Mrema: Mwili TLP, moyo CCM


Fao Katabayanga's picture

Na Fao Katabayanga - Imechapwa 27 January 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala
AUGUSTINE Mrema

AUGUSTINE Mrema amefanikiwa mara mbili. Kwanza, amefanikiwa kutetea waziwazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.

Pili, kwa juhudi zake hizo, Mrema amefanikiwa kushawishi wanachama wa chama chake – Tanzania Labour Party – kuanza kwenda au kurejea CCM; tena kwa kasi.

Wabaki TLP kufanya nini wakati kiongozi wao amekuwa mtetezi wa wazi wa uongozi wa CCM na sera zake? Mwili wake uko TLP, lakini moyo wake uko CCM.

Wanachama wafanye nini TLP wakati kiongozi wao, Mrema, anasema bado anafanya kazi ya kulinda watawala; kazi ambayo alipewa na serikali ya CCM na anadai anaijua, anaipenda na kuitekeleza – ushushushu?

Sasa wanachama wa TLP ambao miaka nendarudi wamekuwa wakimsikiliza akitukana na kukandia mashushushu, wamweleweje kiongozi wao anayetamani ufalme wa chama kingine?

Soma hapa: Wanachama 48 wa TLP wamerudi/wamejiunga na CCM. Ni kutoka jimbo la Vunjo ambako ni nyumbani kwa Mrema. Kwa ujinga wao, na hii ni bahati mbaya, wamepeleka kadi zao kwa uongozi wa CCM.

Kadi ni mali ya aliyeinunua. Mtu hana haja ya kupeleka kadi yake kokote. Akihama chama kimoja kwenda kingine, aweza kuhifadhi kadi yake na kuandika historia kwa njia ya kadi.

Kwa mfano, Augustine Mrema anaweza kuwa tajiri wa kadi za vyama. Alikuwa na ile ya TANU. Akawa na ya CCM. Akawa na ya TLP. Akawa na ya NCCR-Mageuzi. Akawa na ya TLP tena. Huenda na nyingine. Tuendelee kuchunguza.

Leo hii, kwa mfano, na kutokana na jukumu alilojipa la kutetea CCM ya Kikwete, Mrema aweza kurudi CCM na kupewa kadi mpya.

Hivyo, kwa msururu wa kadi tu, mtu na tabia yake, aweza kufanyiwa uchambuzi kwa urahisi, hasa leo hii anapokuwa anakiri kuwa bado anatamani na anatumika kama shushushu.

Wanachama wa TLP wanasema wanarudi CCM kwa kuwa hawaoni “maendeleo” katika chama chao. Mrema anasema Kikwete anafanya kazi yake vizuri na kwamba wanaomwandama wanatenda jinai ya “uchochezi.”

Kama Mrema na wanachama wake wanakubaliana, kwa njia na sababu tofauti, kuwa chama ni CCM, kwa nini wabaki TLP? Kwa nini wasubiri kiongozi wao anayesuasua na kufanya kama anabembeleza wakati kuingia CCM ni suala la sekunde tu – papohapo.

Mrema anatafuta upenyo CCM. Anaomba kazi? Anatafuta ushirika na nafuu katika kugombea ubunge Vunjo? Ni yeye mwenye majibu. Amesema mwaka huu anajitupa uwanjani; hivyo yote hayo yanawezekana.

Wanaomfahamu Mrema hawawezi kushangaa. Hakuna ajuaye neno la hekima linalokaririka kimantiki au kifalsafa kutoka kinywani mwa kiongozi huyu wa TLP anayeelekea CCM.

Mbali na majigambo kwamba alikuwa naibu waziri mkuu, cheo alichopachikwa na Mzee Rukhsa (Ali Hassan Mwinyi) kisicho ndani ya katiba ya nchi, Mrema hafahamiki kuwa na mchango kifikra juu ya maendeleo ya nchi na ukabilianaji na changamoto za kisiasa na kiuchumi na kijamii.

Kama mwandishi mmoja alivyowahi kuandika juu ya Mrema, “…jua la kisiasa sasa limezama.” Je, linaweza kuzamia CCM? Kipi cha kujivunia kama si ombwe hadi ombwe na muda unakatika?

Mrema alichomoka CCM akitafuta ngazi ya kupandia kuingia urais. Akaipata: NCCR-Mageuzi. Kwa kujua au kutojua, akaivunjavunja vipande. Bado akataka kufika ikulu.

Sasa imeshindikana. Amechoka. Amekata tamaa. Leo anatamani ubunge Vunjo kwa kuamkia CCM. Si muujiza jua kuzama lilipochomozea. Muujiza ni nani anaona hivyo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: