Mnamlinda Pinda au mna lenu jambo?


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 22 December 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

KATIKA lugha ya Kifaransa, kuna maneno ambayo mtu hatakiwi kuyasema hadharani. Mojawapo ni neno Merde. Hata hivyo, baada ya kusikia kilichotokea katika Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es Salaam Ijumaa iliyopita, nilishindwa kujizuia kusema neno hilo.

Mhariri Mtendaji wa gazeti hili, Saed Kubenea, alikuwa amekwenda kwenye ofisi hizo kuhudhuria mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na ofisi hiyo. Hata hivyo, alikataliwa asiingie ndani ya mkutano huo.

Sababu pekee iliyotolewa na Mwandishi wa Waziri Mkuu, Irene Kakiziba Bwire, kumzuia Kubenea asiingie ndani ya mkutano huo ni kuwa hakuwa amealikwa. Sababu ya kijinga kabisa, kwa kifaransa ningesema Merde.

Cha ajabu ni kwamba Irene alitupa lawama kwa bosi wake, Said Nguba, kuwa ndiye aliyeandaa orodha ya waandishi waalikwa. Kwamba kwa kuwa Nguba alikuwa amesahau waandishi, yeye asingeweza kufanya chochote.

Irene anamfahamu Kubenea. Na hamfahamu kwa jina tu lakini anamfahamu kwa sura na wadhifa wake. Si kwamba alimnyima mwandishi huyo ruhusa ya kuingia mkutanoni kwa sababu hakuwa akimfahamu.

Irene alimkatalia Kubenea ruhusa ya kuingia kwenye mkutano huo kwa makusudi. Alijua anachokifanya hata kama alimsukumia Nguba mzigo huo.

Na hii si mara ya kwanza kwa Irene kukataa kutoa taarifa kwa MwanaHALISI. Kuna kipindi, aliwahi kukataa kutoa namba ya simu ya msaidizi wa karibu wa waziri mkuu kwa sababu anazozijua yeye.

Ana hasira na MwanaHALISI. Waingereza wangesema ana ‘vendetta’ na gazeti hili. Ana chuki na MwanaHALISI. Halipendi. Halitaki.

Cha ajabu ni kuwa, gazeti hili, kwa kadri ya kumbukumbu zangu, halijawahi hata siku moja kuzozana na mwanamama huyo. Linampenda na kumheshimu kama ilivyo kwa watumishi wote wa umma.

Zaidi, MwanaHALISI halijawahi kuzozana na bosi wa sasa wa Irene, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Lakini, gazeti hili limewahi kumchunguza kwa kina na kubaini bosi wa zamani wa Irene, Edward Lowassa alivyogubikwa na kashfa ya Richmond. Irene na Nguba waliajiriwa kipindi cha Lowassa.

Irene, ambaye kitaaluma ni mwandishi amezima fursa ya MwanaHALISI kumsikiliza Waziri mkuu wakati akizungumza na wananchi kupitia kwa wahariri wa habari.

Kwanza alikuwa akifanya kazi katika gazeti la Majira na baadaye kama Mwanaharakati katika Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA).

Mimi ni miongoni mwa wanahabari tuliofurahi wakati Irene alipoteuliwa kuwa mwandishi wa habari wa waziri mkuu. Kwa historia yake kama mwanahabari na mwanaharakati, nilidhani ofisi hiyo kubwa na nyeti itakuwa wazi zaidi kwa wanahabari.

Sikutegemea kama Irene angeweza kuthubutu kufanya alichokifanya dhidi ya Kubenea. MwanaHALISI limesajiliwa na linafahamika kote nchini, Irene alikuwa na sababu gani ya kumkatalia mwandishi mwenzake kama hakuwa na maagizo kutoka mahali kwingine?

Nimemfahamu Pinda kwa muda mrefu kidogo. Ni msomi mzuri na ana uzoefu mkubwa wa kazi unaotokana na kufanya kazi kwa karibu na viongozi werevu wa nchi yetu.

Pinda alikuwa msaidizi wa Mwalimu Nyerere. Aliwahi kuwa msaidizi wa Benjamin Mkapa. Ni mwanasheria, taaluma inayomfanya asiwe mwoga kuzungumza mbele za watu.

Katika vikao vya Bunge, Pinda anajibu maswali magumu kutoka kwa wabunge kwa umakini na ufasaha jambo ambalo mara zote, limemjengea heshima sana mbele ya jamii, amekuwa mkweli kwenye majibu yake.

Kwa maelezo haya, ni vigumu kuamini kwamba mtu mwenye uwezo na uzoefu huu anaweza kufanya mpango wa kukimbia maswali ya Kubenea tu. Kuna kila sababu ya kujenga shaka kuwa Irene alikuwa anatekeleza maagizo ya mtu mwingine na si bosi wake huyu.

Pinda angejibu swali lolote ambalo angeulizwa na kama angekuwa hana jibu, angesema. Huyo ndiye Pinda tunayemfahamu.

Irene ni aina ya waandishi ambao ni vigumu kufahamu nini kimewakuta. Wameingia kwenye nafasi zao za sasa kwa sababu ya kuwa wana taaluma ya habari, lakini wanafanya kila wawezalo kuwadhalilisha wanahabari wenzao.

Alichokifanya kwa Kubenea wiki iliyopita, hakitamjengea sifa kokote mbele ya macho ya wanahabari na sidhani kama ofisi ilimtaka azuie MwanaHALISI kuwaeleza wananchi alichosema Waziri mkuu. Na kazi anayofanya sasa si ya kudumu.

Hana hisa yoyote katika cheo cha waziri mkuu. Jacob Tesha, Isaack Mruma, Akadonga Chiledi na wengine wamepita katika nafasi aliyonayo sasa na wameondoka. Ipo siku na yeye ataondoka pia.

Kwa bahati nzuri, magazeti yataendelea kuwapo hata yeye atakapoondoka. Bahati nzuri, taaluma yake ni uandishi wa habari, hatakuwa na pa kwenda zaidi ya kurudi kwenye fani hii.

Atawatazama vipi wana habari wenzake kama akina Kubenea pale naye muda wake wa kurejea kijiweni utakapowadia? Atapata wapi mamlaka ya kujiita mwandishi wa habari mbele ya wenzake?

Siamini kama Irene na au Nguba walifanya walichofanya kwa Kubenea lengo likiwa ni kumlinda Pinda. Siamini kama Pinda anahitaji ulinzi wa aina hiyo na kama anahitaji, basi kuna kitu hatukifahamu vizuri kuhusu waziri mkuu wetu.

Lakini, kama Irene alifanya alichokifanya kwa sababu ya mtu mwingine, basi ni wazi kuwa Pinda hayuko salama.

Ina maana Irene anafanya kazi ya mtu mwingine anayekinzana na Pinda. Na inawezekana, inawezekana kabisa, kuwa Irene ni mwaminifu zaidi kwa huyo kuliko kwa Pinda.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: