Moto wa kampeni chafu wawaka Tabora


Hastin Liumba's picture

Na Hastin Liumba - Imechapwa 30 March 2010

Printer-friendly version

MTAFARUKU unanukia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Tabora baina ya wanachama na viongozi. Yamezuka makundi matatu makubwa yanayotishia uhai wa chama hicho.

Kundi la kwanza linajiita ni "kundi la maslahi mbele." La pili linaitwa "CCM halisi (TITANIC)." La tatu lipo kati kati ya makundi yote likiwa linaburuzwa, na linajiita "Kinyonga," kwa maana kwamba linaweza kubadilika wakati wowote.

Kundi la kwanza ndilo linalotumia fedha nyingi kwenye maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. Ni kundi ambalo limesababisha kuwepo kwa uwezekano wa mpasuko na mitafaruku ya kila mara.

Kundi hili mara nyingi limekuwa likitumia fedha kuwapa wajumbe wa mikutano ya halmashauri kuu ili waweze kuwasulubu viongozi wao pale inapotokea kuwepo kwa kikao cha kumaliza tofauti zinazojitokeza kwa maslahi yao.

Kundi hili ambalo linahusisha wabunge na wanachama wanaohitaji uongozi (hasa ubunge na udiwani), linafanya vikao usiku.

Mara nyingi hutumia baadhi ya hotel za hapa mjini kufanikisha malengo yao, na lilikuwa linamuunga mkono mwenyekiti aliyeshinda uchaguzi wa chama hicho, Hassan Mohammed Wakasuvi.

Aidha, kundi hili limekwenda mbali zaidi kwa kuwahusisha hata baadhi ya watendaji wa serikali wa kata, makatibu kata na matawi wa CCM, baadhi yao ambapo hadi sasa uchunguzi umebaini baadhi yao wameingiza pikipiki na baiskeli ili kurahisisha kazi zao kuwania ubunge hapo oktoba mwaka huu.

Kundi la pili ni lile ambalo lilijeruhiwa kwenye uchaguzi wa chama hicho uliofanyika nchi nzima mwaka 2007, ambapo wengi wao wameamua kujiweka pembeni baada ya kushindwa vibaya.

Aidha kundi hili ambalo kwa kiasi kikubwa lilikuwa linamuunga mkono mwenyekiti aliyeangushwa wakati huo, Juma Samweli Nkumba ambapo ni dhahiri hadi sasa bado lina nguvu za ushawishi.

Kundi hili ndilo linalojiita CCM halisi likijipambanua ni kundi ambalo liliweza kusimamia kanuni na taratibu za chama sawasawa na kwamba makundi yaliopo yanasababishwa na kundi maslahi ambalo linalelewa na uongozi wa chama mkoani hapa kwa kuwa lina fedha za kuwapa.

Kundi la tatu ni lile ambalo liko tayari kupokea chochote na kuacha mambo yaende kombo, ilimradi wahusika wamepata chochote. Ni kigeugeu na jepesi kununuliwa na kubadili muelekeo.

Wakati haya yakifanika viongozi wa CCM ngazi ya mkoa na wilaya zake wamekaa kimya huku mambo yakiharibika na wengi wa viongozi hao wamewekewa mazingira mazuri katika baadhi ya hotel kwa kupata mahitaji kwa bili.

Mkoa wa Tabora una wilaya sita. Wilaya ambazo zina tuhuma nzito za viongozi kujihusisha na wanachama na baadhi ya wabunge wanaotaka ubunge ni Uyui, Tabora Mjini na Urambo.

Tabora Kaskazini, Urambo Mashariki, Igalula na Tabora Mjini yanadaiwa kuongoza kwa hujuma.

Wakati hayo yakifanyika katika majimbo hayo majimbo ya Urambo Magharibi, Igunga, Sikonge, Nzega na Bukene nayo hayako shwari. Hata hivyo, angalau katika majimbo hayo kuna tofauti kidogo ukilinganisha na majimbo mengine.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: