Mmiliki Dowans aja na mazingaombwe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 23 February 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

BRIGEDIA Jenerali mstaafu, Suleiman Mohammed Yahya Al Adawi, anayetajwa kuwa mmiliki wa kampuni ya kufua umeme ya Dowans Holdings SA ameongeza utata nchini.

Al-Adawi alitua Dar es Salaam, Jumapili iliyopita akitokea Oman kwa lengo la kumaliza utata kuhusu hisa zake, lakini akakataa kupigwa picha.

Hakutaka Watanzania wengine waone sura yake. Kwa hiyo, waliofanikiwa kumwona ni waandishi wateule waliohudhuria mkutano huo uliofanyika katika hoteli ya Kilimanjaro Kempiski, isipokuwa wa MwanaHALISI.

Waandishi wa MwanaHALISI kutengwa si jambo la kushangaza kutokana na msimamo wao katika masuala mengi likiwemo la Dowans.

Maswali yanaibuka: Kwa nini mtu mwenye hisa nyingi (mmiliki) alikataa kupigwa picha wakati alikuja nchini kukata mzizi wa fitina juu ya mmiliki halali wa Dowans?

Alikuwa anaogopa nini wakati amekuja kudai tuzo ya Sh. 94 bilioni aliyoshinda katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Biashara (ICC) dhidi ya TANESCO?

Katika majibu yake, Al Adawi alidai kwamba kokote anakokwenda huwa anakataa kupigwa picha, kwa hiyo hakutaka kuvunja mwiko huo hapa nchini.

Kitendo cha kuficha sura yake kimeongeza utata, kwani mshirika wake mkuu katika sakata hili, Rostam Azizi anayedaiwa kumshawishi mwarabu huyo alete mitambo ya kufua umeme nchini ni kiini cha utata huu.

Rostam Azizi, mfanyabiashara na Mbunge wa Igunga (CCM) awali alidai haifahamu kampuni ya Richmond iliyoshinda zabuni ya kufua umeme mwaka 2006, na alidai haifahamu Dowans iliyorithi mkataba baadaye.

Pamoja na kukataa kuzijua kampuni hizo ndiye wakati wote amekuwa akiita waandishi na kujibu tuhuma zote dhidi ya Richmond na baadaye Dowans.

Ushiriki wa Rostam Azizi katika kampuni mbili hizo umejulikana wazi katika hukumu ya kesi iliyofunguliwa na Dowans katika ICC dhidi ya TANESCO kwa kuvunjiwa mkataba iliorithi.

Ni katika hukumu hiyo, Rostam Azizi inadaiwa alifanya ushawishi Richmond kushinda zabuni, na ni katika hukumu hiyo ametajwa kwamba amepewa mamlaka kisheria (Power of Attorney)  ya kusimamia shughuli za Dowans duniani kote isipokuwa Costa Rica.

Rostam ndiye aliyemleta Al Adawi kutegua kitendawili cha Dowans, lakini mwarabu huyo anaongeza utata kwa kudai pia haifahamu Richmond. Dowans ilirithi vipi mkataba wa kampuni ambayo mmiliki haijui?

Haya ni mazingaombwe.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: