Mpango wa kumfukuza Sitta waiva


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 03 February 2010

Printer-friendly version
Spika wa Bunge Samwel Sitta

KUMEKUCHA. Juhudi za kumfukuza Spika wa Bunge Samwel Sitta kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimeanza upya, MwanaHALISI limeelezwa.

Viongozi kadhaa ngazi ya mkoa wanadaiwa kutumwa kushawishi wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho kumfukuza Sitta uanachama wakati wa vikao vya wiki ijayo mjini Dodoma.

Taarifa zinasema mpango wa kumng’oa Sitta ndani ya CCM umeandaliwa na watuhumiwa wa ufisadi ambao wamekuwa wakidai Sitta amekuwa “kisiki cha mpingo” kwa juhudi zao za kujisafisha ndani na nje ya bunge, taarifa zimeeleza.

Njama za kumng’oa Sitta ni za muda mrefu na gazeti hili liliwahi kuchapisha taarifa hizo mara tatu mwaka jana.

Lakini njama zimepamba moto mara baada ya kuvuja, miezi miwili iliyopita, taarifa za Kamati ya rais mstaafu Ali Hassani Mwinyi iliyopewa jukumu la kutafuta kiini cha migogoro kati ya Bunge, wabunge kwa upande mmoja, na serikali.

Katika taarifa yake iliyokabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete, Kamati ya Mwinyi ilipendekeza kuvuliwa nafasi za uongozi katika chama vigogo wanne wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Vigogo hao wametajwa kuwa ni Edward Lowassa, Rostam Aziz, Nazir Karamagi na Andrew Chenge. Hakuna hata mmoja wao aliyepatikana juzi kueleza juu ya kushiriki kwao katika njama za kumng’oa Sitta.

Tarifa zinasema hadi sasa wajumbe wanne wa waandaaji wa mpango wa kumng’oa Sitta tayari wametembelea baadhi ya mikoa na kukutana na wajumbe wa NEC.

Mikoa iliyoripotiwa kutembelewa ni pamoja na Kigoma, Tanga, Lindi, Morogoro, Iringa, Ruvuma na Dar es Salaam..

Taarifa zinasema wajumbe hao waliopachikwa jina la “wapanda fitina,” tayari wamekwenda Zanzibar kwa shughuli hiyohiyo.

Maandalizi hayo yamejengwa kwenye misingi miwili ambayo inadhaniwa itavuta wajumbe wengi wa vikao vya Kamati Kuu (CC) na NEC vinavyotarajiwa kufanyika tarehe 9 hadi 11 mwezi huu mjini Dodoma.

Msingi wa kwanza umejengwa kwenye madai kuwa Sitta amekuwa akiendeleza ukaidi dhidi ya taarifa ya serikali kuhusu kashfa ya Richmond iliyomng’oa Edward Lowassa kwenye nafasi ya waziri mkuu.

Msingi wa pili ni kwamba, Sitta amekaidi ushauri wa mwenyekiti Mwinyi unaomtaka akutane na Lowassa ili “wayamalize.” Hatua hiyo inachukuliwa kuwa ni dharau na kwamba anakitakia mabaya chama chake.

“Ni lazima Sitta ang’oke ndani ya chama. Nakuhakikishia kwamba tunakwenda Dodoma kwa kazi moja tu: Kumfukuza Sitta,” amesema mwenyekiti mmoja wa CCM wa mkoa kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.

Amesema, “Sitta amedhoofisha chama chetu. Amevuruga serikali yetu. Hatuwezi kukubali kuona anabaki katika nafasi yake.”

Septemba mwaka jana, Sitta alipata wakati mgumu kukabiliana na wajumbe wa NEC waliotaka kumfukuza katika chama.

Katibu Mkuu wa CCM Yusuf Makamba alikuwa wa kwanza kumweleza mwenyekiti Kikwete kwamba wajumbe walikuwa na mengi ya kusema na kwamba awaache waseme.

Mtoa taarifa ametaja katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Shaaban Kilumbe Ngenda kuwa ni miongoni mwa viongozi wa chama hicho waliotumwa mikoani. Mwingine ni katibu wa mkoa wa Arusha, Mary Chatanda.

Hata hivyo, Kilumbe amekana kuwa miongoni mwa wajumbe waliotumwa mikoani na watuhumiwa wa ufisadi.

“Ni kweli, kwamba mimi nilikuwa Kigoma. Lakini sikwenda huko kwa kazi hiyo. Nilikwenda likizo,” alisema Kilumbe.

Alipoelezwa kwamba gazeti lina taarifa kwamba safari yake hiyo ilimpeleka hata mikoa mingine, na kwamba kote huko alikuwa anatumia gari la kifahari aina ya Land Cruiser, Kilumbe alisema, “Nilikwenda Kigoma kwa ndege na nikarudi kwa ndege.  Sikwenda Kibondo wala Kasulu; nilikaa palepale Kigoma Mjini..

“Ni kweli nilikuwa natumia magari. Lakini nina gari langu, la ndugu zangu na marafiki. Na usisahau kwamba mimi ni kiongozi wa chama na sikatazwi kutumia usafiri wa aina yoyote,” amejitetea.

Alipoelezwa kwamba inawezekana alikutana na walengwa mjini Kigoma, Kilumbe alisema, “Hivi nishiriki kwenye mpango huo dhidi ya Sitta kwa manufaa gani? Hayo ni mambo yaliyozushwa tu.”

Kwa upande wake, Chitanda amesema hajawahi kusikia madai hayo hata mara moja.

Mwandishi: Kuna madai kuwa wewe ni miongoni mwa makatibu wa CCM wa mikoa, mnaopita na kushawishi wajumbe wa NEC kumfukuza Spika Sitta uanachama. Ni kweli?

Chatanda: Mmepata taarifa hizo kutoka wapi?

Mwandishi: Kutoka vyanzo vyetu vya habari.

Chatanda: Kwanza sijawahi kusikia taarifa hizo, ndiyo kwanza nazisikia kutoka kwako.

Mwandishi: Hivi karibuni ulikuwa na likizo. Inadaiwa ulikwenda katika baadhi ya mikoa na lengo la safari hizo lilikuwa kutekeleza jambo hilo. Ni kweli?

Chatanda: Si kweli. Kwanza mimi sijapata likizo hivi karibuni. Ninachofahamu, majuzi nilikwenda mkoani Tanga kumzika Mkuu wa Kitengo cha Usalama na Maadili. Nilizika na kurejea kituoni kwangu siku hiyohiyo.

Mjumbe mmoja wa NEC ambaye anatoka katika kundi la wapigavita ufisadi amethibitishia MwanaHALISI, kwamba mpango huo upo na unafahamika hata kwa viongozi wa juu wa CCM akiwamo Rais Jakaya Kikwete.

MwanaHALISI imeambiwa kwamba taarifa za Sitta kung’olewa tayari zimemfikia mwenyewe, na kwamba alilieleza suala hilo kwa Rais Kikwete walipokutana ikulu wiki mbili zilizopita.

Imeelezwa kuwa Sitta alimuuliza rais, “Unajua kwamba viongozi wako wanatembelea mikoani kutaka kunifukuza katika chama?” mtoa taarifa anamnukuu Sitta akimuuliza rais.

Lakini Spika Sitta akiongea kwa simu kutoka Dodoma alisema amesikia hilo, bali kwa sasa anachofanya ni kusimamia sera za CCM na kuendesha bunge bila upendeleo.

Alisema, “Mimi natekeleza misingi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kusimamia haki na usawa katika jamii. Wenye mpango huo, kama kweli wapo, ninawatakia mafanikio mema.”

Spika Sitta ndiye aliunda Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba wa kufua umeme wa dharura kati ya Tanesco na kampuni ya Richmond Development Company (LLC) ya Marekani. Kamati iliongozwa na mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe.

Mapendekezo ya Kamati ndiyo yalizaa maazimio 23 ya Bunge ambayo yalikabidhiwa kwa Waziri Mkuu ili serikali iweze kuyatekeleza. bado inayapiga danadana.

Kauli za “Sitta hafai” zilisikika zaidi kwenye mkutano wa bunge wa Agosti mwaka jana. Baadhi ya wabunge walisema Sitta “anasaliti wenzake na anaangamiza chama.”

Shutuma zilipoongezeka, Sitta aliibuka na kusema bungeni kuwa hawezi kukubali watu waibe halafu bunge linyamaze. Aliongeza kwa mshangao, “Wanataka bunge hili liwe bunge poa.”

Gazeti hili limethibitishiwa kuwapo kwa mpango wa kumng’oa Sitta na kwamba wahusika watatumia vikao vya CCM kuufanikisha.

Malalamiko dhidi ya Sitta yalitanda katika moja ya vikao vya Kamati Kuu mwaka jana. Aliyepeleka malalamiko hayo alikuwa Haji Omari Kheri, mwakilishi wa Tumbatu na Katibu wa wajumbe wa CCM katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Hata hivyo, mwenyekiti, Rais Kikwete aliepusha mjadala kuhusu suala hilo kwa kusema panahitajika siku nzima “kujadili masuala hayo ya bunge.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: