Mponda asulubiwa, MSD wanaponaje?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 April 2012

Printer-friendly version

MKUTANO wa saba wa Bunge umemalizika huku mawaziri kadhaa wakitakiwa kujiuzulu. Miongoni mwa mawaziri hao ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda.

Waziri Mponda alikabwa koo na kila mbunge aliyepewa nafasi ya kuchangia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu madudu katika Bohari ya Madawa (MSD).

Mawaziri wengine walishambuliwa na hata kutakiwa kujiuzulu baada ya kamati mbalimbali za bunge kutoa ripoti zinazoonyesha wizi, ubadhirifu na ufisadi mwingi katika wizara na hata mawaziri wengine kuhusishwa.

Waliokumbwa na dhahama zaidi ni Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo; Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige; Waziri wa Tamisemi, George Mkuchika; Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami; Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,   Prof. Jumanne Maghembe.

Wizara hizo pia zimefanyiwa ukaguzi wa kina na CAG na ripoti imebainisha uoza katika maeneo mengi lakini waliomponza Dk. Mponda ni watendaji wa MSD.

Ripoti ya CAG iliyoandaliwa kwa utaalamu mkubwa inaonyesha katika jedwali namba saba kuna dawa zenye thamani ya Sh. 8.4 bilioni ambazo muda wa matumizi yake umeisha zikiwa kwenye bohari.

CAG ameonyesha pia katika ripoti yake kuwepo tofauti kubwa kati ya mali halisi iliyopo na takwimu zilizopo kwenye vitabu kwa kiasi cha Sh. 2,08 bilioni.

Kasoro hii si ya bahati mbaya imetengenezwa na watu kwa makusudi. Kasoro nyingine iliyotajwa na CAG na ambayo imetengenezwa kwa makusudi na watendaji ni upungufu mkubwa wa dawa muhimu kama absorbent surgical gauzes, quinine,  dawa mseto ya malaria (ALU) na uwepo wa mashine za kupimia mapigo ya moyo (BP) zisizo na ubora.

Kitu kingine kilichomo katika ripoti ya CAG ni ukaguzi wa zabuni tisa ambazo zilionekana kuwa hazikuwa katika Mpango Kazi wa manunuzi ya mwaka. Kiasi cha Shs. 2.9 billioni, USD 9.4 millioni na EURO 99.6 elfu kilitumika nje ya Mpango Kazi huo.

Ripoti ya CAG imeonyesha pia kuwa kulikuwa na uvunjifu wa sheria namba 69(7) ya sheria ya manunzi ya mali ya umma ya mwaka 2004 ambayo inaharamisha ununuzi wa kutoka kwa muuzaji mmoja au ‘single source’.

Kiasi cha manunuzi ya ‘single source’ kilikuwa Sh. 20 milioni, USD 4.6 milioni na Euro 1.54 milioni. Kasoro nyingine iliyotengenezwa kwa makusudi na ambayo CAG aligundua ni mikataba ya thamani ya Sh. 3.95 bilioni, USD.9.4 milioni na EURO 1.5 milioni ambayo ilifanyika bila ya kuthibitishwa na Bodi ya Zabuni ya MSD. Utaratibu huu ni uvunjaji wa kifungu 30 cha sheria ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2004.

Wakati madudu yote haya yakifanyika na kuisababisha hasara serikali, bado CAG akagundua dawa zenye thamani ya Sh. 5.0 bilioni zimehifadhiwa kwenye maghala ya MSD zikisubiri kibali cha kuharibiwa.

Dawa hizi ziliingia nchini mwaka 2010/11 na ni mbali ya zile zilizofutwa mwaka jana ambazo zilikuwa na thamani ya Sh. 4.0 bilioni na ambazo zilikusanywa kuanzia mwaka 2002 hadi 2008.

Hata katika kipindi cha Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya mwaka 2011/ 2012 kulikuwa na mjadala mkali juu ya utendaji wa chombo hiki nyeti katika sekta ya afya.

Wabunge waliopata fursa ya kuchangia hotuba ya wizara ya afya walihusisha uharibifu wa dawa na utendaji mbovu wa taasisi hii.

Mjadala wa mwaka jana haukuwa mkali kama mwaka huu kwa vile Waziri Mponda alikuwa mpya na hakuwa amemaliza hata mwaka. Dk. Mponda aliahidi kuifanyia mabadiliko MSD ili kuleta ufanisi katika utendaji.

Uchunguzi unaonyesha kuwa mabadiliko yaliyofanyika ni kufanya uhamisho wa ndani. Mathalani waliohusika na ununuzi mbaya wa dawa wamehamishwa toka idara zao walizokuwa wanasimamia na kupelekwa idara nyingine.

Kutokana na madudu mengi kutopatiwa tiba na ukweli kwamba mpaka sasa Bodi inayosimamia MSD bado haijampata Mkurugenzi wa Manunuzi kutokana na sababu zisizojulikana, wabunge wamekuwa mbongo na kwa kuanza wametaka Waziri Mponda aachie ngazi.

Wakati waziri anajiuzulu kutokana na uzembe na hata ufisadi ndani ya MSD, watendaji waliosababisha hasara hii wanasubiri nini ofisini? Kwanini hawa wasiwe wa kwanza?

Je ni sahihi kweli watu ambao wamelitia hasara taifa ya mabilioni ya shilingi kupewa shukrani kwa kupangiwa kazi zingine?

Je, ni hatua gani wizara itachukua kuhakikisha wahalifu waliosababisha hasara hiyo wanafikishwa mahakamani ili kuweza kuleta uwajibikaji katika mali ya umma na usimamizi wa fedha zitolewazo na wafadhili?

Je, wizara haioni sasa kuwa umefika wakati ikaivunja Bodi ya Wadhamini ya MSD pamoja na menejimenti ili kuleta ufanisi katika utendaji?

Kama wizara inashindwa kufanya haya vyombo kama PPRA, TAKUKURU na Usalama wa Taifa visaidie kuzuia hasara zaidi.

Baada ya sekeseke kubwa kutokea bungeni litakuwa jambo la busara serikali ikafanyika kazi ripoti ya CAG au ikafanya uchunguzi maalumu kuhusu tatizo la dawa zenye thamani ya Sh. 5.0 bilioni kwisha muda wake wa matumizi kwa mwaka mmoja ili  wahusika wawajibike kwa ufisadi au uzembe waliofanya.

Katika makala niliyoandika mwaka jana nilihoji hatua ya wakandarasi wanaopewa mikataba kuleta shehena ya dawa ambayo ina muda mfupi wa kutumika nchini.

MSD imejiwekea utaratibu wa kupokea dawa ambazo zimebakiza asilimia 80 ya muda wa matumizi. Mfumo huu unaligharimu taifa kwani matokeo yake ni dawa nyingi kutotumika.

Mfumo huu umejenga mazingira ya rushwa na kwamba watendaji wasio waaminifu wanaweza kupokea hata dawa ambazo muda umebakia kidogo sana mradi tu wapate rushwa. Watendaji wasio waaminifu ni rahisi kushiriki ufisadi unaoitia hasara nchi.

0
No votes yet