Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 25 January 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

KAULI aliyoitoa Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro kuhusu uanachama wa Profesa Abdallah Safari ina madhara.

Iwapo alinukuliwa kwa usahihi kusema kwamba tukio la kuhama CUF kwa Profesa Safari ni tukio la kawaida, basi kauli hiyo ya Mtatiro haikuwa na tija.

Kwa wengi, kauli hiyo inaweza kuonekana ya kawaida isiyo na tatizo. Lakini, kwa wale waliopata bahati ya kufuatilia mwenendo wa siasa za mageuzi nchini, wanaweza kujua athari zake.

Kwa watu wa rika langu linalofanana na lile la Mtatiro, na ambao kwa bahati mbaya hatukuwa tumeanza hata darasa la kwanza wakati harakati za mageuzi zilipoanza na hatukuwa tumezaliwa katika miaka 15 hadi 20 ya kwanza baada ya uhuru, pengine kuna vitu huwa tunazungumza bila ya kujua kile tunachozungumza.

Ili kufahamu wapi tulikotoka, angalia mifano ijayo michache. Majuzi kabla ya kampeni za uchaguzi mkuu kuanza, niliwahi kuzungumza na aliyekuwa mgombea urais wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa.

Alinieleza namna siku moja, miaka zaidi ya kumi iliyopita, alivyokutana na mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Faida Mohamed Bakari, wilayani Kiteto mkoani Manyara. Alisema walisalimiana kwa furaha na kukumbatiana.

Siku chache baadaye, Dk. Slaa alipata taarifa kuwa Faida alipewa karipio kali na chama chake kutokana na kusalimiana kwake naye. Maana yake, kosa la mbunge Faida, lilikuwa ni kusalimiana “kwa furaha na mtu wa upinzani.”

Leo hii, watu wa CCM na upinzani wanakutana na kucheka pamoja. Lakini wapo watu waliowahi kuchukuliwa hatua kali zilizoharibu maisha yao moja kwa moja kwa sababu ya mahusiano yao na upinzani. Tumetoka mbali.

Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF, alikuwa rafiki mkubwa wa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha. Hata majina yao ya kwanza yanafanana!

Lakini, kuna kipindi, nilipata kuambiwa na mmoja wa watu rafiki wa wanasiasa hao wawili kuwa Dk. Msabaha alikuwa akimkwepa Profesa Lipumba mara tu profesa huyo alipojiunga na kambi ya upinzani.

Dk. Msabaha alijua wazi kwamba angeingia matatizoni iwapo angeonekana ni rafiki wa Profesa Lipumba. Akaamua kumtosa. Na wapo wengi waliomtosa Profesa Lipumba kama rafiki yao kwa sababu tu amekuwa mwanasiasa wa upinzani.

Profesa amepoteza fursa na marafiki wengi kwa sababu ya kujiunga na CUF. Akiudhiwa kitu miaka 10 ijayo na akaamua kuhama chama hicho, kiongozi kijana au mtu mzima ataibuka na kusema “aondoke tu, hakufanya lolote.”

Abdalla Kassim Hanga, alikuwa mwanasiasa mahiri wa Zanzibar katika miaka ya harakati za ukombozi hadi miaka ya 1960. Kwa sababu ya upinzani wake kwa sera za aliyekuwa rais baada ya mapinduzi ya 12Januari 1964, Abeid Amani Karume na mahusiano yake na watu waliodaiwa kupanga njama za ‘kuhujumu’ mapinduzi, aliuawa.

Kama angekuwa hai leo na kuamua kujiunga na chama chochote kingine, nahisi wangejitokeza viongozi wa chama alichohama kumponda. Kwamba hakufanya lolote au si lolote. “Ni mtu wa kawaida sana.”

Kwa suala la Mtatiro, sina hakika kama anajua kuwa Profesa Safari alikuwa miongoni mwa wasomi wa mwanzo na waajiriwa wa serikali kujiunga na vyama vya upinzani baada ya mfumo wa vyama vingi kurudishwa mwaka 1992.

Mtatiro sijui kama akijua kuwa Profesa Safari alifukuzwa kazi kwa sababu ya kumtetea Profesa Lipumba katika ile kesi yake ya uchochezi ya mwaka 2001. Profesa Safari ndiye aliyekuwa mshauri wa sheria wa CUF.

Maisha yake yaliharibiwa baada ya kufukuzwa kazi. Baba yake mzazi, Kapteni Jumbe Safari, alipatwa na ugonjwa wa kiharusi na baadaye kufariki dunia kwa sababu ya kadhia iliyompata mwanawe huyo ya kufukuzwa kazi. Aliumia kwa kufikiria itakuaje.

Mtu kama huyu anapohama chama chako, inatakiwa wahusika waonyeshe heshima kwake. Hata kama hawakubaliani naye, ni muhimu kuonyesha heshima kwa kwa kile alichokileta.

Ni sawa tu na namna baadhi ya viongozi wa chama cha NCCR-Mageuzi, walivyomponda Mabere Marando, pale alipotangaza kukihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Wanachama wa NCCR-Mageuzi wanapaswa sana kumshukuru Marando. Na hili si kwa chama hicho pekee lakini kwa wapenzi wote wa siasa za mageuzi nchini.

Marando na Ndimara Tegambwage ni miongoni mwa Watanzania waliokuwa waasisi wa mageuzi ya kisiasa nchini. Walipoteza marafiki, walinyanyaswa, walipigwa kwa virungu na mabomu ya machozi. Walivunjiwa hadhi zao kama wanadamu.

Harakati zao ziliwafanya wao na familia zao kuishi katika hali ya wasiwasi na shaka kwa muda mrefu. Leo hii, vijana kama mimi na Mtatiro tunafaidi zile haki ambazo wanamageuzi hao walizipigania na huenda wasingezifaidi. Wanastahili heshima.

Sasa badala ya kuonyesha heshima kwao, tunawaponda wanapoamua kufanya maamuzi ambayo hatuyapendi. Sisemi wao si binadamu na hawawezi kukosea. Nazungumzia kuwaheshimu kama watu muhimu waliotoa mchango katika jamii.

Nchi yetu ina bahati mbaya kwamba historia yake, kuanzia upatikanaji wa uhuru, haijaelezwa vizuri hasa kwa vijana kama mimi. Kuna upungufu mkubwa katika suala hilo.

Najua baadhi ya vitabu vimeyaeleza masuala ya historia ya uhuru na yaliyokuja baadaye, lakini kuna tatizo vijana wangapi wamevisoma.

Ndiyo maana, si ajabu kuona Watanzania wengi hawafahamu mchango wa watu kama Abdulwahid Sykes, Christopher Kassanga Tumbo, Hanga, Mshume Kiate. Hawa na wenzao walitoa mchango mkubwa hadi nchi kuwepo hapa ilipo leo.

Ninaweza kumsamehe mwananchi wa kawaida akishindwa kujua mchango wa baadhi ya watu kwenye siasa za nchi yetu. Lakini nitaendelea kushangazwa na kiongozi wa siasa asiyetaka kuonyesha thamani au mchango wa mtu kwa kuwa tu amemuudhi.

Ndipo inapaokuja ile methali ya “Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.”

<p> 0718 81 48 75</p>
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: