Mongella atimuliwa urais PAP


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 09 June 2009

Printer-friendly version
BALOZI Getrude  Mongella

BALOZI Getrude Mongella, Rais wa kwanza wa Bunge la Afrika (PAP) amelazimika kujiuzulu kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha na ajira za upendeleo katika ofisi hiyo.

Hatua ya kulazimishwa kuachia ngazi imekuja baada ya mlolongo wa malalamiko kutoka kwa wabunge wa PAP kutokuridhika na mwenendo wa matumizi ya fedha na uendeshaji wa ofisi hizo.

Nafasi yake imechukuliwa na Dk. Idriss Ndele Moussa, Mbunge kutoka Chad, katika uchaguzi uliofanywa na bunge hilo 28 Mei mwaka huu. PAP ina makao makuu katika mji wa Midrand, nchini Afrika Kusini.

Dk. Ndele aliibuka mshindi baada ya kuwashinda wagombea wenzake wawili;   Lassane Sawadogo, mbunge kutoka Burkina Faso na Mustafa El Gendy, kutoka Misri.

Dk. Ndele aliapishwa na Dk. Mongella kuchukua wadhifa huo mpya, akiwa na kazi ya kufanya mabadiliko makubwa ya uongozi na utendaji wa PAP, kutokana na maagizo ya wabunge ya 19 Mei, mwaka huu huko Midrand.

Bunge la Afrika pia lilichagua makamu wanne wa rais ambao ni Bethel Amadi (Nigeria), anayewakilisha Kanda ya Afrika Magharibi na Mary Mugyenyi (Uganda) anayewakilisha Afrika Mashariki.

Wengine ni Laroussi Hammi (Algeria) anayewakilisha kanda ya Kaskazini, na Joram Gumbo (Zimbabwe) anayewakilisha kanda ya Kusini mwa Afrika.

Mabadiliko yanatokana na kuwapo tuhuma dhidi ya Mongella kuwa chini ya uongozi wake, ajira zilipatikana kwa misingi ya upendeleo na bila kufuata taratibu za ajira wala sifa za watumishi.

Habari zinasema kuwa katika siku za karibuni, kabla ya mabadiliko hayo, Mongella alijaribu kung’ang’ania ili aendelee na wadhifa huo, lakini alishinikizwa kuachia ngazi, jambo ambalo lilikamilika 28 Mei mwaka huu.

Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Dk. Thomas Kashilila, alipoulizwa juzi Jumatatu, alikiri kuwa na taarifa za Mongella kuacha wadhifa huo, ingawa ofisi yake haikuwa na taarifa rasmi kutoka PAP.

“Tumepata taarifa kupitia njia nyingine, lakini hatuna taarifa rasmi kuwa kaacha wadhifa huo,” alisema Dk. Kashilila.

Mwenendo wa Mongella uliishakuwa hoja hadi wakuu wa nchi za Afrika kuunda kamati maalum ya kufanya uchunguzi wa usimamizi na uendeshaji wa PAP.

Taarifa zinasema bunge lilijadili kwa kina taarifa ya kamati hiyo na kujiridhisha kuwa kulikuwa na matumizi mabaya ya fedha.

Katika hatua ambayo haikutarajiwa, inaelezwa kuwa serikali ya Tanzania imekubali kubeba mzigo wa kulipa fedha zote ambazo Mongella alituhumiwa kuzitumia vibaya.

Taarifa zinasema awali, hata baada ya serikali ya Tanzania kuchukua mzigo huo, Mongella alishauriwa ajiuzulu ili kulinda heshima ya Tanzania, lakini aligoma kufanya hivyo.

Wabunge wa Bunge walilalamika kwa viongozi wakuu wa nchi za Afrika juu ya uongozi wake kwa ujumla, ambao wanadai haukuwa na dira wala tija.

“Kuna madai pia kwamba aling’ang’ania kubaki katika nyumba ya Bunge na alipolazimishwa kuondoka akaamua kuhama na fenicha zote za ndani akidai ni zake, jambo ambalo si la kweli,” alisema mbunge mmoja wa Bunge la Afrika kutoka Tanzania ambaye hakupenda kutajwa jina.
 
Aidha, uongozi wa Mongella umelalamikiwa kwa  kushindwa kufanya jambo la maana wakati uliendelea kugharimu rasilimali za nchi za Afrika.

Mjadala wote wa kumuondoa Mongella ulikuwa unaripotiwa moja kwa moja kwenye vyombo vya habari vya Afrika Kusini na Namibia. Kuna wakati Mongella alilazimika kukatisha kikao cha Bunge hilo na kufanya mazungumzo ya faragha na makamu wake wawili.

Baada ya kikao hicho cha siri, Mongella aliamuru waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia kikao waondoke, jambo ambalo lilifanyika.

Naye mbunge mpya wa Tanzania katika PAP, John Cheyo amesema Mongella atakumbukwa kwa kuwa rais wa kwanza wa PAP.

Ni MwanaHALISI iliyowahi kuandika katika toleo Na. 73 la Novemba 28 hadi 4 Desemba 2008, kwamba Mongella alikuwa anatuhumiwa kutenda makosa ya kukosa uaminifu, wizi na utoaji ajira kinyume cha taratibu.

Kuhusu wizi, Mongella anatuhumiwa kutafuna dola za Kimarekani 138,000 sawa na Sh. 180 milioni za Tanzania, mali ya PAP.

Katika tuhuma za utoaji ajira, Mongella anatuhumiwa kuajiri jamaa zake ndani ya  Sekretarieti ya Bunge hilo, kinyume cha taratibu. Tayari Bunge limeagiza kufuta ajira zilizofanywa na Mongella.

0
No votes yet