Mr. II apeleka rap bungeni


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 03 November 2010

Printer-friendly version
Joseph Mbilinyi, mbunge wa Mbeya mjini

HISTORIA imeandikwa. Alipotangaza dhamira yake kutaka kuwania ubunge katika jimbo la Mbeya Mjini miezi minne iliyopita, wengi walifikiri kuwa ni utani na mzaha wa mwaka.

Akaidhinishwa na chama chake, akachukua fomu na mara alipoanza kampeni, mamia kwa maelfu ya watu, wazee kwa vijana, wake kwa waume walifurika kumsikiliza na ilipofika siku ya kupiga kura hawakumwangusha.

Leo hii, Joseph Mbilinyi, mwanamuziki wa muziki wa kufokafoka (rap) maarufu kama Mr II au Sugu ametangazwa mbunge mteule katika Jimbo la Mbeya Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kitu kinachofurahisha ni kwamba Sugu amemwangusha mbunge mzoefu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Benson Mpesya. Lakini zaidi, Sugu amembwaga aliyekuwa mwalimu wake.

Mr II ameandika historia kuwa msanii wa kwanza wa rap kutinga bungeni. Huko atakutana na mwimbaji kwaya na Mkurugenzi wa TOT, John Komba.

Sugu ambaye ni miongoni mwa wasanii wa kwanza kutunga na kuimba vibao vya rap amekuwa mtetezi wa wanamuziki wengine wasinyonywe na wanaoitwa maprodyuza na mawakala. Hata hivyo, ujumbe huo mwema haukusikika.

Hivi karibuni wakati akifikia uamuzi wa kuwania ubunge, tayari alikuwa ameingia kwenye matatizo na vyombo vya dola kuhusu albamu yake aliyoitoa mwaka huu ya Anti Virus.

Kwenye albamu hiyo, Sugu alidaiwa kutishia maisha ya promota maarufu wa muziki nchini, Ruge Mutahaba, kwenye wimbo wake wa “Wanna Kill”.

Ugomvi huo ulikuja baada ya Sugu kufanya mazungumzo na mapromota wa Marekani katika tamasha la kupambana dhidi ya malaria lililojulikana kama “Malaria No More” au Malaria Haikubaliki.

Lakini wakati akisubiri Wamarekani waje nchini, alishtukia tamasha hilo likiandaliwa na Ruge aliyetia saini mkataba huo. Sugu alilalamikia kuporwa haki yake, lakini hakusikilizwa na badala yake alifikishwa kortini. Sugu aliyewahi kuachana na muziki huyo kutokana na uonevu mwingi, aliamua kujiingiza katika masuala ya siasa na alipopata fursa akajitosa mjini Mbeya.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa walidhani kwamba Sugu asingefanikiwa kutokana na ukabila wa hali ya juu katika mkoa huo. Vilevile ilifikiriwa kwamba kama angeungwa mkono basi ingekuwa mjini, lakini amepata uungwaji mkono wa hali ya juu mjini na vijijini.

Matokeo ya kura zilizopigwa Jumapili yanaonyesha alipata kura 46,411 huku akimwacha mwalimu wake na kura 24236.

Matokeo hayo yalitangazwa baada ya polisi kulipua ya machozi na kuwarushia maji ya kuwasha dhidi ya maelfu ya mashabiki wake waliokusanyika kusubiri kutangazwa kwa matokeo hayo.

Huo ndiyo ubatizo wa kisiasa ambao Sugu ameanza nao. Na pengine, huu ndiyo mwanzo wa safari ndefu ya kisiasa ya Mbilinyi kutetea haki za watu siyo kwa njia ya muziki bali bungeni.

Ushindi wake umedhihirisha kwamba Mbilinyi ni sugu kweli na washabiki wa muziki wa kizazi kipya hawakukosea kumpa jina hilo.

Swali kubwa ambalo wengi walijiuliza wakati alipotangaza nia yake hiyo lilikuwa ni; kwa nini ameamua kujitosa kwenye siasa?

“Kwa muda mrefu katika maisha yangu ya kimuziki pamoja na kuimba nyimbo za kuburudisha nimekuwa zaidi mstari wa mbele kuimba nyimbo za kutetea haki za makundi mbalimbali katika jamii na taifa kwa ujumla.

“Wakati umefika sasa wa kuhamisha jukwaa la mapambano ya kudai haki kutoka jukwaa la muziki mpaka jukwaa la siasa kwa dhamira ile ile ya kutumia kipaji changu alichonijalia Mwenyezi Mungu kuimba na kuhutubia kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya kweli katika taifa letu.

“Nyimbo zangu zimekuwa zikibeba sauti ya watu wasio na sauti ili zisikike na watawala; lakini hata hivyo kwa kipindi chote ambazo nimekuwa nikifanya harakati hizi watunga sheria na wafanya maamuzi ya kisera chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameshindwa kuongoza vizuri taifa kuweza kufanya mabadiliko ya kweli yenye kuhakikisha watanzania wananufaika na vipaji vyao ambavyo Mwenyezi Mungu amewajalia na taifa linanufaika na rasilimali na maliasili ambazo tumejaliwa kuwa nazo.

“Natambua kwamba kwa muda mrefu Mbeya Mjini yetu ina kero ya umeme wakati ambapo tupo jirani na Mgodi wa Kiwira ambao ungeweza kuzalisha umeme wa kututosheleza lakini kutokana na ufisadi tunashindwa kuondokana na hali hii ambayo inasababisha ugumu na kupanda kwa gharama za maisha na kukosa taa za barabarani hali ambayo inaweka mazingira ya kuongezeka kwa uhalifu.

“Natambua kwamba viwanda vyetu vya Mbeya Mjini vimeuzwa kwa bei chee na vingine vimeshindwa kuendeshwa na kubaki magofu na kusababisha vijana kukosa ajira na uchumi kuathirika kama ilivyokuwa kwa viwanda vya pamba, mafuta na nyama,” alisema Mbilinyi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Julai 29 mwaka huu.

Je, Watanzania na hasa wananchi wa Mbeya Mjini watarajie nini kutoka kwake mara baada ya kuchaguliwa kwake kuwa mbunge?

Anasema, “Jiji la Mbeya linakabiliwa na ubovu wa barabara ukiondoa barabara kuu inayokwenda Tunduma, barabara za mitaani ni mbovu wakati ambapo kuna fursa ya kuwa mkoa wenye makaa ya mawe ambayo mabaki yake yangeweza kutumika kukarabati barabara za mitaani Uyole, Soweto na kwingineko.

“Natambua kwamba wafanyabiashara wa Mbeya Mjini wana malalamiko mengi kuhusu kubambikiwa kodi huku wafanyabiashara wadogowadogo wakiwa wananyanyaswa katika maeneo wanayofanyia biashara kwa kuwa hata mimi mwenyewe nimewahi kuwa mfanyabishara katika soko letu la Mwanjelwa.

“Natambua kwamba jiji letu la Mbeya ni kitovu cha elimu katika mkoa wetu hata hivyo lugha zinazotolewa na uongozi wa mkoa zinadhalilisha walimu wakati uongozi huo unashindwa kuweka mazingira bora ya elimu na kusababisha Mbeya kuanza kudorora kielimu. Kwa upande mwingine, kadiri mji unavyopanuka ndivyo kero ya usafiri wa wanafunzi inakithiri na shule za pembezoni zinakosa walimu.”

Sugu anakuwa mwanamuziki wa kwanza wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini kuwa mbunge. Ingawa John Komba ni msanii wa kwaya, kuingia bungeni, kwa Mr. II kunamaanisha ingizo la maslahi na tamaduni za kizazi kipya cha vijana ndani ya bunge lijalo la Tanzania.

Wasanii wenzake wa muziki wa kizazi kipya watarajie nini kutoka kwake baada ya kuingia bungeni?

Anajibu, “Mimi ninajulikana tangu zamani kuwa ni mbishi kwenye kutetea na kudai haki za wanaonyonywa. Harakati zangu za siku zote za kupambana na wanyonyaji dhidi ya maslahi ya wasanii Tanzania zitaendelea ndani ya bunge na sasa nitazipeleka katika kiwango kingine,” alisema katika taarifa yake hiyo kwa waandishi wa habari.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: