Mpango wa CCM ‘kuua’ CUF waelekea kufanikiwa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 04 January 2012

Printer-friendly version
Gumzo

KIKAO cha dharura cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama cha Wananchi (CUF), kimeitishwa mjini Zanzibar leo (4 Junuari 2012) ili kubariki “mradi” wa kumvua uanachama mbunge wa Wawi kisiwani Pemba, Hamad Rashid Mohammed.

Kisa: Ni tuhuma kwamba Hamad Rashid anaendesha kampeni za kutaka Maalim Seif Shariff Hamad ang’olewe kwenye nafasi ya katibu mkuu.

Kuitishwa kwa kikao hicho cha baraza kuu la uongozi la taifa (BKUT), kumefuatia kumalizika kwa mkutano wa siku mbili wa Kamati ya Utekelezaji (KUT), uliofanyika 30 na 31 Desemba 2011 mjini Zanzibar.

Hamad anatuhumiwa kueneza taarifa kuwa tangu Maalim Seif ateuliwe kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), chama kimedhoofika hasa Tanzania Bara ambako kwa sasa CUF “kinaonekana kama tawi la Chama Cha Mapinduzi (CCM).”

Aidha, Hamad anadaiwa kufadhili viongozi 13 wa chama hicho, “kuzunguka wilaya zote nchini bila kujulisha mamlaka za chama zilizowekwa kikatiba; kuhamasisha wanachama wake kukihama chama chao; kufanya kampeni dhidi ya viongozi wakuu wa chama na kuwazushia viongozi wake madai ya uwongo.”

Miongoni mwa yanayodaiwa kuelezwa mikoani ni taarifa kuwa Maalim Seif hana muda wa kutekeleza majukumu ya chama, ikiwamo udhibiti wa fedha za chama. Wanatuhumiwa kusema kwenye uchaguzi mdogo wa Igunga, CUF ilitumia zaidi ya Sh. 400 milioni; fedha zilizotumika hazilingani na kilichopatikana.

Wanatuhumiwa kueneza taarifa kuwa ni Maalim Seif aliyezuia maandamano ya kupeleka rasimu ya katiba kwa waziri wa sheria na katiba; na kwamba ni yeye aliyezuia kufanyika kwa maandamano yao ya kupinga unyanyasaji unaofanywa na vyombo vya dola kwa wabunge wa upinzani.

Wamekuwa wakitoa mfano wa kukamatwa na kusekwa gerezani kwa siku kadhaa Magdalena Sakaya, mbunge wa chama hicho mkoa wa Tabora na viongozi wenzake waandamizi waliokuwa mkoani humo kwa shunghuli za chama.

 Madai mengine ni kwamba ni Maalim aliyewalazimisha “wabunge wake” waunge mkono muswaada wa kuundwa kwa katiba mpya. Wanadaiwa kusema kuwa Maalim alifanya yote hayo baada ya kushinikizwa na CCM na serikali yake ambayo yeye ni mmoja wa watumishi wake.

Wanaodaiwa kufadhiliwa na Hamad na kuzunguka nchi mzima, ni pamoja na wajumbe wa baraza kuu la taifa – mbunge wa zamani wa Micheweni Pemba, Shoka Khamisi Juma, Doyo Khassani Doyo na Amir Kirungi.

Wengine, ni Juma Said Saanani, Yasin Mrotwa, Mohamed Albadawi, Doni Waziri, Mohamed Masaga, Yusuf Mungiro, Ahmed Issa, Tamim Omar, Ayub Kimangale na Haji Nanjase.

Mkutano wa KUT uliofanyika chini ya uenyekiti wa Maalim Seif unadai umejiridhisha na kile ulichoita “ukweli wa tuhuma dhidi ya Hamad na wenzake 13.” Umependekeza kwa baraza kuu kuchukua hatua stahiki, kamvua Hamad uanachama na wengine kupewa onyo.

Kwa hiyo, kikao cha baraza kuu kilichoitishwa, hakiendi kujadili tuhuma zilizotolewa na Hamad na wenzake juu ya hatua ya Maalim Seif kukabidhi chama kwa Ismail Jussa Ladhu, naibu katibu mkuu Zanzibar, ambaye baadhi ya wenzake ndani ya chama hicho wanamtuhumu kuitumia CUF kwa “maslahi binafsi.”

Wala baraza kuu halikuitishwa kujadili madai ya kudhoofika kwa chama, hasa Tanzania Bara. Halikuitwa kujadili madai kuwa Maalim Seif amekaa sana kwenye nafasi hiyo “kama kiongozi wa kiroho” na hivyo kusababisha chama kukosa mvuto.

Baraza halitajadili tuhuma za CUF kuitwa CCM B. Halitajadili tuhuma juu ya Maalim Seif na Jussa kukitambulisha chama chao zaidi na CCM kuliko upinzani.”

Bali baraza kuu lililoitishwa linakwenda kufanya kazi moja ya kumfukuza Hamad Rashid kwenye chama na kutoa onyo kwa wenzake 13 waliopachikwa jina la “waasi ndani ya chama.”

Lakini kama Maalim Seif angekuwa mkweli wa kukitazama chama chake kilipo sasa na kinakoelekea; kama angekuwa bado anaamini alichokuwa anakisimamia kipindi kile cha vuguvugu la kuanzishwa kwa mageuzi, hakika angelitazama jambo hili kwa jicho la nyongeza.

Maalim angeangalia kwanza iwapo kuna ukweli katika madai ya Hamad na wenzake. Angeangalia kama yanakidhi matakwa ya kikatiba. Angeangalia pia kama yanagusa hisia za wanachama wengi.

Kama Maalim Seif angejipa muda na kuangalia hayo, haraka angebaini kuwa CUF ya sasa ni tofauti na ile ya miaka sita iliyopita. Hii imedhoofika. Imepoteza mvuto. Imeacha kutetea wanyonge na kusimama kwenye ukweli.

CUF ya sasa, si tena chama cha ushindani, hasa Tanzania Bara. Katika baadhi ya maeneo, wanachama wake wameanza kukichongea jeneza. Viongozi wake wakuu kama vile, Julius Mtatiro, naibu katibu mkuu Bara, anadaiwa kushirikiana na polisi kubambikiza tuhuma wanachama na wafuasi wao.

Wengine akiwamo Maalim Seif mwenyewe, wamekuwa wakiimwagia sifa serikali iliyopo madarakani. Wanasifia utendaji wake, vyombo vyake vya ulinzi na wakati mwingine sera zake na mipango yake.

Kwa mfano, kuna wakati Maalim Seif amenukuliwa akituhumu wanaobeza maendeleo aliyodai yamepatikana katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru wa taifa hili. Alitaka wote wanaobeza maendeleo hayo “walaaniwe na umma.”

Kauli za aina hii, ilikuwa ni mwiko kutolewa na kiongozi wa kimapinduzi aina ya Maalim Seif. Zilikuwa zikitolewa na viongozi wa CCM, tena wakiwa kwenye mikutano ya hadhara. Hawakuweza kusema haya wakiwa kwenye mikutano yao ya ndani ya chama.

Maalim Seif angeangalia kama ni kweli madai kuwa ameshindwa kutenganisha wadhifa wake wa ukatibu mkuu na shughuli za serikali anakotumikia. Kama ni kweli kazi ya umakamu wa rais imemfanya kuwa bize, basi hatua yake hiyo, imechangia kudhoofisha chama chake.

Kama angeliangalia hilo, hakuna shaka angebaini hatua yake ya kuwamo serikalini inavyomlazimisha kutetea kila linalofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Kwa mfano, hatua ya Maalim Seif kuwamo serikalini na huku akiwa ndiye mtendaji mkuu wa chama cha upinzani chenye ubia, imesababishia CUF kushindwa kukemea serikali kwa uzembe wa kuiruhusu kuondoka bandarini meli ya mv. Spice Islander iliyozama kwenye mwambao wa Nugwi, kisiwani Unguja, wakati tayari ilikuwa imesheheni abiria na mizigo.

CUF imeshindwa kukemea serikali kwa kutopeleka mapema vifaa vya uokoaji; kushindwa kuokoa watu zaidi ya 3,000 waliokuwamo kwenye meli hiyo na hivyo kusababisha vifo vyao na kushindwa kufika kwa haraka vyombo vya uokoaji kwenye eneo la ajali.

Kabla ya kutekeleza mradi wake huu wa kuwafukuza wenzake kwenye chama, Maalim angejipa muda wa kutafakari kwa makini taarifa zilizotolewa na idara ya usalama ya chama chake. Angeangalia iwapo zina ukweli au ni majungu.

 Angalia mfano huu: Idara ya usalama imepeleka kwenye kamati ya utendaji, lundo la tuhuma kwamba Hamad Rashid na wenzake wanatumiwa na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ili kuidhoofisha CUF.

Taarifa zinasema, “Hamad Rashid amekubaliana na Lowassa” iwapo atafanikiwa (yeye Hamad) kushika uongozi wa CUF, “Lowassa atajiunga na chama hicho na kisha atagombea urais.” Hamad atakuwa mgombea mwenza. Wanasema mradi wote huo, unafadhiliwa kwa asilimia 100 na Lowassa mwenyewe.

Lakini katika eneo jingine, idara ya usalama ya CUF inasema, “Hamad Rashid hana hata shilingi.” Anaendesha operesheni yote hiyo kwa njia ya mkopo. Anakopa huku na kurejesha kule. Anarejesha huku na kukopa kule.

Idara inasema Hamad amejaribu kutaka kukopa kwa mfadhili mmoja, lakini wao wamefanikiwa kumzuia kwa kuweka fitna. Akaenda kwa mtu wa pili ambako nako alikwama. Akaenda kwenye Benki ya Exim ambako wamefanikiwa pia kujipenyeza na kuzuia mkopo wake.

Katika nyaraka hiyohiyo, idara ya usalama ya CUF inasema, “Hamad Rashid na kundi lake wana fedha nyingi za kufanya kazi hiyo. Je, wamezipata wapi, wakati wanasema Hamad hana fedha na hivyo ni ombaomba?

Hamad anayedaiwa kufadhiliwa na Lowassa kwa asilimia 100, kwa nini amekuwa ombaomba ghafla? Kwa nini aendeshe operesheni yake hiyo ya kutafuta ukatibu mkuu kwa njia ya mikopo?

Kwa nini amejiingiza kwenye mikopo ambayo anajua ina masharti magumu na riba kubwa? Kipi kinachomfanya ajiweke rehani kiasi hicho, wakati Lowassa anaweza kutoa kiasi chote cha fedha kinachohitajika?

Ni idara hiyohiyo ya usalama ya chama inayosema, tena kwenye waraka wake uleule, “Nyuma ya Hamad Rashid yuko Waziri Mkuu Mizengo Pinda.” Inasema kila kinachofanyika sasa kinalipiwa na Pinda.

 Pengine inasema, Hamad Rashid anataka kugombea urais wa Zanzibar mwaka 2015; amepiga hesabu zake vizuri na kuona hawezi kufika hapo, bila kwanza kuwa katibu mkuu wa chama chake.

Je, wanachama washike lipi hapa? Waamini Hamad Rashid anataka kugombea urais wa Zanzibar au anataka kuwa mgombea mwenza wa Lowassa? Waamini Hamad Rashid hana fedha, au amekusanya fedha nyingi kutoka kwa Lowassa? Waamini Hamad Rashid anafadhiliwa na Lowassa au anafadhiliwa na waziri mkuu Pinda?

Mbona idara ya usalama ya CUF haisemi uhusiano wa Pinda na Lowassa katika hili? Makubaliano yao ni yapi? Je, Lowassa anataka urais kupitia CUF na Hamad anataka kuwa makamu wake? Je, Pinda anataka nini? Wamekubaliana nini na Hamad? Je, Pinda hataki urais?

Inawezekana Hamad Rashid akawa na ajenda yake katika mbio zake za kutafuta ukatibu mkuu wa chama chake. Lakini kwa vyovyote vile, Maalim Seif hapaswi kutekeleza mradi wake wa kumfukuza Hamad Rashid na wenzake kwa kutumia taarifa hii ya idara ya usalama ambayo tayari imethibitika kuwa na matundu.

Je, hatua ya Maalim Seif itakiokoa chama, kukijeruhi au kukiua kabisa? Tusubiri.

0
Your rating: None Average: 2 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: