Mrema atamani kurudia ushushushu


Editha Majura's picture

Na Editha Majura - Imechapwa 06 January 2010

Printer-friendly version
Akiri kuwa katika mtandao wa Kikwete
Alenga upya ubunge Jimbo la Vunjo
Agustine Mrema akisalimiana na Rais Kikwete viwanja vya Ikulu

MWENYEKITI wa Tanzania Labour Party (TLP), Agustine Mrema bado anafanya kazi ya usalama wa Taifa.

Amesema ataendelea kutumia ujuzi na uzalendo aliojengewa na Taasisi ya Usalama wa Taifa kwa maslahi ya Taifa, siyo kwa maslahi ya mtu au kundi lolote.

Aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na MwanaHALISI wiki iliyopita, nyumbani kwake Sinza, jijini Dar es Salaam.

Mahojiano hayo yalitokana na hatua yake ya kuwashambulia kwa maneno waliomkosoa Rais Jakaya Kikwete, kupitia kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, (MNF) lililomalizika 2 Desemba mwaka jana.

“Nilistaafu kutumwa na kulipwa na wale jamaa (Usalama wa Taifa) lakini hakuna anayeweza kuninyang’anya ujuzi na uzalendo niliojengewa. Naendelea kutumia profession (taaluma) yangu kwa maslahi ya taifa,” anaeleza Mrema.

Swali: Hii kazi ya usalama wa taifa ulisomea wapi?

Jibu: Siwezi kukwambia. Hiyo ni siri kwa ajili ya usalama.

Swali: Ulifundisha wapi usalama wa taifa?

Jibu: We, mama vipi? Siwezi kutaja hiyo kwa usalama wa nji!

Swali: Kwa muda gani ulifanya kazi hii?

Jibu: Miaka mingi, tangu nikiwa mwalimu wa shule.

Swali: Ni wapi ulifanya kazi hii?

Jibu: Sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa mkuu wa usalama wa wilaya na katibu msaidizi Tume ya Ulinzi na Usalama ya CCM.

Taarifa za kuaminika, hata hivyo, zinasema Mrema alipata mafunzo ya usalama daraja la chini (Juniour Course) na kwa muda mfupi katika chuo cha Malindi, Mbweni wilayani Bagamoyo katika miaka ya 1970.

Wafuatiliaji wa nyendo za Mrema watakumbuka kuwa alipokuwa mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, hakujivunia ushushushu, badala yake alizunguka nchi nzima akisema kuwa mpinzani wake mkuu, Katibu Mkuu Mabere Marando ndiye alikuwa “mtu wa usalama.”

Kwamba Mrema amekumbuka kile anachoita kazi yake ya zamani na “aliyosomea,” ni hoja mpya inayoweza kuhusishwa na “toba ya kisiasa” kuelekea uchaguzi mkuu ambapo yeye anataka kugombea ubunge jimbo la Vunjo.

Hata hivyo, bila kutoa maelezo kamili, Mrema anasema hali ya nchi kiusalama ni “mbaya kuliko mtu yoyote anavyoweza kufikiri.”

Anawaelezea walioshiriki kongamano la MNF na kumkosoa Kikwete kuwa dhamira yao si nzuri na kwamba wanalenga kumchonganisha Kikwete na raia anaowaongoza.

Anasema kama tatizo ni ufisadi kweli, haukuanzia kwenye utawala wa Kikwete, akiongeza kuwa afadhali rais huyu amethubutu kuchukua hatua za kukabiliana nao. Akahoji kama hata hilo hawalioni.

Anatoa mifano ya mawaziri katika awamu zilizopita ambao wizara zao zilihusika katika ufisadi lakini hawakuchukuliwa hatua.

Anasema wizara ya ujenzi ilinunua kivuko kibovu; hakuna hatua iliyochukuliwa; nayo wizara ya mawasiliano ilinunua ndege mbovu lakini waziri akaendelea “kupeta” katika nafasi mpya.

“Wote hao wanaosimama hadharani kumchachamalia Kikwete walikuwepo wakati yote hayo yakitendeka, mbona walikaa kimya wakati huo? Wasituletee unaa bwana! Wale wana lao jambo,” alieleza Mrema

Alipotakiwa kusema hilo jambo ni nini, alisema ni wivu na chuki kwa sababu baadhi ya wanaopiga kelele dhidi ya Kikwete waliwania urais mwaka 2005, wakashindwa. Wengine ni wapambe wao.

Mrema anasema kuwa anashangazwa na kundi hilo kuendekeza chuki hadi kufikia kusahau hata misingi ya sheria za nchi inayozuia kauli zenye lengo la kumchonganisha rais na raia anaowaongoza.

Mrema aliwahi kuwa waziri wa mambo ya ndani na naibu waziri mkuu wakati wa serikali ya awamu pili. Aliwahi pia kuwa mbunge wa majimbo ya Vunjo na Temeke.

Anadai kuwa alishika nyadhifa mbalimbali kwenye taasisi ya usalama wa taifa, ukiwemo wa afisa wa wilaya.

Siku 27 baada ya kongamano la MNF kumalizika, Mrema alifanya mkutano na vyombo vya habari, akamtetea Rais Kikwete dhidi ya tuhuma na kasoro zilizoelezwa kwenye kongamano hilo ambalo naye alihudhuria.

Miongoni mwa mambo yaliyoelezwa na Mrema kuwa ni kero kwa usalama ni kauli iliyotolewa kwenye mkutano huo, kwamba “Kikwete azifanyie kazi kasoro hizi la sivyo, mwaka kesho (mwaka huu) tutamtosa.”

Aidha, anasema waliomtaja rais kwa jina na kusema amezungukwa na wezi, wametenda kosa kwa mujibu wa sheria ya uchochezi na ikithibitika kimahakama, adhabu yake ni kifungo cha miaka saba jela.

Kuhusu Mrema kuwa kibaraka wa CCM kutokana na kauli zake za sasa za kufanya kinachoonekana kuwa ni “kumtetea” Kikwete, alisema:

“Watu wanadai mimi ni kibaraka wa CCM, kwa sababu sijatiwa kikaangoni, profession (taaluma) ya usalama wa taifa inanisaidia,” anajitapa Mrema.

Mrema anashangazwa na aliowaita “wanasiasa uchwara” kwamba wanapata wapi jeuri ya kutamka jina la rais hadharana na kudai watamtosa asipochukua maamuzi magumu.

Anawataka wao ndio wachukue uamuzi mgumu kwa kukihama CCM na kwamba kiusalama neno “tutamtosa rais” ni zito na wahusika walistahili kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kuhusu kauli zake kutafsisiriwa kuwa yeye ni mmoja wa wanamtandao wa kumsaidia rais katika uchaguzi ujao, Mrema alisema,

“Sina sababu ya kuwa katika mtandao wowote. Lakini kwa sababu rais amewekwa madarakani kwa mujibu wa Katiba halali ya nchi; na amechaguliwa na Watanzania, ni lazima kila Mtanzania awe katika mtandao wake. Mtandao wowote kinyume na ule wa rais, kama upo, ni uasi.”

Alipoulizwa iwapo hatua yake hiyo haikutokana na kuahidiwa kuwezeshwa na CCM kupata ubunge Vunjo, Mrema alikana.

“Huo ni upuuzi kama upuuzi mwingine kwamba nimehongwa, nimeahidiwa kufadhiliwa; wengine wanahoji kwa nini sipigwi virungu na polisi; eti mimi ni kibaraka wa CCM. Kwa taarifa yao, uwezo wa kuwakilisha jimbo la Vunjo bila kusaidiwa na CCM ninao na nitashinda,” alisema kwa njia ya kujigamba.

Mrema amepuuza madai hayo na kusema wenye hoja zilizojikita katika “taaluma ya Usalama,” wampinge kwa misingi hiyo kwa lengo la kuweka taifa salama.

Katika hali ambayo haikutegemewa, huku akiwa bado mwenyekiti wa TLP, Mrema anasema kuwa amevuka “mipaka ya vyama vya siasa” na kujikita kwenye taaluma yake ambayo amesema hataacha kuitumia “kuliepusha taifa na balaa linalolinyemelea.”

Swali: Umesema umetoka viwango vya vyama, ina maana unataka kujiuzulu uenyekiti wa TLP?

Jibu: Siwezi kujiuzulu hata nikiwa mwenyekiti wa TLP hainizuii kuzungumzia usalama wa nji wakati nji inataka kusambaratishwa kwa maneno ya uzandiki na kufanya wananchi waandamane kwenda ikulu.

Swali: Au unataka kuhama kabisa kutoka siasa za upinzani?

Jibu: Hapana. Hayo ni mawazo potofu; siwezi kutoka kwenye upinzani na haimaanishi ukiwa kwenye upinzani ndio usambaratishe nchi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: