Mpinga umoja unaojengwa Z’bar ndiye shetani


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 16 June 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

MAKADA wa Kisonge wanasema: TANU na ASP ndio walioleta umoja wa kitaifa. Hatudanganyiki; hapana hapana.

Usemi huu ulioandikwa kwenye ubao wa matangazo wa maskani yao iliyopo Michenzani, mjini Zanzibar , unahamasisha watu kukataa kura ya maoni itakayopigwa 31 Julai Zanzibar .

Ni matokeo ya vijana wasiojua historia ya kweli ya nchi yao . La kama wanaijua, basi wanaivuruga makusudi kwa kudhani wao wana haki zaidi Zanzibar kuliko wengine, wakiwemo wale wenye asili ya vizazi vinne, vitano na kuendelea.

Kabla, waliandika, “Kula mseto ni hiyari ya mtu siyo lazima; hatudanganyiki; hapana.”

Maudhui ni yale yale: hawataki mabadiliko ya mfumo wa utawala itakapokuja kura ya kuamua pendekezo la Zanzibar kuwa chini ya serikali ya umoja wa kitaifa.

Makada wa Kisonge hawataki kinachotakiwa na chama chao – ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro wa kisiasa uliogharimu maisha ya watu, mali zao na thamani ya utu kwa wengine. Wanataka kura ikwame ili nchi ibaki katika mifarakano na wao wajinufaishe kupitia matumizi mabaya ya madaraka kama vile watu wa Unguja na Pemba wanehulukiwa kuongozwa na kikundi tu cha watu tena kwa kuvunja sheria za nchi na za kimataifa.

Hawataki kuiona Zanzibar inapata maendeleo ya kasi kwa kuchangiwa na kila mwananchi – badala ya yale ya kusuasua yanayochangiwa na sehemu tu ya jamii.

Mbali na maoni ya makada hawa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuitazama nchi kwa jicho la husda zaidi, nabaini tatizo jingine kubwa.

Kwamba wengi wa vijana – ninaamini ndio wenye ushawishi mkubwa katika kuamua nini kiandikwe ubaoni – wanaoidhinisha kuandikwa kwa matamshi ya kihafidhina, inaonekana hawajui historia ya nchi yao .

Wanadhani historia ya Zanzibar ilianzia 11 Januari 1964, siku ya mkesha wa mapinduzi yaliyokuja kwa kaulimbiu ya kuondoa utawala wa Kisultani.

Naona hawajui hata nani walishiriki mapinduzi; nani na nani waliunda serikali baada ya mapinduzi; na hawajui malengo ya mapinduzi yale.

Iweje waseme TANU na ASP ndio walioleta “umoja wa kitaifa” wakati serikali ya uhuru ilijumuisha watu wa makabila tofauti? Sijui kama wanajua kulikuwa na mawaziri mchanganyiko.

Kulikuwa na mchanganyiko wa karibu nusu kwa nusu katika Baraza la Mawaziri la serikali iliyoundwa na Waziri Mkuu Mohammed Shamte Hamad (Mpemba wa Chonga), baada ya uhuru wa Zanzibar wa 10 Desemba 1963.

Walikuwepo Maulid Mshangama na Ibuni Saleh (Wangazija), Haji Muhamadi (Mtumbatu wa Mkokotoni), Juma Aley (amechanganya), Salim Kombo Saleh, (Mpemba aliyefia Kijichi Bububu, Aprili mwaka huu), Abadhar Juma Khatib (Mpemba), Ali Muhsin Barwany na Idarus Baalawy (Waarabu, mmoja wa Unguja na mwengine wa Pemba), Ameir Tajo (Mmakunduchi), Rashid Hamad (Mpemba wa Ole, aliyekuwa kiongozi wa Hizbu Pemba.

Mabalozi walikuwa mchanganyiko akiwemo Ali Abdalla Khamis (Spika wa Baraza la Wawakilishi 1980-1995).

Lakini watazame nani walikuwa mawaziri katika serikali ya kwanza baada ya mapinduzi. Nini kilitendeka baada ya mapinduzi? Ni Waarabu watupu walioumizwa? Au wengi wa waliokuwa wanaharakati wa kisichokuwa Chama cha Afro-Shirazi Party (ASP), wakiwemo waliokuwa makomredi chini ya Umma Party?

Sijawahi kuhoji vitu hivi maana havikuwa na maana sana . Ninajali mustakbali wa nchi. Naingia kwa sababu naona kunajitokeza vijana wapotoshaji wa historia kwa makusudi yao .

Fikra zao zinawafikisha kutoa matamshi ya ovyo; hayafai. Ni kueneza kasumba; haziwafai Wazanzibari wala Watanzania, si watu wazima wala vijana wa leo. Hawajijui.

Harakati kama zao zimelengwa kufutwa na dhamira njema waliyoiweka Rais Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF na Waziri Kiongozi wa zamani wa Zanzibar , Maalim Seif Shariff Hamad.

Viongozi hawa wamekubaliana kwa moyo mmoja kujenga Zanzibar njema. Kuondoa maovu na makovu ya mambo yaliyopita. Kuondoa chuki baina yao na baina ya vyama wanavyosimamia.

Wao wanajua siasa chafu haziendelezi nchi na hazijengi maendeleo ya watu. Siasa chafu hazikufaa – maana ukweli ziliichana na kuipasua nchi – wakati ule na hazifai tulipo wala twendako.

Wote wameuona ukweli kwamba kisasi hujenga mazingira ya kulipiza kisasi na kwa hivyo huzaa kisasi na kinachozaliwa baadaye huwa ni kuendelea kulipiza kisasi.

Ni elimu muhimu ya kihistoria kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla kuwa Zanzibar haikupata kusumbuliwa na tatizo la ukabila hasa. Tatizo ilikuwa ni nani alipenda chama cha ASP na nani alikipinga.

Kwa wasioelewa, wakiwemo wahafidhina vijana wa Kisonge, wazazi wa viongozi wengi wa CCM na baadhi ya viongozi wa juu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar walikuwa viongozi au wanachama mashuhuri wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP) au Hizbu kwa umaarufu wake, na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP).

Wafanye tu utafiti watajua. Wasije kushangaa wakakuta hata wao kumbe wazazi wao waliunga mkono Hizbu.

Mabadiliko ya mfumo wa utawala yanayotakiwa yanataka wananchi wote bila ya kujali asili zao washiriki kikamilifu na kwa uwazi katika kuijenga Zanzibar . Iwe nchi inayong’ara kiuchumi, kielimu na kiutamaduni kama ilivyopata kuwa hadi miaka ya 1970.

Zanzibar ilikuwa nchi ya juu katika nyanja hizi ikifuatana na Misri na Ghana . Mamia ya watu kutoka Tanzania Bara, Kenya, Uganda, Malawi, Afrika Kusini, Msumbiji, Yemen, Oman, Ghuba, Pakistan, India na kwengineko walikuja kwa masomo na kutafuta maisha. Ndio maana Zanzibar ina machanganyiko wa watu.

Zanzibar ni nchi ya kila mtu aliye halali Mzanzibari kisheria. Inajulikana ilivyo toka zamani. Nchi inayoundwa na jamii za watu kutoka sehemu mbalimbali duniani. Kila mmoja alikuja kwa sababu yake. Wote walitaka maisha mema.

Ni ujinga tu mtu kusema leo mabadiliko yanataka kuvunja muungano. Upi lakini? Kwa Zanzibar, muungano ni jambo linalofahamika hata kabla ya 26 Aprili 1964. Watu wake wameoana na Watanganyika kabla hapo. Wapo waliooana wakiwa Unguja au Pemba . Lakini wapo waliooa na kuolewa na hata kujukuu Tanganyika kabla ya uhuru wa 9 Desemba 1961.

Mtu mmoja amenisimulia alivyooa Kilwa mwaka 1946 na aliwajua wengine waliokuwa wakifanya biashara ya miti ya kujengea ya Simba Uranga waliofanya hivyo kabla yake. Huyu alikuwa kinda la Kizanzibari miaka hiyo ambaye alipata kusafiri kwa jahazi kwenda Kilwa. Akakaa kwa muda. Akafanya kazi ya uvuvi na baadaye akaoa Kilwa. Ana watoto na wajukuu tele.

Huyu anasimamaje ukivunjwa muungano wa 1964? Watoto wake ni wa kabila gani? Wandingo au Wamakunduchi? Hivi leo zaidi ya robo ya familia za Wazanzibari zipo Bara na Visiwani, utaona baba yupo Unguja mjini, mama Dar es Salaam na mjukuu Tanga. Ni ujinga tu kueneza kasumba za kikabila karne hii.

Nimesimuliwa kwamba Arusha alikuwepo mzee Anwar (akikaa Kaloleni) na umaarufu wake akiitwa Muunguja. Pembezoni mwa mtaa aliokua akiishi, paliitwa Unguja kabla ya Tanganyika kupata uhuru.

Alikuwa sahiba mkubwa wa familia zenye asili ya Arusha kama za kina Mzee Ngororo, Kihago, Mkindy na Zidikheri. Mzee huyu alihamia Arusha mwaka 1937 na akifika Unguja mara moja tu tagnu hapo miaka ya mwisho 1970 na watu aliokuwa anawajuwa aliweza kuhesabu vidoleni.

Wazanzibari wengi waliondoka Unguja au Pemba miaka ya 1950, hata kabla ya siasa, wakahamia Mrima. Walioa. Wamezaa na wanawake wa karibu kila mkoa wa bara.
Hiyo ndiyo historia ya kweli. Hatuwezi kurudi wala kurudishwa nyuma kwa kasumba za kitoto. Watu wanataka maendeleo si mifarakano ambayo haizai isipokuwa chuki na hasama. Matunda yake ni ushetani na usaliti. Hatuwezi kurudi nyuma. Mbele tu.

Wazanzibari watakwenda mbele wakikubali kura ya maoni kwa kutia NDIYO siku ya uamuzi; 31 Julai. Muungwana hupenda umoja na asiyeupenda mchawi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: