kutokomea.

Juzi, Jumatatu, ofisa mmoja wa bunge aliliambia gazeti hili, “Nilipaki gari langu tarehe 21 Februari mwaka huu. Nikaondoka na kuingia sokoni. Nilikuta wamebomoa.”

Ofisa huyo alieleza katika sauti ya huzuni, “Niliporudi nilikuta kioo cha dirisha nyuma kimevunjwa na kompyuta yangu ndogo imechukuliwa.”

Amesema alipomweleza ndugu yake juu ya tukio hilo, alielezwa na ndugu yake kuwa yeye si wa kwanza kuibiwa katika viwanja hivyo vya kuegesha magari.

Ofisa aliyeibiwa kompyuta amesema alivyoarifu tukio hilo kwa kampuni ya OMEGA Nitro inayofanya lindo katika eneo hilo, walisajili tukio hilo kwa Kumb. Na. OB No. 1763 kwa lindo la Mlimani City.

Aidha, walitoa OB No. 684 kwa makao makuu yao yaliyopo Mikocheni, Dar es Salaam na kuahidi kuendelea kuchunguza. OB ni kama RB za polisi wakati mtu anaporipoti shauri.

Aliyeibiwa kompyuta anasema alikuwa ameegesha gari “hatua chache” kutoka kwenye kichanja alipokuwa amekaa askari wa kampuni hiyo ya ulinzi.

Mkaguzi wa malindo wa OMEGA Nitro inayotokea Afrika Kusini alifika na kushuhudia jinsi wizi ulivyotokea.

“Cha kushangaza ni kwamba niliomba atafutwe askari aliyekuwa analinda eneo hilo, aliyekuwa kwenye kichanja pale juu; lakini walishindwa kumpata eti hawamjui.

“Jambo hilo lilinipa mashaka kuwa wizi unaotokea hapo una uhusiano wa moja kwa moja na walinzi wa kampuni iliyopata kandarasi ya kusimamia usalama wa wajeta na mali zao,” anasema.

Ofisa huyo anasema ni aibu kwa eneo kama Mlimani City kutokuwa na kamera za usalama (CCTV) za kusaidia lindo kwa kuonyesha kila tendo ndani ya maegesho.

“Nimeambiwa kila anayeibiwa huambiwa kuwa utawala wa eneo hauhusiki na lindo la gari lake. Huu ni upuuzi,” amesema huku akilalamika.

“Wanakimbilia kuonyesha kadi kuwa unapoingia na gari lako, unapewa kadi ambayo nyuma yake inaeleza kuwa usalama wa mali yako ni juu yako na kwamba unatakiwa kuondoa vitu vya thamani katika gari ulilopaki,” anaeleza.

Ofisa huyo anakataa maelezo hayo akisema, “Kama hivyo ndivyo, kwanini wanatoa kandarasi kwa kampuni ya ulinzi ya kuhakikisha usalama wa eneo lao?”

0
No votes yet