Mpango kununua Dowans waiva


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 18 March 2009

Printer-friendly version
Waziri wa Nishati na Madini,  William Ngeleja

SERIKALI na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), bado wanaendelea na mazungumzo ya kununua mitambo ya Dowans, MwanaHALISI limegundua.

“Kwa ushahidi uliopo, madai yote ya kujiondoa katika mjadala wa kununua mitambo ya Dowans ni kiini macho; na mjadala mkubwa juu ya ununuzi ndio hasa umepamba moto,” kimeeleza chanzo cha habari.

Taarifa za kuaminika kutoka kwa anayedaiwa kuwa “mmiliki” wa kampuni ya Dowans Holding Tanzania Limited, Jenerali Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), zinasema serikali imemhakikishia kununua mitambo yake.

Katika mahojiano na shirika moja la habari nchini Marekani, KLHN International, Jumapili iliyopita, Bregedia Jenerali Al Adawi amesema, “Bado tunaendelea na mazungumzo na serikali, ili waweze kununua mitambo yetu… Tunaendelea kujadiliana nao katika hilo.”

Mahojiano na Bregedia Jenerali Al Adawi yalifanywa na mwandishi wa habari Mtanzania, M.M. Mwanakijiji anayeishi Dettroite, Marekani. Mahojiano yalitokana na jina la Jenerali huyo kutajwa katika jarida la Africa, toleo la 7 Machi 2009.

MwanaHALISI limepata nakala ya mazungumzo kati ya Bregedia Jenerali Al Adawi na shirika la KLHN.

Kwa mujibu wa mahojiano hayo, majadiliano kati ya serikali na anayejiita mmiliki wa Dowans, yalizidi kupamba moto baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Idris Rashid kutoa kauli ya kujiondoa katika mazungumzo.

Ni kutokana na kauli ya Dk. Rashid na msimamo wa Jenerali Adawi, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alipata nguvu za kutamka hadharani kuwa “hakuna sheria inayozuia ununuzi wa mitambo iliyotumika.”

Waziri aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wiki iliyopita kuwa ana mamlaka ya kuamua kununua mitambo iliyotumika pale mazingira ya kufanya hivyo yatakaporuhusu.

Tayari mazingira ya kusababisha ununuzi wa mitambo ya Dowans iliyotumika yamejengwa.

Dk. Rashid amesema kwa kuwa umezuka mzozo kuhusu ununuzi wa mitambo ya Dowans, basi Tanesco isilaumiwe iwapo nchi itaingia gizani. Hii imetafsiriwa kuwa uwezekano wa Tanesco kuingiza nchi gizani ili mitambo hiyo inunuliwe.

Aidha, tamko la waziri Ngeleja kuwa ana uwezo wa kuamuru ununuzi wa mitambo iliyotumika, unaongeza nguvu juu ya mpango na makubaliano kinyemela ya kununua mitambo hiyo.

Shirika hilo la habari linasema, “Wenye Dowans hawajakubali kushindwa. Watafanya lolote mpaka mitambo inanunuliwa.”

Lakini Waziri Ngeleja alipoulizwa msimamo wa serikali, juzi Jumatatu alisema, “Haiwezekani. Hizo ni fitina. Mimi ndiye msimamizi wa utekelezaji wa sera za serikali. Hakuna kitu kama hicho.” Alimwambia mwandishi kuwa yuko  kwenye kikao, aitwe baadaye. Hakupatikana.

Hata hivyo, bado utata umeighubika Dowans. Anayeitwa mmiliki, Jenerali Al Adawi, awali alikanusha kuwa mmiliki.

Alipobanwa akamtaka Mwanakijiji kusoma katika tovuti ya makampuni yake yenye anwani: http://www.stcgroups.com ili kujiridhisha kwamba Dowans siyo moja ya makampuni anayomiliki.

Al Adawi alisisitiza kuwa makampuni yake hayajishughulishi na mambo ya nishati bali ujenzi na kwamba Dowans siyo kampuni ya ujenzi.

Alisema iwapo kuna kampuni inatajwa kuwa yake wakati hajawekeza humo hata shilingi, basi angefurahi sana kupewa “kwa dezo” kampuni ya namna hiyo.

Hii ilikuwa na maana kuwa Jenerali Al Adawi haifahamu Dowans na wala hajawekeza katika kampuni hiyo.

Lakini kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali za kampuni ya Dowans zilizopo kwa Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA),  zinaonyesha Bregedia Jenerali Al Adawi kuwa mmoja wa wakurugenzi.

Anuani iliyotumika katika fomu hiyo ni P.O.Box 823, PC 112, Sultanate of Oman. Anuani hiyo ndiyo inayotumiwa na kampuni ya Services and Trade ya Oman ambayo Bregedia Jenerali Al Adawi alianzisha na mshirika wake mwingine mwaka 1977.

Al Adawi alipoulizwa uhusiano wake na mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, au uhusiano wa Rostam na Dowans, alikiri kumfahamu Rostam na kusema kuwa ni “rafiki” yake.

Alipoulizwa juu ya uhusiano wa Rostam na kampuni yake ya Dowans, na iwapo Rostam alimfuata na kumshawishi amsaidie kuanzisha kampuni ya Dowans, aling’aka, “Muulize mwenyewe; mbona unaniuliza maswali kama vile nahojiwa na polisi?”

Kwa mujibu wa Mwanakijiji, Jenerali Al Adawi ni mzaliwa wa Zanzibar ambaye alimwonya kuwa si vizuri kwa vyombo vya habari “kuandika vitu ambavyo hawana uhakika navyo.” Alimtaka Mwanakijiji kuwasiliana na wanasheria kwa taarifa zaidi.

Bali Al Adawi alipogundua kuwa Mwanakijiji ni Mtanzania na anafuatilia mambo ya kashfa za nishati zinazoendelea nchini na jinsi gani kampuni ya Dowans inaonekana katikati ya sakata hilo, alianza kuongea kwa sauti ya kunyong’onyea na kujibu kama vile anajitetea mahakamani.

Huyo ndiye Al Adawi, mwenye sura nyingi: Anajitambulisha kuwa mmiliki wa Dowans; huku anakana kuifahamu Dowans na kusema hajawahi kuwekeza katika kampuni yenye jina hilo.

Al Adawi anakataa kuhusishwa na Dowans na kusema hahusiki na makampuni ya nishati ya umme, huku anaonekana katika nyaraka za kuanzisha Dowans inayofua umeme Dar es Salaam; anakana kumfahamu Rostam Aziz na baadaye anakiri kuwa ni rafiki yake.

Imefahamika kuwa mfanyabiashara huyo anamiliki nyumba kadhaa nchini Tanzania na kwamba huja mara kwa mara kutokana na familia yake kuwapo hapa.

Al Adawi kama Rostam Aziz.  Ni Rostam aliyewahi kusema haifahamu Dowans; baadaye akasema walikuwa wakitumia ofisi zake za kampuni ya Caspian; siku zilipopita akasema kampuni yake iliomba kazi kwa Dowans; hatimaye akasema anafahamu wamiliki wa Dowans.

Toleo la Jumatano iliyopita la MwanaHALISI lilimtaja Rostam kuwa mtu muhimu katika uchunguzi wa sakata la Kagoda Agriculture Limited na Dowans lakini serikali ilikuwa haijaonyesha kumtumia.

Wachunguzi wa mambo wanasema kama Al Adawi na Rostam wana ukaribu hata wa tabia, bila shaka kuna uhusiano wa kuaminika miongoni mwa watu hao wawili, Dowans na baadhi ya viongozi serikalini ambao wamekuwa king’ang’anizi kuhusu ununuzi wa mitambo ya Dowans.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini utata ulioghubika uanzishaji wa Dowans. Kwa muda mrefu kumekuwa kukitajwa karibu makampuni manne ya Dowans ambayo yanahusiana na Dowans Tanzania Limited, lakini ukweli ni kuwa kampuni hizo ziko mbili tu.

Awali ilitajwa Dowans Holdings ya Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu. Taarifa zinasema katika falme hizo hakuna kampuni yenye jina hilo.

Taasisi ya Uwekezaji ya Dubai, Wizara ya Uchumi na Biashara ya falme za Kiarabu ambayo hutoa leseni za biashara na Idara ya Kanda Huru za Falme za Kiarabu inayohusika na uwekezaji, vyote vimethibitisha kuwa hakuna rekodi zozote za Dowans.

Vilevile imekuwa ikitajwa kampuni ya Dowans Holdings ya Afrika Kusini. Uchunguzi unaonesha kuwa kuna mtu alichanganya maneno “SA” yanayoonekana kwenye kampuni ya Dowans Holdings SA akifikiri yanamaanisha kuwa ni “South Africa.”  

Nchini Afrika Kusini hakuna kampuni yenye jina kama hilo ambayo inahusiana na Dowans Tanzania Limited; herufi “SA” zinasimama badala ya maneno ya Kiihispania “Sociedad Anónima” ambayo ni sawa na hadhi ya “shirika” katika Tanzania.

Kampuni pekee ya Dowans ambayo inaonekana kuhusiana na Dowans Tanzania Limited ni ile ya Costa Rica ambayo imethibitika kuwa ni kampuni hewa na huku wamiliki wake wakiwa hawafahamiki.

Sheria za uwekezaji nchini Costa Rica zinaruhusu watu kufungua makampuni feki na zinalinda wawekezaji hao kutokujulikana.

Kwenye orodha ya wanaohusishwa na Dowans ni Kampuni ya Portek International ya Indonesia, kupitia kampuni yake tanzu ya Portek Systems and Equipment Ltd., inayodaiwa kuwa na hisa ya asilimia 39.

Bali gazeti hili limegundua kwa mwaka 2007 na 2008 kampuni hiyo ya Indonesia haikuwa na hisa yoyote kwenye Dowans Tanzania Limited wala haikuonesha kuwa wanaitambua kwa namna yoyote ile.

Kwa upande wa Afrika kampuni hiyo ya Portek Systems and Equipment ilikuwa inafanya kazi nchini Algeria kupitia kampuni ya Bejaia Mediterranean Terminals S.p.a. Portek, na kwamba ina asilimia 15 ya hisa kwenye kampuni moja tu ya kigeni nayo iko Phillipines.

Katika nyaraka za awali zilizowasilishwa bungeni na Kamati Teule ya Bunge, ilibainika kwamba Richmond ilikwenda kutafuta mwekezaji Afrika Kusini ambaye ingemuuzia mkataba wake wa kufua umeme.

Hivyo suala linalotajwa sasa la mkataba kuuzwa kwa kampuni ya Dowans ya Oman limeanza kusikika hivi majuzi baada ya upinzani wa asasi za kijamii, watu mashuhuri nchini, wabunge na wanasheria kupinga serikali kununua mitambo ya Dowans.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: