Mpango wa Kikwete, Karume wakamilika


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 07 July 2010

Printer-friendly version
Ni wa kumpa urais Dk. Shein Zanzibar
Bilal kutegemea fadhila za rais mpya
Rais Jakaya Kikwete na Rais Amani Karume

MKAKATI wa marais Jakaya Kikwete na Amani Karume wa kumfanya Dk. Ali Mohammed Shein kuwa rais wa Zanzibar, sasa umekamilika.

“Kwa kadri kikao cha Kamati Maalum ya NEC Zanzibar kilivyochuja majina ya wanaoomba urais Zanzibar, hakuna anayeweza kumpiku Dk. Shein,” kimeeleza chanzo cha habari.

Hivi sasa Dk. Shein ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Taarifa zinasema hatua inayofuata ni kupeleka jina moja tu la mgombea kwenye NEC.

Taarifa kutoka ikulu Dar es Salaam, Zanzibar na makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma, zinasema mkakati wa kumfanya Dk. Shein kuwa mgombea urais wa Visiwani tayari umekamilika.

Mwishoni mwa wiki Dk. Shein alipitishwa kuwa mmoja wa wanachama wa CCM wanaopigania kugombea urais kupitia chama hicho.

Wengine wanne ambao Kamati Maalum iliona wana sifa za juu, ni Shamsi Vuai Nahodha, Ali Juma Shamhuna, Dk. Mohammed Gharib Bilal na Haroun Ali Suleiman.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhani Ferouz amesema majina yote 11 ya walioomba, yatawasilishwa kwenye Kamati Kuu ili ishuhudie uchambuzi wa waombaji.

Maoni ya Kamati Maalum ambayo yameelezwa kumpa Dk. Shein nafasi ya juu, yanasemekana kuwa ni sehemu ya maelekezo ya marais wa Jamhuri na Zanzibar katika kutekeleza mkakati wa kilichoitwa “kumaliza misuguano na makundi Zanzibar.”

Wakati Rais Kikwete ameelezwa kuwa anataka kujivua “migogoro ya Zanzibar,” Rais Karume anajulikana kuwa amekuwa akitaka mgombea anayeweza kuendeleza maridhiano katika siasa za Zanzibar.

Rais Karume ndiye mwanzilishi wa siasa za mapatano ndani ya CCM kwa kukubali kukutana na kiongozi mkuu wa upinzani Zanzibar, Seif Shariff Hamad kutafuta maridhiano ya kudumu.

Makubaliano kati ya rais na katibu mkuu huyo wa Chama cha Wananchi (CUF), ndiyo yalifikisha Zanzibar kwenye hatua ya kutunga sheria ya kuwezeshwa kuundwa serikali ya kitaifa baada ya kura ya maoni mwishoni mwa mwezi huu.

Ni Rais Karume ambaye aliripotiwa katika miezi ya karibuni akisema, “…kwani rais akitoka kisiwa cha Pemba itakuwa nini?” Alikuwa akikabiliana na wapinzani wa mpango wake wa siasa za maridhiano.

Mabadiliko yatakayotokea kwa njia hii yatarasimishwa katika katiba ya Zanzibar na baadaye katiba ya Muungano.

Hatua hizi za marais wawili kujitua mzigo wa kile Rais Kikwete alichoita “mpasuko wa Zanzibar,” ndiyo imesababisha uteuzi wa Dk. Shein anayechukuliwa kuwa pekee miongoni mwa waomba urais CCM anayeweza kusimamia mabadiliko hayo.

Katika kufanikisha ushindi wa Dk. Shein, Rais Karume anaelezwa kuwa tayari amefanya majadiliano na wajumbe kadhaa wa Halmashauri Kuu ya Taifa kwa lengo la kutaka msimamo wao na Kikwete uungwe mkono.

“Ni kweli, tumekutana na Rais Karume. Mheshimiwa huyu hakuficha hisia zake. Amesema wazi, kwamba chaguo lake ni Dk. Shein,” ameeleza kiongozi mmoja wa serikali ya Zanzibar, akinukuu baadhi ya wajumbe wa NEC waliokutana na Rais Karume.

Amesema, “Rais alifika mbali zaidi. Kwanza, alisema mgombea anayemtaka Zanzibar ni yule ambaye atakuwa tayari kuendeleza yale ambayo yeye ameyaanzisha na kuyatekeleza.”

Mtoa taarifa anamnukuu Rais Karume akisema angependa kuacha madaraka mikononi mwa kiongozi ambaye “…atasimamia kwa dhati” misingi ya umoja, maelewano, na “…suala zima la serikali ya umoja wa kitaifa.”

Wajumbe wanaotajwa kufikiwa kwa ushawishi wa rais wa Zanzibar, ni pamoja na waandamizi ndani ya chama hicho katika ukanda wa Ziwa Victoria, Morogoro, Kanda ya Magharibi, Pwani na Kusini.

Mkakati wa kumwingiza Dk. Shein ikulu ya Zanzibar, kwa upande wa Bara, unaratibiwa kwa kiwango kikubwa na waziri mmoja mwandamizi katika serikali ya Rais Kikwete.

Taarifa zinanukuu vyanzo mbalimbali vya ikulu vikisema, msingi mkuu wa Rais Karume kumuunga mkono Shein unatokana na hoja kubwa mbili:

Kwanza, Rais Karume asingependa kurithisha utawala kwa kikundi cha washindani wake ndani ya chama ambao kesho watakuja kuibuka na kusema, “Sisi tumeshinda.”

Hata hivyo, wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, inawezekana mlengwa wa kauli hiyo, akawa ni Dk. Bilal.

Pili, Rais Karume angependa zaidi kuacha madaraka mikononi mwa kiongozi ambaye atasimamia kwa dhati kulinda Muungano ulioasisiwa na baba yake, rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Hata hivyo, taarifa zisizorasmi zinasema huenda Dk. Shein ameingia katika kinyang’anyiro hicho ili aje kujiondoa baadaye na kumwachia mwingine ili kuepusha madai na misuguano kutoka kwa watarajiwa wakuu.

Yule ambaye anatajwa kuwa anaweza kuachiwa ni Shamsi, ingawa uvumi mkuu ni kwamba Dk. Shein asingeingia mbio hizo kama asingekuwa amehakikishiwa kulindwa, kutetewa na kubebwa hadi ikulu ya Zanzibar.

Wakati hayo yakiendelea, taarifa zinasema zogo kubwa liliibuka ndani ya kikao cha Kamati Maalum ya Zanzibar, baada ya wajumbe kushinikiza mwenyekiti wa kikao, Rais Karume, kuacha kutoa alama kwa wagombea na badala yake wapimwe kwa sifa na vigezo.

“Mle ndani ya mkutano, zogo kubwa liliibuka pale wapambe wa Dk. Bilal waliposhinikiza kikao kutotoa alama kwa wagombea. Mwenyekiti alilazimika kubadilisha utaratibu,” amesema mjumbe wa NEC aliyehudhuria mkutano huo.

Amesema baada ya Rais Karume kuona zogo limekuwa kubwa, alitafuta utaratibu mwingine wa kuchuja wagombea. “Mwenyekiti aliagiza tubadilishe utaratibu kwa kuangalia sifa 13 zilizowekwa na chama bila kuweka alama,” amesema.

Ni katika hatua hiyo wanachama sita kati ya 11 walioomba uteuzi walijikuta wakiondolewa kwa kukosa sifa. Walioenguliwa ni pamoja na Mohamed Raza, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Ali Karume, Omari Sheha, Hamad Mshindo, Mohammed Yusuf Mshamba na Mohammed Aboud Mohammed aliyewekwa kiporo kusubiri maelezo ya nyongeza.

Taarifa zinasema baada ya kuondolewa kwa wagombea hao, Kamati Maalum ikajikita katika kuangalia wagombea ambao hawakuwa na chembe ya mashaka.

“Hapa ndipo walipopatikana wagombea wanne huku Dk. Bilal akiachwa nje,” anasema mtoa taarifa wetu.

Wagombea waliopitishwa baada ya mchujo, ni Dk. Shein, Vuai, Shamhuna na Haroun.

“Baada ya wagombea hao wanne kupatikana, ndipo ilipoamriwa kuongezwa jina la Dk. Bilal, ili kama kuna kasoro za msingi, suala lake likajadiliwe na vikao vya juu vya chama,” imeelezwa.

“Nakuambia, ni busara tu zilizomvusha hapo Dk. Bilal. Alikuwa na sifa za chini lakini wazee wakasema ni muhimu kupeleka jina lake Dodoma ili kama kukatwa au kurejeshwa, ijulikane huko,” ameeleza mtoa taarifa.

Amesema awali Dk. Bilal alitakiwa kutoa ufafanuzi wa kile mtoa hoja aliita, “Dk. Bilal na kauli tata.” Mtoa hoja anayetajwa kumweka “kiti moto” Bilal ni Salum Msabah Mbarouk, mwanachama na kiongozi wa zamani wa CUF ambaye sasa ni mjumbe wa NEC kupitia Zanzibar.

Msabah anadaiwa kumtaka Dk. Bilal kueleza maana halisi ya kauli yake, “Sitalipiza kisasi, ingawa kisasi ni haki” aliyoitoa wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari mara tu baada ya kuchukua fomu ya kuomba uteuzi.

Aidha, Msabah alimtaka Dk. Bilal kueleza kwa nini alikiuka maadili ya chama katika kipindi cha kuchukua na kurejesha fomu.

Inadaiwa kwamba Msabah alieleza wajumbe wa kikao kwamba mara baada ya Dk. Bilal kurejesha fomu alikwenda moja kwa moja maskani maarufu ya Kisonge, Michenzani mjini Zanzibar ambako alihutubia mamia ya wafuasi wake; jambo ambalo lilikatazwa na chama chake.

Dk. Bilal alikuwa waziri kiongozi katika kipindi cha pili cha urais wa Dk. Salmin Amour (1995-2000).

Ameomba kugombea urais Zanzibar mara mbili ikiwemo 2005 alipolazimishwa kuondoa jina lake ili kumpisha Rais Karume kumalizia kipindi cha pili cha miaka mitano ya uongozi wake.

Huyu ni mtaalam wa sayansi ya nyuklia. Aliibukia kwenye siasa baada ya kuwa katibu mkuu wizara ya elimu ya juu, sayansi na teknolojia katika serikali ya Rais Benjamin Mkapa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: