Mongella amwingiza Pinda mkenge


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 30 June 2009

Printer-friendly version
Aliyekuwa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), Gertrude Mongella

VYOMBO vya habari vya Kusini mwa Afrika vitamshangaa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa kumtetea aliyekuwa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), Gertrude Mongella, ambaye alilazimishwa kujiuzulu nafasi hiyo.

Mongella aliondolewa katika nafasi hiyo kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka, ufujaji wa fedha za PAP, ajira za upendeleo na utendaji mbovu.

Lakini Pinda alisema bungeni wiki iliyopita kuwa Mongella hakujiuzulu bali muda wake ulikwisha katika bunge hilo.

MwanaHALISI linazo taarifa za uhakika kuwa ilikuwa mbindembinde na mshikemshike kufikia kumwamuru Mongella kuitisha kikao cha uchaguzi na yeye kung’olewa.

Pinda alisema kuwa alizungumza na Mongella, ambaye pia ni mbunge wa Ukerewe, mkoani Mwanza aliyemweleza kuwa hakufukuzwa urais wa PAP.

“Inaonekana Pinda alichukulia mambo kijuujuu; hakufanya utafiti na kujua kuwa Mongella alilazimishwa kujiuzulu,” kimeeleza chanzo cha taarifa hizi.

Televisheni za Afrika Kusini na Namibia, na nyingine za baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika, zilikuwa zikionyesha majadiliano ya PAP moja kwa moja, hadi pale Mongella alipoamuru wanahabari wasiruhusiwe kuhudhuria, kimeeleza chanzo cha habari.

Hatua ya Pinda kumtetea Mongella, kuwa alimaza muda wake, imewashangaza wafuatialiaji wa Umoja wa Afrika (AU).

Viongozi wa Afrika wanaelewa vema kuwa kabla Mongella kung’olewa PAP, hakukuwa na ukomo wa urais.

Hata hivyo, Mongella analaumiwa, pamoja na mambo mengine, kutoshughulikia suala la ukomo wa urais na ule wa maofisa wengine, tangu alipoingia madarakani.

Kwa hiyo, utetezi wa Pinda, alioufanya wiki iliyopita Bungeni, Dodoma, unaweka pabaya heshima yake, kwa kuwa taswira ya Mongella katika PAP imeharibika.

Mjadala wa kumuondoa Mongella ulionekana duniani kote kutokana na kuonyeshwa moja kwa moja na vyombo vya habari vya Afrika Kusini na Namibia.

“Pinda alipaswa kufahamu kuwa tangu kuasisiwa Bunge la Afrika, 18 Machi 2004, katiba ya PAP haikuwa na ukomo wa urais, na kwa hiyo Mongella kama asingetuhumiwa, alikuwa na nafasi ya kuendelea,” zimeeleza taarifa za PAP.

Aidha, Pinda hakuwa na taarifa kuwa hata wakuu wa nchi za Afrika, katika kikao chao cha Januari mwaka huu, walikuwa wameamuru uchaguzi wa rais wa PAP ufanywe haraka.

Wakuu hao walikuwa wamekubaliana na tuhuma nyingi alizokuwa amebebeshwa Mongella kuhusu utendaji mbovu, upendeleo, matumizi mabaya ya fedha na kushindwa kuweka taratibu za kupokezana uongozi.

0
No votes yet